1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maoni ya wahiriri

29 Machi 2007

Wahariri wa magazeti leo, katika maoni yao wanazingatia mvutano unaoendelea baina ya Iran na Uingereza. Wahariri hao pia wanazungumzia juu ya uamuzi wa baraza la mawaziri hapa nchini Ujerumani kuhusu haki za wahamiaji.

https://p.dw.com/p/CHTN

Juu ya mgogoro unaoendelea kushtadi baina ya Iran na Uingereza kufuatia kukamatwa kwa mabaharia 15 wa Uingereza mhariri wa gazeti la FRANKFURTER ALLGEMEINE anasema Uingereza kwa sasa imesimamisha uhusiano wake na Iran kwa sababu inaamini kuwa mabaharia wake hawakufanya kosa.

Gazeti hilo linatilia maanani kuwa Uingereza imetumia picha zilizopigwa kutokea angani ili kuthibitisha kuwa mashua ya mabaharia hao ilikuwa katika himaya ya Irak na siyo katika himaya ya Iran.

Mhariri huyo anaeleza wasiwasi juu ya shabaha za Iran katika kuwakamata askari hao. Yumkini anasema mhariri huyo utawala wa Iran unakusudia kuwatumia mabahari hao kwa shabaha za kisiasa.

Juu ya mgogoro huo naye mhariri wa gazeti la OSNABRÜCKER anasema, kuwa inapasa kwa waziri mkuu wa Uingereza bwana Tony Blair kuwa na msimamo mkali dhidi ya utawala wa Iran. Kusimamisha mawasiliano na serikali ya mamulah wa Iran ni hatua ya kwanza. Gazeti hilo linaitaka Uingereza ichukue hatua zaidi ikiwa askari maji hao 15 , hawataachiwa haraka.

Anashauri katika maoni yake kuwa nchi zote za Umoja wa Ulaya zisimame pamoja na Uingereza katika kuishinikiza Iran.

Gazeti la FINANCIAL TIMES DEUTSCHLAND linaunga mkono msimamo wa Uingereza kwamba mashua ya nchi hiyo haikuwamo katika himaya ya Iran.

Mhariri wa gazeti hilo anaamini kuwa itakuwa vigumu kwa Iran kuthibitisha vinginevyo, na kwamba hatua iliyochukua kuwakamata askari hao haitashangiliwa hata na rafiki zake.

Katika maoni yao wahariri wa magazeti ya hapa nchini leo pia wanazungumzia juu ya uamuzi wa baraza la mawaziri la Ujerumani juu ya haki ya wahamiaji kuendelea kuishi hapa nchini Ujerumani.

Gazeti la mjini Munic MÜNCHNER MERKUR linasema wahamiaji laki moja wanahusika na uamuzi huo. Anakumbusha kuwa kwa muda wa miaka mingi wakimbizi waliokuwa wanavumiliwa nchini Ujerumani hawakuruhusiwa kufanya kazi. Lakini sasa kufuatia uamuzi wa serikali, watu hao watapewa muda wa mwaka mmoja na nusu ili kutafuta kazi, Atakaefanikiwa kupata ajira ataruhusiwa kuendelea kuishi nchini

Lakini katika upande mwingine uamuzi huo unakaza sukurubu dhidi ya wahamiaji .

Kwa mfano anasema mhariri wa gazeti la SÜDDEUTSCHE ZEITUNG anaeteoroka masomo ya lugha ya kijerumani atapunguziwa posho.Na atakaeolewa ama kuoa mjerumani ili kuweza kuja Ujerumani anapaswa kujua lugha kidogo.

Mhariri anasema huo ni uamuzi mzuri, lakini anatilia maanani kwamba sheria hiyo haitawahusu watu kutoka Marekani, Canada na Japan.

Gazeti linaeleza kuwa ni uamuzi kama huo unaowafayna vijana wa kituruki wahisi kuwa serikali ya Ujerumani inawabagua.

Na Abdu Mtullya