Maoni ya wahariri. | Magazetini | DW | 12.03.2009
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Magazetini

Maoni ya wahariri.

Wahariri wa magazeti wataka sheria kali kudhibiti umilikaji wa silaha nchini Ujerumani.

Kijana alieua watu katika jimbo la Baden Würtemberg jana.

Kijana alieua watu katika jimbo la Baden Würtemberg jana.

Wahariri wa magazeti karibu yote wanazungumzia juu ya mkasa wa kusikitisha uliotokea jana katika jimbo la kusini magharibi mwa Ujerumani,Baden Würtenberg.

Kijana mmoja aliekuwa na umri wa miaka17 aliingia katika shule moja iliyopo katika mji wa Stuttgart, kusini magharibi mwa Ujerumani, na kuanza kufyatua risasi kila upande. Aliua watu 16 wanafunzi na walimu kabla yeye mwenyewe kupigwa risasi na polisi.

Sasa watu wanauliza ilikuaje, kwa nini,nani anabeba dhamana ya kosa hilo.

Mhariri wa gazeti la Südkurier anasema jambo moja limeshabainika wazi kabisa kwamba kijana huyo alipata silaha kutoka kwenye kabati la baba yake.


Mhariri huyo anakiri katika maoni yake kwamba kila kitu ni halali kabisa juu ya silaha aliyotumia kijana huyo, kwa sababu Iliorodhoshwa kwa mujibu wa sheria. Lakini anasema,silaha hiyo ilikuwa mahala ambapo iliweza kuingia katika mikono ya mtu asiestahili kuipata.

Ndiyo sababu mhariri huyo anataka sheria za kudhibiti umilikaji wa silaha ziwe kali zaidi.

Gazeti la Neue Westfällische pia linasisitiza hayo.

Lakini mhariri wa gazeti hilo anasema, kabla ya kuanza kupitisha sheria kali,lazima watu waulize, kwa nini silaha nyingi zinazunguka katika mikono ya watu nchini.

Mhariri amekariri takwimu za polisi zinazoonesha kuwa bunduki na pistola milioni10 zimeorodheshwa kisheria, lakini nyingine milioni kumi zimo katika mikono ya watu kinyume cha sheria.

Pamoja na hayo mhariri anatilia maanani kwamba mlikuwa na bunduki 15 nyumbani kwa wazazi wa kijana muuaji.

Gazeti la Cellesche nalo pia linatoa mwito wa kupitishwa sheria kali.Lakini gazeti hilo linasema sheria hizo lazima zitekelezwe kwa moyo wa dhati.

Na mhariri wa gazeti la Abendzeitung, anasema ili kuepusha maafa kama hayo yaliyotokea katika mji wa Stuttgart pana haja kwa walimu na polisi kutafakari njia za kuwasaidia vijana wenye mwelekeo wa kuwa hatari.