1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maoni ya wahariri

12 Julai 2007

Katika maoni yao wahariri wa magazeti leo wanazungumzia juu ya kuachiwa mwananchi wa Ujerumani bibi Hannalore Krause baada ya kutekwa nyara miezi mitano iliyopita. Wahariri hao pia wanatoa maoni juu ya adhabu ya kifo dhidi ya manesi wa Bulgaria na daktari mmoja nchini Libya.

https://p.dw.com/p/CHSQ


Baada ya hofu ya miezi mitano wajerumani wametoa pumzi ya faraja kutokana na wateka nyara nchini Irak kumwachiwa bibi Krause.

Lakini mhariri wa gazeti la ESSLINGER anasema katika maoni yake kuwa bibi Krause alitekwa nyara pamoja na mwanawe miezi mitano iliyopita . Yeye ameachiwa lakini mwanawe bado yumo mnamo mikono ya wateka nyara. Kwa hiyo mama huyo sasa yumo katika taharuki kubwa zaidi. Mhariri huyo pia anaeleza wasi wasi mkubwa kwani haijulikani iwapo watu hao wana shabaha za kisiasa ama ni wahalifu tu wanaotafuta fedha?


Lakini gazeti la THÜRINGER ALLGEMEINE linaeleza katika maoni yake kuwa haitakuwa sawa kusema, mjerumani huyo bibi Krause na mwanawe hawakuwa waangalifu.!Gazeti linatilia maanani kwamba wateka nyara ni watu wasioogopa chochote .

Bibi Hannalore Krause na mwanawe Sinan walitwaliwa nyumbani kwao. Mhariri anasema hayo yanathibitisha hulka ya kihalifu ya wateka nyara .Hivyo basi haitakuwa sawa kusema kwamba bibi Krause na mwanawe hawakuwa waangalifu.

Katika maoni yake gazeti la KÖLNISCHE RUNDSCHAU linatafakari sababu za kuachiwa kwa mama huyo wa kijerumani. Mhariri anasema siyo lazima kwa mtu kuwa na upeo wa juu wa akili kutambua kwamba utekaji nyara sasa umekuwa njia ya kuingizia pesa nchini Irak.

Mhariri huyo anafafanua kuwa serikali ya Ujerumani imekataa kutekeleza tashi la wahalifu hao juu ya kuondoa majeshi kutoka Afghanistan.Wahalifu hao mara kadhaa walisisitiza tashi hilo katika kanda za video. Hivyo basi ni dhahiri kuwa shabaha ya wateka nyara hao ni kujipatia fedha.

Katika maoni yao leo ,wahariri pia wanazungumzia juu ya adhabu ya kifo iliyothibitishwa kwa manesi wa Bulgaria na daktari mmoja wa kipalestina nchini Libya.

Mahakama ya nchini Libya imethibitisha adhabu hiyo kwa watu hao kutokana na madai ya kuwaambukiza , watoto wa nchi hiyo, maradhi ya ukimwi kwa kudhamiria . Juu ya hukumu hiyo magazeti karibu yote yana maoni mshabaha.

Gazeti la HAMBURGER ABENDBLATT linasema adhabu hiyo ina manufaa ya kisiasa kwa kiongozi wa Libya Muammar Gaddafi.

Naye mhariri wa gazeti la LANDESZEITUNG anaafiki kwa kusema kuwa Gaddafi hana nia ya kuchochea mvutano zaidi .Hivyo basi ataibadili adhabu hiyo ili kujenga wajihi wake kimataifa.

AM