Maoni ya wahariri wa magazeti ya Ujerumani. | Magazetini | DW | 02.08.2010
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Magazetini

Maoni ya wahariri wa magazeti ya Ujerumani.

Katika maoni yao leo magazeti ya Ujerumani yanazungumzia juu ya kupigwa marufuku mabomu ya mtawanyiko!

Mabomu ya matawanyiko(Cluster bombs)

Mabomu ya matawanyiko(Cluster bombs)

Magazeti ya Ujerumani leo yanatoa maoni juu ya vita vya Afghanistan,mkataba wa kupiga marufuku mabomu ya mtawanyiko na pia yanazungumzia juu ya mgogoro wa Ugiriki.

Mhariri wa gazeti la General Anzeiger amesikitishwa na uamuzi wa Uholanzi wa kuondoa majeshi yake kutoka Afghanistan. Mhariri huyo anasema hatua hiyo maana yake ni ushindi kwa Taliban.Mhariri huyo anaeleza kuwa Uholanzi imekifanya kile ambacho taliban wanakitaka, yaani kuendesha kampeni ya mauaji ya kigaidi ili kufikia shabaha yao.

Gazeti la Stuttgarter Nachrichten pia linazungumzia juu ya vita vya Afghanistan na jinsi waziri wa ulinzi wa Ujerumani zu Guttenberg anavyovishughulikia vita hivyo.Mhariri wa gazeti hilo analalamika juu ya madai yaliyotolewa kuhusu kuhusika wanajeshi wa Ujerumani na mpango wa vikosi maalumu vya Marekani vinavyowalenga na kuwaua wapiganaji wa Taliban.

Mhariri wa gazeti hilo anatilia maanani kwamba habari juu ya kuhusika wanajeshi wa Ujerumani zilijulikana tokea msimu wa mpukutiko mwaka jana.Lakini wabunge wa Ujerumani wanapaaza sauti kulalamika juu ya mpango huo.Jee wao hawakuwa na habari?

Hata hivyo gazeti la Stuttgarter Nachrichten linasema kuwa waziri wa ulinzi zu Guttenberg alitoa taarifa kwa kamati zote husika za vyama vyote vitano vya kisiasa.Lakini gazeti linasema serikali ya Ujerumani haipaswi kuvishughulikia vita vya Afghanistan namna hiyo.

Mhariri wa gazeti la Hannoversche Allgemeine anazungumzia juu ya mkataba wa kuyapiga marufuku mabomu ya mtawanyiko(Cluster bombs) duniani. Lakini mhariri huyo anasema mafanikio bado hayajakamilika. Anaeleza kuwa hakuna vita vinavyoweza kuitwa safi, na wala hakuna silaha za kibinadamu.

Anasema vita ni chafu na silaha zote ni za kinyama na miongoni mwa silaha hizo ni mabomu ya matawanyiko yanayoendelea kuwaua na kuwajeruhi raia, hata ikiwa miaka mingi imepita baada ya vita kumalizika.

Na kwa kuwa mabomu hayo aghalabu ya wanawaathiri raia,kuyaunda ni hatua inayokiuka mkataba wa Geneva juu ya kuwalinda raia.Baada ya muda mrefu mkataba wa kuzipiga marufuku silaha hizo umetiwa saini na mataifa mengi .Lakini mhariri anasema ni jambo la kusikitisha kwamba mataifa makubwa na yenye nguvu yanakataa kuutia saini mkataba huo.

Gazeti la Frankfurter Allgemeine linazungumzia juu ya mgogoro wa Ugiriki kwa kusema kwamba itafika siku ambapo watu nchi hiyo watamshukuru waziri wao mkuu kwa hatua anazozichukua ili kuukabili mgogoro mkubwa wa madeni.

Gazeti hilo linasema Waziri Mkuu wa Ugiriki Papandreou amedokeza kwamba migomo inayofanywa na pande fulani za jamii asilani haitateresha sera anayoitekeleza.Gazeti linasema serikali ya hapo awali siku nyingi ingelibadili nia ili kuziridhisha pande fulani.Lakini waziri mkuu Papandreou amesema atasonga mbele na sera anayoitekeleza,na siku moja wananchi wake watamshukuru kwa msimamo huo.

Mwandishi Mtullya Abdu/Deutsche Zetungen/

Mhariri/Abdul-Raahman