1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maoni ya wahariri wa magazeti ya Ujerumani.

Abdu Said Mtullya25 Februari 2010

Wahariri wa magazeti ya Ujerumani wanakubaliana kwamba ni sahihi kwa Askofu Margot Käßmann kujiuzulu.

https://p.dw.com/p/MBJD
Kiongozi wa kanisa la Kilutheri nchini Ujerumani Margot Käßmann aliejiuzulu.Picha: dpa

Wahariri wa magazeti karibu yote ya Ujerumani leo wanatoa maoni juu ya kujiuzulu kwa kiongozi wa kanisa la kilutheri nchini Ujerumani Askofu Margot Käßmann.

Uamuzi wa askofu huyo kujiuzulu unatokana na kosa alilofanya la kunywa pombe kuvuka kiwango kinachoruhusiwa wakati akiwa anaendesha gari.

Hayo yalibainika baada ya kusimamishwa na maafisa wa usalama wa barabarani.

Mhariri wa gazeti la Sächsiche Zeitung anasema uamuzi wa mwanamke huyo jasiri kujiuzulu hakika unasababisha uchungu, na mtu akiangalia katika mtazamo wa kibinadamu , hatua hiyo ni ya kusikitisha sana.Kwani imemfika mtu anaewakilisha usahihi wa tabia na mtu aliekuwa amesimama kidete katika kutetea maslahi ya masikini.

Mhariri wa gazeti la Sächsiche Zeitung anasema kutokana na sifa hizo mama huyo anastahiki heshima pia ya watu ambao siyo wakristo.

Mhariri wa gazeti la Der neue Tag pia anasema , mwanamke huyo anastahili heshima ingawa ni jambo la kusikitisha kwamba ameamua kuondoka.

Mhariri wa gazeti hilo anafafanua kwa kueleza kuwa Margot Käßmann ametumia maadili yale yale, kama msingi wa kupitishia uamuzi alioufanya.

Alionyesha msimamo uliokuwa wazi juu ya masuala ya kijamii na kisiasa.

Mhariri huyo anatilia maanani kwamba mwanamke huyo hakungoja kushinikizwa kutoka nje .Alipitisha uamuzi bila ya kusita , na kwa hiyo anastahili heshima.

Na mhariri wa gazeti la General Anzeiger anasema kiongozi huyo wa kanisa alipaswa kuwa mfano wa tabia nzuri kwa jamii. Wadhifa wake una wajibu maalumu .Lakini hakuutekeleza wajibu huo mwishoni mwa wiki iliyopita.

Kwa hiyo amelazimika kujiuzulu- ni jambo la kusikitisha anasema mhariri huyo.

Gazeti la Saarbrücker linasema kujing'atua kwa Margot Käßmann ni pigo kubwa kwa kanisa la kiprotestanti nchini Ujerumani, kwani alikuwa kiongozi wa kanisa, mwenye hadhi ya kimataifa.

Lakini gazeti la Neue Osnabrücker linasema Käßmann hakuwa na njia nyingine ila kujiuzulu.

Mhariri wa gazeti hilo anakumbusha juu ya msimamo thabiti wa mama huyo wa kupinga vita vya Afghanistan na juu ya ulumbi alioutumia mwanadini huyo kupiga vita maovu ya ulevi na mihadarati.

Kwa hiyo gazeti,linasema anaetumia maneno makali dhidi ya wengine asitarajie kuonewa huruma anapokengeuka! Hatahivyo ameufinyanga udongo ungali maji.

Mhariri anaeleza kuwa uamuzi wake kujiuzulu umeziba vicheko vya vilabuni.

Mhariri wa gazeti la Münchner Merkur anasema watu wanaotumikia nyadhifa fulani hawapaswi kutoka nje ya mstari wa maadili.

Lakini mhariri huyo anaeleza,kwamba kukosea ni ubinadamu!

Hatahivyo uamuzi wake kujiuzulu ni sahihi kabisa kwa sababu asingeliweza tena kuyatekeleza majukumu yake bila ya kulitia kanisa katika mijadala, na hasa miongoni mwa maadui wa taasisi hiyo.

Gazeti la Recklinghäuser linaunga mkono hoja hiyo kwa kusisitiza kwamba mwanadamu hufanya makosa!

Mwandishi/Mtullya Abdu,DZ

Mhariri/Abdul-Rahman.