1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Magazetini

Abdu Said Mtullya27 Januari 2010

Magazeti ya Ujerumani leo yanatoa maoni juu ya pendekezo la kupiga marufuku,nchini Ufaransa vazi la kufunika mwili mzima-Burka.

https://p.dw.com/p/LhlE
Wabunge nchini Ufaransa wataka kupigwa marufuku kwa vazi la Burka.Picha: AP

Tume  ya wabunge  nchini Ufaransa imependekeza kupigwa marufuku kwa  vazi linalofunika mwili mzima.

Magazeti  ya Ujerumani  leo yanatoa maoni yao juu ya suala hilo.

Lakini wahariri hao pia wanaungumzia juu  ya uhusiano baina ya Israel  na Ujerumani.

Tume ya  wabunge kutoka vyama vyote vikuu nchini Ufaransa inataka watu wapigwe marufuku kuvaa, hadharani kwa vazi linalofunika mwili wote, yaani  burka,

Gazeti la Volksstimme linasema watu barani Ulaya  tayari inawawia vigumu  kuwaona akina mama wa  kiislamu  wakivaa  hijab  tu, sembuse Burka, linalofunika  mwili mzima.

Gazeti hilo linasema, vazi la Burka limevuka mipaka yote.

Mhariri wa Volkstimme  anaeleza kuwa vazi hilo halitangamani na utamaduni wa kifaransa kama  vile jinsi kichupi  cha  upati-yaani bikini  kisivyoweza kukubalika  katika utamaduni  wa  Yemen.

Kwa hiyo rais Sarkozy wa Ufaransa amesema vazi  la Burka halitakiwi, na linapaswa kupigwa  marufuku.

Gazeti linasema msimamo wa rais huyo hauwafiki na jamii yenye tamaduni mbalimbali-jamii ambayo kwa kawaida inahakikisha uhuru wa  mavazi  kwa wananchi  wote. Kwa hiyo Sarkozy anapaswa kusema wazi  kwamba stahamala ya demokrasia  sasa imefikia mwisho nchini Ufaransa.

Lakini gazeti la Allgemeine  Zeitung linaunga mkono msimamo  wa rais Sarkozy kwa kusema

kwamba kila  raia  mwema  katika nchi anapaswa kuwa na uhusiano mzuri na  jirani yake  bila ya kujali iwapo jirani  huyo ana nasaba  ya uhamiaji ama  la. Lakini  haina maana kwamba  raia mwema huyo akubali kila kitu cha jirani yake,  hata kile ,kinachoenda kinyume  na utamaduni  wake.

Gazeti la Braunschweiger leo linazungumzia juu  ya uhusiano baina ya Ujerumani  na Israel  kwa kutilia  maanani  historia ya nchi hizo mbili.

Gazeti hilo ,linaeleza kuwa yaliyotokea katika miaka  ya  nyuma bado ni zigo  kubwa, linalowalemea wajerumani. Na hakuna maneno  yanayotosheleza kulielezea  zigo hilo.

Ndiyo sababu anatamka mhariri  wa gazeti hilo  kuwa ni sahihi  kwamba rais Horst Köhler  wa Ujerumani ametoa mwito wa kuendelea kuyakumbuka yaliyotokea  mnamo miaka ya nyuma baina  ya  wajerumani na wayahudi. Mhariri wa gazeti la Brauschweiger anasisitiza   kwamba,  ili kujenga mustakabal mzuri katika uhusiano baina  ya Israel na Ujerumani ni muhimu kutekeleza wajibu wa kuhadithia historia  juu ya wahanga na walionusurika maangamizi  yaliyofanywa na mafashisti wa kijerumani.

Mwandishi/Mtullya Abdu/Deutsche Zeitungen.

Mhariri/Othman Miraji,