Maoni ya wahariri wa magazeti ya Ujerumani | Magazetini | DW | 21.02.2007
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Magazetini

Maoni ya wahariri wa magazeti ya Ujerumani

Magazeti ya Ujerumani hii leo yamezungumia juu ya mzozo unaoikabili kampuni ya ndege ya Airbus kuhusu mpango wake wa mabadiliko.

Mzozo unaoikabili kampuni ya ndege ya Airbus umekuwa mvutano baina ya washirika wa Ujerumani na Ufaransa. Pande zote mbili zinataka kuzuia mzigo wa mpango wa kuifanyia mageuzi kampuni ya Airbus nchini mwao. Kuna uhusiano wa kutilia shaka baina ya siasa na usimamizi wa kibiashara katika kampuni hiyo ya kutengeneza ndege.

Gazeti la Pforzheimer Zeitung limesema haiwezekani kuweka kiwango cha uwakilishi wa kitaifa katika utendaji bora wa kazi na uzalishaji wa bidhaa wakati nchi zinapojumuika pamoja katika kampuni moja. Kwa hiyo lilikuwa swala la muda tu, kufikia wakati ambapo kampuni ya Airbus haingeweza tena kufanya lolote bali kuugeukia mpango wake wa kupunguza matumizi ya fedha. Kama viongozi wa kampuni ya Airbus wanataka kuendelea kubakia katika mashindano na kampuni ya Boeing na kuzuia kushindwa, lazima waamue kwa haraka iwezekanavyo juu ya mpango wao wa kutaka kukata matumizi.

Mhariri wa gazeti la Nürnberger Nachrichten amesema hoja ya biashara katika kampuni ya Airbus kila mara huchukua nafasi ya pili. Kwa wakati huo juhudi za wazi za kisiasa za kuingilia kati hukua kufikia kiwango hatari kabisa. Tangu kampuni ya Airbus ilipokuwa katika njia panda, mipaka ya wizani sawa wa Ujerumani na Ufaransa katika kilele cha kampuni ya EADS umedhihirika wazi zaidi. Pande zote mbili zinajizuia. Mhariri anasema hali ya kutoaminiana baina ya Ujerumani na Ufaransa haijakuwa kubwa zaidi kuliko ilivyo leo.

Gazeti la Frankfurter Allgemeine limesema kwamba katika siku za usoni ruzuku itaamua kwa kiwango kidogo hali ya baadaye ya sehemu za uzalishaji yaani viwanda na nafasi za ajira kuliko utendaji bora wa kiufundi. Hicho ndicho kiini cha mzozo baina ya Ujerumani na Ufaransa. Kiongozi wa kampuni ya Airbus nchini Ufaransa, Louis Gallois, amejaribu kumvuta mshirika wa Ujerumani upande wake. Kiongozi wa kampuni ya EADS nchini Ujerumani, Thomas Enders, amepinga. Mhariri anasema Enders amechukua uamuzi wa sawa. Sio tu mzigo wa mageuzi unaotakiwa kugawanywa sawa bali pia nafasi za siku za usoni lazima zigawanywe sawa.

Gazeti la Leipziger Volkszeitung linaona kwamba serikali ya Ufaransa ina beba dhamana. Mara kwa mara Ufaransa imejaribu kutumia sera ya kiviwanda kuwa na hali bora ya bei. Serikali ya mjini Berlin imelitambua hilo, lakini kwa muda mrefu imeendelea kunyama kimya pasipo kulalamika. Hali haiko hivyo tena katika kampuni ya Airbus ingawa itachukua muda. Kwa sababu kinachozungumziwa hapa ni nafasi za ajira za wafanyakazi wenye ujuzi wa kiwango cha juu, kuweza kuendeleza teknolojia ya kisasa na ya hali ya juu, na uwezo wa uvumbuzi. La maana ni ikiwa Ujerumani nayo pia katika siku za usoni itakuwa katika nafasi muhimu miongoni mwa mataifa yanayoongoza kiviwanda.

 • Tarehe 21.02.2007
 • Mwandishi Josephat Charo
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/CHTe
 • Tarehe 21.02.2007
 • Mwandishi Josephat Charo
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/CHTe