1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maoni ya wahariri wa magazeti ya Ujerumani

Josephat Charo22 Februari 2007

Wahariri leo hii wamezungumzia juu ya hatua ya Uingereza na Danemark kuwaondoa wanajeshi wao kutoka Irak na Jumatano ya majivu ya kisiasa ya kiongozi wa zamani wa chama cha Christian Social Union, CSU, bwana Edmund Stoiber.

https://p.dw.com/p/CHTd

Wakati Marekani ikiongeza idadi ya wanajeshi wake mjini Baghdad, Uingereza na Danemark zinaondoa zaidi ya wanajeshi 2,000 kutoka kusini mwa Irak. Gazeti la Tagesspiegel la mjini Berlin limesema hatua ya Uingereza na Denmark ni ishara ya kushindwa. Baada ya maelfu kwa maelfu ya Wairaki kulazimika kuikimbia nchi yao, sasa washirika wakubwa wa Marekani nao wanaihamaha Irak. Tena katika wakati ambapo Marekani inajaribu kufanya juhudi za mwisho kufungua ukurasa mpya.

Gazeti la Märkische Allgemeine kutoka mjini Potsdam limetoa hukumu dhidi ya waziri mkuu wa Uingereza Tony Blair. Mhariri amesema kwa rais Bush wa Marekani ni kitu tofauti mbali na ushindi kwa washirika wake muhimu nchini Irak kuondoa majeshi yao, wakati yeye mwenyewe akijaribu kwa bidii kuibadili hali nchini humo kwa kutuma wanajeshi 21,000 zaidi.

Blair mwenyewe anakaribia kutumbukia mashakani. Tayari kupitia uaminifu wake wa kipofu amejiharibia sifa kwa kuiunga mkono Marekani katika vita vya Irak na kupuuza bila kujali wapinzani wa vita vya Irak waliozidi kuwa wengi. Sasa wakati anapokaribia kumaliza utawala wake anajaribu kukabiliana na mbinyo wa kisiasa kwa kutangaza kuwaondoa wanajeshi kutoka Irak. Mhariri anasema nafasi yake katika vitabu ya historia kama kibaraka cha rais Bush itaendelea kuwepo. Anastahili kuitwa hivyo.

Mhariri wa gazeti la Stuttgarter Zeitung naye amesema waziri Blair hataweza tena kurekebisha anavyoeleweka katika vitabu vya historia kwa kutangaza kuwaondoa wanajeshi wake kutoka Irak. Blair alitaka kuiongoza Uingereza barani Ulaya, katika moyo wa Ulaya, kama alivyosema yeye mwenyewe. Lakini ukweli ni kwamba ameifanya Uingereza kuwa nchi inayobeba madege ya kivita ya Marekani. Wapiga kura wa Uingereza huenda pengine wakakiadhibu chama cha Labour cha waziri mkuu Tony Blair kama wapiga kura wa Marekani walivyokiadhibu chama cha Republican cha rais Bush.

Tukigeukia siasa za hapa Ujerumani, gazeti la Frankfurter Allgemeine limemuaga bwana Edmund Stoiber kwa wimbo wa sifa. Mpango wake wa kisiasa ulikuwa wa kikristo, kijamii na wenye kushikilia ukale kana kwamba serikali na chama cha wananchi cha karne ya 21 kingeweza tu kuwa hivyo.

Msimamo wa Stoiber hauwezi kuzozaniwa na mtu yeyote, mawazo yake yameacha alama itakayokionyesha njia ya kufuata chama cha CSU katika miaka ijayo. Kuwa wazi kwa mambo mapya, kwa mengi, lakini sio kwa kila kitu, si kilele kizuri kwa chama cha CDU, ambacho Stoiber mara kwa mara alikisaidia kutokana na hali ngumu kana kwamba angebeba dhamana na kukielewa.

Gazeti la Süddeutsche Zeitung limesema juu ya yote sasa inajulikana vipi Stoiber anavyofikiria kuhusu maisha yake ya siku za usoni. Bwana Stoiber ambaye katika mawazo yake bado ni kiongozi wa chama cha CSU hafikirii kung´atuka kutoka ulingo wa siasa, bali anataka kuendelea kutumia nguvu zake kushiriki katika mambo yote yanayowezekana. Mhariri anamalizia kwa kusema bwana Stoiber alitoa hotuba ya kuaga mjini Passau lakini binafsi hataki kuaga.