Maoni ya wahariri wa magazeti ya Ujerumani | Magazetini | DW | 05.11.2007
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Magazetini

Maoni ya wahariri wa magazeti ya Ujerumani

Rais wa Pakistan, jenerali Pervez Musharaf, ametangaza hali ya hatari. Anajaribu kuwazima viongozi wenye ushawishi mkubwa wa kisiasa wanaompinga na anaendeleza wimbi la watu kutiwa mbaroni nchini kote. Katika maoni yao hii leo wahariri wa magazeti ya Ujerumani wamejishughulisha na hali nchini Pakistan.

Gazeti la Frankfurter Allgemeine linasema kwa sasa demokrasia na uthabiti nchini Pakistan uliojengwa na Marekani kupitia rais Pervez Musharaf umevunjika.

Muda mfupi kabla hali ya hatari kutangazwa nchini Pakistan waziri wa mashauri ya kigeni wa Marekani, Condoleezza Rice, na jenerali Pervez Musharaf walijadiliana na rais Musharaf akasema hapendi kufuata njia iliyo kinyume cha sheria.

Mharari wa gazeti la Frankfurter Allgemeine lakini anasema kinachoendelea hivi sasa nchini Pakistan ni hali isiyowezekana. Kwa kuzingatia uchafu unaoendelea nchini Pakistan Marekani inaachilia mambo yaendelee kama kawaida kana kwamba Pakistan bado ni kinga dhidi ya itikadi kali ya kiislamu. Hakuna anayefikiria juu ya kusitisha msaada wa kifedha kwa rais Pervez Musharaf.

Nalo gazeti la Süddeutsche limesema, kama mtu anayeyashughulikia maswala makubwa, rais Musharaf alijidhihirisha baada ya mashambulio ya Septemba 11 mwaka wa 2001 nchini Marekani, kama bwana mwenye mamlaka makubwa aliyejiunga na vita dhidi ya ugaidi na kuwa dikteta aliyependwa na nchi na magharibi.

Rais Musharaf anajua kwamba Marekani huzungumzia sana kuhusu maadili na maswala ya umuhimu mkubwa lakini hata hivyo inamuunga mkono mtawala mdhalimu ambaye anakabiliana na wanamgambo wa kiislamu, kama mtetezi wa demokrasia ambaye wanalazimika kumtumia. Ndio maana rais Musharaf anatumia sababu ya vita dhidi ya ugaidi kuikandamiza demokrasia kwa pigo lake jipya la kutangaza hali ya hatari nchini Pakistan.

Gazeti la Tageszeitung la mjini Berlin linaamini rais Musharaf amefika mwisho. Mhariri anasema makubhaliano kati ya waziri mkuu wa zamani wa Pakistan, Benazir Bhutto, na rais Musharaf yalifufua matumaini kwamba tofauti kati ya utawala wa kidemokrasia na kiimla zingeweza kumalizwa. Sasa jumuiya ya kiraia inamtaka rais Musharaf aondoke madarakani. Jenerali Musharaf atakuwa mhanga wa juhudi zake mwenye huku akijaribu kupigania masilahi yake binafsi lakini wakati huo huo akiendeleza masilahi ya taifa.

Kana kwamba tayari hajachukua hatua za kutosha kuushinikiza mtandao wa wanamgambo wenye itikadi kali ya kiislamu, bado anaendelea kujitengezea maadui zaidi. Sasa ni swala la muda kabla jeshi la Pakistan ambalo ni chombo kikubwa chenye nguvu kinachomuunga mkono Musharaf, kutambua njama yake. Maslahi ya kibinafsiy a rais Musharaf kwa vyovyote si sawa ya makamanda wa jeshi la Pakistan.

Gazeti la Nürnberger Nachrichten linaiona Marekani na Umoja wa Ulaya zikiwa katika mgogoro. Marekani na Umoja wa Ulaya juu ya yote zinaridhika na maendeleo nchini Pakistan. Lakini kuna uongo kidogo wakati zinapozungumzia wasiwasi wao kwamba uchaguzi nchini Pakistan huenda ukatatizwa. Marekani na Umaja wa Ulaya haziwezi kutokana na sababu za masilahi yenye umuhimu mkubwa wa kisiasa, kusitisha msaada kwa rais Musharaf, kwa kuwa Pakistan ina umuhimu mkubwa katika vita dhidi ya al Qaeda.

Huku uchaguzi ukikaribia nchi za magharibi zinalazimika kuchagua katiy a mambo mawili: kumuunga mkono dikteta au kuhatari ya wanamgambo kuwa na ushawishi mkubwa. Nchi za magharibi zimechagua kufanya uovu mdogo, yaani kumuunga mkono rais Musharaf. Na machoni pake Musharaf hivo ni vita baridi.

 • Tarehe 05.11.2007
 • Mwandishi Josephat Charo
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/C7l2
 • Tarehe 05.11.2007
 • Mwandishi Josephat Charo
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/C7l2