1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maoni ya wahariri wa magazeti ya Ujerumani leo

Charo Josephat 6 Julai 2009

Ziara ya Obama Urusi na serikali ya Ujerumani kuzikosoa benki humu nchini

https://p.dw.com/p/Ii2A
Rais wa Marekani Barack ObamaPicha: AP

Tukianza na ziara ya rais Barack Obama nchini Urusi hii leo, gazeti la Rheinpfalz la mjini Ludwigshafen linaonya dhidi ya kuwa na matumaini makubwa kuhusu ziara ya kiongozi huyo wa Marekani

Mhariri wa gazeti la Rheinpfalz anasema mwanzo mpya wa uhusiano kati ya Marekani na Urusi ambao nchi hizo zilikubaliana mjini London mwanzoni mwa mwezi Aprili mwaka huu, ni kibarua kigumu ambacho hakijulikani kitaanzia wapi na kumalizikia wapi. Hususan ikizingatiwa kwamba swala la madaraka mpaka sasa halijawekwa wazi nchini Urusi. Waziri mkuu wa Urusi Vladamiri Putin amejitokeza kuwa msitari wa mbele na kuonekana kuwa mwenye madaraka makubwa kuliko rais wa nchi hiyo Dmitry Medvedev. Rais Putin ameonekana akitofuatiana na rais Medvedev kwa matamshi yake ya mamlaka makubwa na ambayo hayafai kutolewa na kiongozi kama yeye serikalini, linasema gazeti la Rheinpfalz katika maoni yake.

Nalo gazeti la Müncherner Merkur kuhusu ziara ya rais Obama mjini Moscow limeandika: Jambo linalosubiriwa kwa hamu kubwa ni ikiwa Warusi wanatashawishika, na ikiwa pia ni katika masilahi yao, kuizuia Iran kutengeneza silaha za nyuklia. Ziara ya rais Obama ni jaribio jipya na gumu ikiwa uhusiano wa kiitikadi kati ya Urusi na Marekani ambao umeharibika, inawezekana kuujengea msingi mpya wa kinadharia, limeandika gazeti la Münchener Merkur.

Gazeti la Handelsblatt la mjini Düsseldorf lina shakashaka kuhusu ziara ya Obama mjini Moscow.

Gazeti hilo linasema wazo kwamba Wamarekani na Warusi wanaweza baada ya kumalizika vita baridi kujongeleana na kufikia makubaliano ya maana, ni ndoto! Rais wa Urusi, Dmitry Medvedev anapendelewa kwa kuwa bado anaonekena kijana na mwenye kupendelea mabadiliko ya wastani kuliko mtangulizi wake Vladamir Putin. Lakini katika sera ya kigeni mpaka sasa rais Medvedev hajaweza kujikwamua kutokana na sera za waziri mkuu Putin. Mkakati mpya wa Urusi kuhusu maswala ya ulinzi ambao rais Medvedev aliuridhia, bila shaka una maandishi mapya, lakini kimsingi haujabadilika sana.

Serikali ya Ujerumani yazikosoa benki

Likitugeuzia mada gazeti la Süddeutsche Zeitung linazungumzia hatua ya serikali ya Ujerumani kuzikosoa benki za humu nchini.

Mhariri wa gazeti hilo anasema hali ya mabenki kwa matazamo wa serikali ni ya kukatisha tamaa. Serikali tayari imetumia kiasi cha euro nusu bilioni kuzisaidia benki kukabilian na mgogoro wa kiuchumi. Vyama vya kisiasa haviwezi kuongeza shinikizo kwa sekta ya fedha kama inavyoweza kufanya katika kampeni za uchaguzi. Iwapo serikali itazilazimisha benki kutoa mikopo au yenyewe igawe fedha, baadaye itabeba dhamana kwa hasara itakayotokea. Je hilo ndilo analolitaka waziri wa fedha Peer Steinbrueck na wengine wanaopaza sauti kuhusu tatizo la kiuchumi humu nchini? Linauliza gazeti la Süddeutsche Zeitung.

Gazeti la Frankfurter Allgemeine Zeitung linakataa ukosoaji ulioelekezwa kwa mabenki humu nchini kwamba zimezuia fedha zilizopkea kutoka kwa serikali kwa kiwango cha chini kabisa cha riba. Mhariri wa gazeti hilo anasema madai kwamba benki za Ujerumani zimezuia fedha na kukataa kutoa mikopo si sahihi.

Katika miezi ya kwanza ya mwaka huu, benki za Ujerumani zilitoa mikopo inayokaribia kiwango kilichotolewa mwaka jana. Sasa lakini zinakabiliwa na shinikizo kutokana na athari za mgogoro wa kiuchumi unaoikabili dunia na kunywea kwa uchumi, mambo yatakayoongeza idadi ya watu watakaoshindwa kulipa mikopo yao. Lakini hatua ya serikali kuzielekezea hasira yake benki humu nchini haisaidii kitu. Chanzo cha mgogoro wa kiuchumi ni utoaji kiholela wa mikopo. Mhariri wa Frankfurter Allgemeine Zeitung anamalizia kwa kusema funzo linalotakiwa kujitokeza hapo ni kuwa hofu kupita kiasi ya utoaji wa mikopo kwa mara nyengine tena inadhihirisha kuna gharama ya kulipa.

Na kwa maoni hayo ya gazeti la Frankfurter Allgemeine ndio tunakamilisha maoni ya wahariri wa magazeti ya Ujerumani yaliyochapishwa leo.