1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maoni ya wahariri wa magazeti ya Ujerumani leo

Charo, Josephat21 Julai 2008

Wahariri wa magazeti ya Ujerumani wanazungumzia kuachiwa huru kwa wajerumani watatu nchini Uturuki, kuapishwa kwa makurutu 500 wa jeshi la Ujerumani na mazungumzo kuhusu mpango wa nyuklia wa Iran

https://p.dw.com/p/Eg8s
Wawili kati ya wapanda milima watatu wajerumani wakiwasili kwenye kituo cha usalama katika mji wa Agri mashariki mwa Uturuki.Picha: AP

Tunaanza na kuachiwa huru kwa wajerumani watatu waliokuwa wakizuliwa mashariki mwa Uturuki.

Gazeti la Die Welt linasema kwamba wajerumani hao kufumba na kufumbua wameachiwa huru wakiwa salama salmini hawawashukuru sana wapatanishi wa Uturuki wala Ujerumani waliotumwa kujaribu kuwaokoa bali wanashukuru zaidi ufahamu wa watekaji nyara waliokuwa wakiwazuilia. Kwa kuwa chama kilichopigwa marufuku cha PKK nchini Uturuki tangu awali kiliona utekaji nyara wa wajerumani hao kuwa kosa kubwa ambalo lingekiharibia sifa.

Wajerumani hao waliokuwa wakipanda milima mashariki mwa Uturuki walikuwa na bahati kwamba pande zote zilijizuia na hakukutokea kituo chochote kibaya. Mhariri wa gazeti la Die Welt anamalizia kwa kusema Chama cha PKK bila shaka kupitia utekaji nyara wa wajerumani hao kimedhihirisha wazi mpasuko uliopo katika muundo na uongozi wake.

Gazeti la Frankfurter Rundschau kwa maoni yake linasema chama cha PKK kimevunjwa makali kutokana na utekaji nyara wa wajerumani hao watatu. Hata hivyo mhariri anaonya hiyo haina maana kwamba chama hicho sasa sio hatari tena. Ingawa wanachama wa chama hicho wamesimama wakiilekeza migongo yao ukutani, ni vigumu kutathmini kitu gani wanachopanga kufanya. Kwa hiyo chama hicho kinaweza kufanya chochote wakati wowote.

Kuapishwa kwa makurutu wa jeshi la Ujerumani

Kuhusu kuapishwa kwa makurutu 500 wa jeshi la Ujerumani nje ya bunge jana jioni gazeti la Ostsee Zeitung la mjini Rostock linasema tukio hilo la kwanza kuwahi kufanywa mahala hapo lilikaribia kuwa tukio la kuchukiza kwani wanasiasa wengi mashuhuri walichagua kwenda likizo badala ya kujumuika na makurutu hao wakila kiapo kutii katiba ya Ujerumani.

Kuapishwa huko kulikofanyika kwa mara ya kwanza nje ya bunge ambamo wanasiasa hupitisha maamuzi yanayoyahatarisha maisha ya wanajeshi wa Ujerumani kungekuwa kashfa kubwa. Kansela wa Ujerumani Angela Merkel alitambua hatari ya hilo kutokea na hatimaye akahudhuria sherehe ya kuapishwa kwa makurutu hao. Hata hivyo mhariri wa gazeti la Ostsee Zeitung anaona uamuzi huo ulichukuliwa dakika za mwisho.

Gazeti la Rheinische Post la mjini Düsseldorf linasema linabakia kuwa jambo la kuudhi kwamba kansela Merkel, naibu kansela Frank Walter Steinmeier na wengine walijihisi kulazimika kuhudhuria kuapishwa kwa makurutu 500 wanajeshi nje ya bunge.

Inabakia kuwa aibu kwa wanasiasa wengi ambao kwa sababu ya kuwa likizoni au waliokuwa wakifanyiwa mahojiano na televisheni, hawakuonekana kwenye sherehe ya kuapishwa wanajeshi hao.

Mazungumzo kuhusu mpango wa nyuklia wa Iran

Na hatimaye ni kuhusu mazungumzo ya mpango wa nyuklia wa Iran mjini Geneva Uswisi. Gazeti la Frankfurter Allgemeine Zeitung linasema ni jambo la busara kwamba sasa kwa mara ya kwanza mjumbe wa ngazi ya juu wa Marekani anashiriki kwenye mazungumzo hayo na ujumbe wa Iran hauna tena jipya la kuwasilisha mbali na ukaidi wake.

Gazeti linasema, ukweli kwamba kuwepo kwa mjumbe wa wizara ya mambo ya ndani ya Marekani katika mazungumzo hayo hakuna maana Iran itabadili msimamo wake, kunatilia shaka wazo la mgombea urais wa Marekani Barack Obama na viongozi wengi wa Ulaya kuwa mzozo wa Iran unaweza kutanzuliwa kwa njia ya mazungumzo ya ana kwa ana kati ya serikali ya mjini Tehran na Washington.