1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maoni ya wahariri wa magazeti ya Ujerumani leo

Charo, Josephat7 Julai 2008

Wahariri leo wanazungumzia mkutano wa kilele wa nchi zilizoendelea kiviwanda dunaini G8 huko Japan na mwito uliotolewa na baraza la wataalamu la hapa Ujerumani kutolewe fedha zaidi kwa elimi ya juu

https://p.dw.com/p/EXeO
Waziri mkuu wa Japan Yasuo Fukuda (kulia) na kansela wa Ujerumani Angela MerkelPicha: AP

Tukianza na mkutano wa nchi za G8 ulioanza hivi leo nchini Japan, gazeti la Die Welt linasema kuhusu maswala nyeti yanayohitaji ufumbuzi wa haraka, nchi husika hazihudhurii mkutano huo ili kushiriki katika kutafuta ufumbuzi wa matatizo hayo.

Mhariri anauliza je itawezekana vipi kumaliza mzozo katika masoko ya mafuta ikiwa Saudi Arabia na China hazishirikishwi kila mara. Itawezekana vipi kulitatua tatizo la mfumuko mkubwa wa bei na kuporomoka kwa sarafu ya dola ya kimarekani kwenye mkutano huo ikiwa jamii za kiraia ambazo zinaathirika zaidi kutokana na kupanda kwa bei za bidhaa, hazijaalikwa angalau kwa chakula cha mchana kandoni mwa mkutano huo?

Gazeti la Die Welt laendela kusema kuwepo kwa China, Saudi Arabia na Brazil katika mkutano huo kungepelekea kupitishwa kwa maamuzi magumu, lakini bila nchi hizo makubaliano yatakayopitishwa hayatakuwa na maana. Nchi za G8 zina asilimia zaidi ya 50 ya nchi zilizoendelea kiuchumi duniani, na zinaongoza katika ukuaji wa kiuchumi. Kutokana na hayo, itakuwa sawa tu ikiwa rais wa Ufaransa Nicholas Sarklozy atatoa mwito muungano wa G8 upanuliwe.

Gazetila Neue Presse la mjini Hannover linasema nchi zinazoendelea haraka kiuchumi kama vile China na India zenye mahitaji yake makubwa ya nishati sharti zibebeshwe jukumu la matumizi mazuri ya raslimali kama vile pia nchi zinazoinukia haraka kiuchumi zikiwemo Brazil, Mexico na Afrika Kusini. Rrais wa Marekani naye anatakiwa pia ashinikizwe.

Mhariri wa gazeti la Neue Presse anasema mara kwa mara katika mikutano ya G8 hutolewa maneno matupu lakini katika mkutano wa safari hii nchini Japan hiyo itakuwa hatari kubwa. Hakujakuwepo na shinikizo kubwa dhidi ya wanasiasa kama wakati huu. Kwa kuwa wakati wa kupigania maslahi ya kibinafsi na wakati wa mchezo wa paka na panya umekwisha. Ulimwengu unahitaji mwelekeo mpya.

Gazeti la Thüringer Allgemeine la mjini Erfurt lina wasiwasi. Mhariri anasema haiwezi kuwa kwa maslahi ya Ulaya ya sasa, kwamba katika nchi tajiri bei za ngano na mahindi zisiwe thabiti, huku mamia ya mamilioni ya watu wakiteseka kutokana na njaa duniani.

Swala lengine lililozingatiwa na wahariri leo ni mwito uliotolewa na baraza la wanasayansi la hapa Ujerumani kutaka fedha zaidi zitolewe kwa ajili ya elimu ya vyuo vikuu.

Gazeti la Tagesspiegel limedokeza kwamba kiwango cha elimu katika sehemu mbalimbali kimeporomoka. Hili linadhihirika kutokana na ongezeko la wanafunzi wanaolazimika kukatiza masomo yao.

Mpango wa kuanzisha mfumo wa masomo ya shahada ya kwanza ulitakiwa kutoa ufumbuzi wa tatizo hili. Lakini kutokana na usimamizi mbaya idadi wa wanafunzi wanaoacha masomo kabla kumaliza muda wao kupata shahada nayo inazidi kuongezeka.

Ujerumani haiwezi kuruhusu watoto wa kijerumani pekee waweze kumaliza masomo yao ya chuo kikuu kwa kuwa wana uwezo wa kifedha. Hatari ya kupungua kwa wataalamu na mabadiliko yanayotokea hapa nchini yanailazimisha Ujerumani kutumia akiba yake kwa ajili ya elimu ili kuboresha elimu.