Maoni ya wahariri wa magazeti ya Ujerumani leo | Magazetini | DW | 08.08.2007
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Magazetini

Maoni ya wahariri wa magazeti ya Ujerumani leo

Katika maoni hii leo wahariri wa magazeti ya Ujerumani wanazungumzia michezo ya Olimpik, iliyopangwa kufanyika mwaka ujao nchini China. Licha ya serikali ya China kutoa ahadi nyingi, swala la ukiukaji wa haki za binadamu bado halijabadilika nchini humo.

Mhariri wa gazeti la Handelsblatt anasema ulimwengu mmoja, ndoto moja, ndio mbiu ya michezo ya Olimpik mjini Beijing China. Ama kweli ufanisi wa michezo hiyo hautategemea na viwanja vya michezo na fedha. Kufaulu kwa jamhuri ya umma wa China kuonyesha sura mpya, kutategemea pia maoni ya wakosoaji wa nchi hiyo.

Gazeti hilo limeendelea kusema wanaharakati wa ukimwi wanateswa, uhuru wa vyombo vya habari vya kigeni umebanwa, walio na mawazo tofauti katika maeneo ya kazi wanapigwa marufuku. Serikali ya mjini Beijing itakuwa inafanya kosa kubwa ikiwa inafikiri lazima iwafunge midomo waandishi wa habari wabaya, watu waliopoteza makaazi yao na wapinzani wa kisiasa, ili iweze kuonyesha taswira isiyo na dosari.

Nalo gazeti la Frankurter Rundschau linasema utawala wa Beijing unakosea kwani ufanisi wa michezo ya Olimpik unahitaji mengi zaidi yafanywe mbali na maandalizi mazuri na majengo makubwa ya kisasa. Ulimwengu utatarajia maelezo kutoka kwa China juu ya hukumu nyingi za vifo, pengo linalozidi kuongezeka katika jamii na uharibifu wa mazingira. Mhariri anasema kama China inataka iheshimiwe na ulimwengu, serikali inalazimika kuruhusu uhuru zaidi.

Mhariri wa gazeti la Mitteldeutsche kutoka mjini Halle anadhani serikali ya Peking inataka kuitumia michezo ya Olimpik kama chombo kikubwa cha kutangazia propaganda yake. Lengo hili litachukua nafasi ya kila kitu. Anayetumai hatua ya China kujitangaza wazi kwa ulimwengu kitakuwa chanzo cha kufichua mambo ambayo bado yamefichika, huenda akavuunjika moyo hatimaye. Hii ni kwa sababu umesalia mwaka mmoja tu kabla michezo ya Olimpik kuanza, lakini hali ya haki za binadamu nchini China imezidi kuwa mbaya kuliko ilivyokuwa hapo kabla.

Gazeti la Frankfurter Allgemeine linaingalia China na wasiwasi. Mhariri anasema waandamanaji watatupwa gerezani na vyombo vya habari vitazuiliwa. Kwa miezi kadhaa jamii za wachache zinakandamizwa, kwa mfano jamii ya Watibeti. Kiongozi wa dini, Dalai Lama, ameshushwa hadhi yake na kuelezwa kuwa muasi hatari.

Raia wa Taiwan wamekuwa wakitishwa na vita iwapo watafanya chochote kitakachoonekana kuwa jitihada za kutaka kujitawala. Je, nchi inayojiandaa kuwakaribisha wanariadha bora duniani kwenye mashindano makubwa kama ya Olimpik katika kipindi cha mwaka mmoja ujao, inapaswa kuwa na sifa kama hizo? Ameuliza mhariri wa gazeti la Frankfurter Allgemeine.

Kwamba tunatakiwa kuendelea kufurahia sifa nzuri ya michezo ya Olimpik ni jambo ambalo linatakiwa kuwa wazi, limesema gazeti la Mannheimer Morgen. Serikali ya mjini Peking inaielewa michezo ya Olimpik kama maonyesho sahihi ya propaganda. Hatua zinazochukuliwa kuhakikisha ufanisi wa michezo hiyo zitakuwa kubwa katika kila sehemu. Mjini Beijing kamera laki tatu za kuchunguza mienendo ya watu, zitawekwa ili kudhibiti kila kitu, na bila shaka hata vyombo vya habari.

Gazeti la Landshuter limeeleza maoni yake kwa uwazi. Mhariri wa gazeti hilo anasema kuupa fursa mji wa Beijing kuandaa mashindano ya Olimpik lilikuwa kosa. Matumaini ya kamati ya kimataifa ya maandalizi ya michezo hiyo, IOC, kwamba vijana kutoka sehemu mbalimbali duniani na vyombo vya habari vya kimataifa vitaweza kuisadia serikali ya China kuelekea mageuzi ya kidemokrasia, ni dhahiri hayatatimia.

 • Tarehe 08.08.2007
 • Mwandishi Josephat Charo
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/CHSD
 • Tarehe 08.08.2007
 • Mwandishi Josephat Charo
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/CHSD