1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maoni ya wahariri wa magazeti ya Ujerumani leo Agosti 24

Josephat Nyiro Charo24 Agosti 2010

Mada iliyohanikiza ni uamuzi wa kiongozi wa chama cha Social Democratic, SPD hapa nchini, Frank Walter Steinmeier, kumpa figo mkewe, Elke, anayekabiliwa na tatizo la figo lake. Pia mageuzi katika jeshi la Ujerumani

https://p.dw.com/p/Oufq
Frank-Walter Steinmeier, kiongozi wa chama cha SPDPicha: AP

Gazeti la Lübecker Nachrichten linasema hatua ya Steinmeier kutangaza hadharani uamuzi wake wa kutoa figo na kumpa mke wake huenda ikawasaidia watu wengi wanaougua. Kwa miaka mingi madaktari wamelamika juu ya upungufu wa watu wanaojitolea kutoa viungo vyao kwa hiari kuwasaidia wengine wanaokabiliwa na magonjwa, kwa sababu kwa wengi mada hiyo inakuwa kama mwiko.

Takwimu zinaonyesha kwamba Wajerumani 3 hufariki dunia kila siku, kwa sababu hawakumpata mtu anayetaka kutoa kiungo chake kwa ajili ya kuyaokoa maisha yao. Kwa wakati huu kuna wagonjwa 12,000 nchini kote Ujerumani wanaohitaji kiungo kipya kwa dharura.

Nalo gazeti la Mannheimer Morgen kumhusu bwana Steinmeier linasema kila Mjerumani anafahamu fika idadi ndogo iliyopo ya watu wanaotoa viungo vyao kwa hiari kuwasaidia wengine.

Sasa anajitokeza mwanasiasa wa ngazi ya juu, kiongozi wa chama cha SPD, na kuudhihirishia ulimwengu mapenzi yake kwa mkewe kwa hatua maalumu kabisa ya kishujaa. Ama kweli mara nyingine kuna mambo muhimu zaidi katika maisha kuliko mijadala ya kisiasa, mathalan kustaafu na umri wa miaka 67. Uamuzi wa Steinmeier umeivuka mipaka ya chama chake cha SPD na unamfanya kuwa mtu mwenye huruma kweli.

Gazeti la Bild kumhusu Steinmeier linasema ni habari zinazoigusa Ujerumani nzima. Gazeti linasema mwanasiasa huyo anampa mkewe Elke figo ili awe na nafasi ya kuendelea kuishi. Ni ishara ya mapenzi, lakini uamuzi wake unatakiwa kuwatia aibu Wajerumani kwani katika mwaka uliopita Wajerumani 1,217 walitoa viungo vyao baada ya kufa, lakini Wajerumani 11,710 bado wanasubiri kupata moyo, ini, au figo kwa dharura.

Mhariri anasema Steinmeier hatoi figo lake kwa sababu anampenda mkewe tu, bali ni kwa sababu bado idadi ya Wajerumani walio tayari kufanya hivyo baada ya kufa, ingali ndogo mno.

PK CSU Karl Theodor zu Guttenberg
Karl-Theodor zu Guttenberg, waziri wa ulinzi wa UjerumaniPicha: picture-alliance / dpa

Likizungumzia mapendekezo ya kulifanyia mageuzi jeshi la Ujerumani yaliyowasilishwa na waziri wa ulinzi Karl Theodor zu Guttenberg, gazeti la Der neue Tag linasema asante kansela Angela Merkel kwa tangazo lako la wazi. Tangu mwishoni mwa juma lililopita, tunajua kwamba kansela Merkel hajampiga marufuku mtu yeyote kufikiria kuhusu mada ya kulifanyia mageuzi jeshi la Ujerumani.

Gazeti linasema katika sera kuhusu usalama, sharti kuwepo na fikra za kimkakati za viongozi wa ngazi ya juu wanaohusika. Orodha ya maswali yanayojitokeza ni: Kwa nini tunalihitaji jeshi? Muundo wa jeshi hilo unatakiwa kuwa vipi, na fedha za kuunda jeshi hilo zitatoka wapi? Ndio maana mjadala umegeuka, hata kama waziri wa ulinzi Karl Theodor zu Guttenberg hataki kuliona hilo.

Gazeti la General Anzeiger linasema jeshi la Ujerumani katika siku za usoni litakuwa dogo, imara zaidi na lenye uwezo mkubwa zaidi kuweza kushiriki katika harakati za nje ya nchi.

Mhariri anasema litakuwa jambo la kusisimua kuona kuna ukweli gani uliojificha katika hotuba za Jumapili. Wanajeshi ndio watakaokuwa wa kwanza kupata hisia - kwa mfano wale walioko katika uwanja wa mapambano huko nchini Afghanistan.

Mwandishi: Josephat Charo/DPA

Mhariri: Abdul-Rahman