Maoni ya wahariri na Abdu Mtullya | Magazetini | DW | 09.10.2006
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Magazetini

Maoni ya wahariri na Abdu Mtullya

Katika maoni yao wahariri wa magazeti ya Ujerumani leo wanazungumzia juu ya kuuawa wandishi habari wawili wa Deutsche Welle nchini Afghanistan na mwandishi habari wa Urusi. Wahariri hao pia wanatoa maoni yao juu ya mgogoro unaoikabili serikali ya mseto ya Kansela Angela Merkel.


Mhariri wa gazeti la mjini Rostock mashariki mwa Ujerumani OSTSEE ZEITUNG anamkariri mwandishi habari wa Urusi alieuawa, Anna Politkovskaya aliesema kuwa kazi ya uandishi habari sasa imekuwa ya hatari kubwa zaidi kuliko wakati mwingine wowote.

Lakini mwandishi huyo , anasema mhariri wa gazeti hilo , haukuogopa vitisho vya kuuawa katika utekelezaji wa kazi yake yaani kufichua ukiukaji wa haki za binadamu nchini Urusi na juu ya udhalimu unaotendwa na majeshi ya Urusi nchini Chechnya.

Mwandishi huyo, anatilia maanani mhariri wa gazeti hilo , alikuwa anataka kusema ukweli. Gazeti hilo pia linatilia maanani hatari kubwa inayowakabili wandishi ,na hasa katika sehemu zinazokabiliwa na migogoro kama Afghanistan na Irak.

Juu ya mikasa hiyo ya kuhuzunisha mhariri wa gazeti la KÖLNISCHE RUNDSCHAU anaona mwambatano; kwamba wandishi hao wote watatu wameuawa, kwa sababu tu walikuwa wanataka habari za ukweli ili kuzitangaza.

Mhariri huyo pia anaonya juu ya msimamo finyu wa wale wanaokanganya ujasiri wa uandishi na ukosefu wa tahadhari miongoni mwa wandishi. Mhariri huyo anasema, ikiwa wandishi watashutumiwa kwa kutokuwa na tahadhari katika kazi yao basi Ulaya ya magharibi imeshatokomea katika mkondo mbaya, yaani wa kutokuwapo uhuru wa vyombo vya habari.

Gazeti la mjini Berlin TAZ linasema katika maoni yake kwamba watu nchini Urusi wanahofia kisasi. Hakuna mtu sasa anaethubutu kutoa shingo yake nje ya dirisha ili kushuhudia kinachotokea , watu wanatazama kwengine kabisa na wanazama katika hali ya utepetevu. Kuuawa kwa bibi Politkovskaya kumejenga pengo katika safu ya Urusi adilifu.

Naye mhariri wa gazeti jingine la mjini Berlin la DIE WELT anawasilisha ujumbe kwa rais Putin wa Urusi kwa kumwambia rais huyo kwamba kuua ni njia hasidi ya kukandamiza uhuru wa vyombo vya habari.

Katika maoni yao wahariri wa magazeti ya leo pia wanazungumzia juu ya mgogoro unaikabili serikali ya mseto ya Kansela Angela Merkel . Gazeti la STUTTGARTER NACHRICHTEN linasema badala ya serikali hiyo kuelekeza umakinifu katika utekelezaji wa sera za mageuzi kila mwakilishi wa mseto huo anazingatia maslahi yake binafsi. Hali hiyo anaeleza mhariri wa gazeti hilo, asilani haitajenga mazingira mazuri ya utendaji kazi.

Lakini mhariri wa gazeti la ALLGEMEINE ZEITUNG hakubaliani na tathmini hiyo. Anasema pamoja na mvutano uliopo ndani ya serikali ya mseto hapa nchini,serikali hiyo haipo katika hatari kubwa. Kwani , anahoji mhariri huyo kila upande unaoshiriki katika serikali hiyo ya mseto unauhitaji upande mwingine. Masuala muhimu juu ya mageuzi katika soko la ajira, kodi ya wajasiramali na sheria juu ya ustaafu , hayawezi kutekelezwa bila ya mseto huo.

Lakini mhariri wa gazeti la FRANKFURTER RUNDSCHAU anaesema kuwa anaona hali ya fadhaa inayomkabili Kansela Merkel . Mhariri anaeleza kuwa bibi Merkel anaonyesha dalili za kutojua kwa uhakika jinsi washiriki wa serikali ya mseto watakavyokaribiana tena ili kuufanya mseto huo uwe na nguvu . Mhariri anaeleza kuwa bibi Merkel anatambua kwamba sauti yake haisaidii. Kwa hiyo anachofanya sasa ni kusubiri !

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com