1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

MAONI YA WAHARIRI JUU YA WAZIRI WESTERWELLE

Abdu Said Mtullya30 Agosti 2011

Wahariri wa magazeti wamtaka Waziri Westerwelle ang'atuke!

https://p.dw.com/p/12Pow
Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Guido WesterwellePicha: dapd

Mjadala mkubwa umezuka nchini Ujerumani juu ya mustakabal wa Waziri wa mambo ya nje Westerwelle. Wahariri wa magazeti pia wanatoa maoni yao juu ya waziri huyo . Wahariri hao pia wanazungumzia juu ya mgogoro wa madeni barani Ulaya na juu ya tatizo la ongezeko la idadi ya watu duniani.

Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Westerwelle sasa anakabiliwa na kipindi kigumu katika wadhifa wake. Baadhi ya watu muhimu, pia ndani ya chama chake cha FDP wanamtaka Waziri huyo,afanye uamuzi mwafaka.

Katika maoni yake juu ya Waziri Westerwelle gazeti la Flensburger Tageblatt linasema kuwa Waziri huyo amezipoteza nguzo zote zilizokuwa zinamshikilia. Kwa hiyo,kwa manufaa ya chama chake na ya serikali ya mseto, anapaswa kujing'atua yeye mwenyewe.

Mhariri wa gazeti la Mittelbayerische pia anataka waziri Westerwelle aondolewe. Anauliza, mpaka lini waziri huyo ataendelea kudhalilishwa. ? Mwenyekiti wa chama chake, pamoja na Kansela wa Ujerumani wamemkosoa hadharani kwa makosa aliyoyafanya juu ya suala la Libya. Ni jambo la kusikitisha jinsi bwana Westerwelle alivyoporomoka. Lakini litakuwa jambo la kusikitisha zaidi ikiwa viongozi wa chama chake na kiongozi wa serikali ya Ujerumani hawatachukua hatua zinazostahili.

Mhariri wa gazeti la Neue Westfälische anakubaliana na maoni ya wahariri wengine, lakini anasema kuwa makosa yaliyomo katika sera ya nje ya Ujerumani hayakusababishwa na Waziri Westerwelle peke yake.!

Gazeti la Reutlinger linazungumzia juu ya tatizo la ongezeko la idadi ya watu duniani. Gazeti hilo linasema kwamba ongezeko la idadi ya watu linaonekana kuwa ni mzizi wa matatizo yote ya mwanadamu. Kwa kiasi fulani,mtazamo huo ni sahihi, na hakika ni jambo la fedheha kwa mwanadamu. Lakini gazeti hilo linaeleza kuwa ardhi iliyopo duniani ingelitosheleza kuwalisha binadamu wote mara mbili. Kwa hiyo tatizo siyo ongezeko la watu bali ni ulanguzi wa bidhaa za kilimo zinazotumiwa kwa ajili ya kuzalishia nishati. Mchezo huo unasababisha bei za vyakula kupanda.!

Lakini mhariri wa Westdeutsche anasema nchi zinazoendelea zinapaswa kutekeleza mipango ya uzazi wa majira ili kulitatua tatizo la ongezeko la watu. Mhariri wa gazeti hilo anasema suluhisho limo katika mikono ya nchi zinazoendelea. Lakini nchi za viwanda pia zinapaswa kuzipasia nchi masikini ustadi wa kisasa katika kilimo.

Gazeti la Straubinger Tagblatt linatoa maoni juu ya mgogoro wa madeni barani Ulaya. Ili kuutatua mgogoro huo ,limetolewa pendekezo juu ya kuwa na chombo kimoja cha kuzidhibiti serikali zote. Mhariri wa gazeti hilo anaeleza kuwa ikiwa wapinzani wa utaratibu huo watazidi nguvu,basi huo ndio utakuwa mwisho wa Umoja wa Ulaya.!

Mwandishi/Mtullya Abdu/ Deutsche Zeitungen/

Mhariri/Abdu-Rahman.