1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maoni ya wahariri juu ya Syria na uchaguzi wa Ujerumani

Abdu Said Mtullya17 Septemba 2013

Wahariri wanaizungumzia ripoti ya wakaguzi wa Umoja wa Mataifa juu ya kutumiwa silaha za sumu nchini Syria,na pia wanatoa maoni juu ya uchaguzi mkuu wa Ujerumani

https://p.dw.com/p/19jTH
Wakaguzi wa Umoja wa Mataifa nchini Syria
Wakaguzi wa Umoja wa Mataifa nchini SyriaPicha: Reuters

Kuhusu ripoti ya wakaguzi wa Umoja wa Mataifa juu ya kutumiwa silaha za sumu nchini Syria gazeti la "Der Tagesspiegel" linasema ripoti ya wakaguzi hao imetoa ushahidi juu ya kile ambacho kila mtu aliamini kukijua kwa muda mrefu: kutumiwa kwa silaha za sumu nchini Syria. Lakini mhariri wa gazeti la "Der Tagesspiegel"anaeleza kwamba ripoti ya Umoja wa Mataifa haisemi ni upande gani uliozitumia silaha hizo.

Gazeti la"Osnabrücker"pia linasema sasa pana ushahidi rasmi kwamba silaha za sumu zilitumiwa nchini Syria.Mhariri huyo anasema ushahidi umebainisha kwamba gesi ya sumu aina ya sarin ilitumika,na kwa hivyo ni sahihi kabisa kwa jumuiya ya kimataifa kuweka mkazo juu ya kuondolewa kabisa kwa silaha hizo.

Naye mhariri wa gazeti la "Frankfurter Allgemeine"anakumbusha kwamba mauaji yataendelea nchini Syria hata bila ya silaha za sumu.Mhariri huyo anaeleza kuwa kila siku uhalifu,kama vile wa kuwanyonga watu unatendwa na majeshi ya serikali na waasi. Na kadri vita vya nchini Syria vinavyoendelea ndivyo unyama unavyoongezeka. Na hali haitabadilika, ati kwa sababu Assad amekubali silaha zake za sumu ziondolewe. Makubaliano yaliyofikiwa baina ya Urusi na Marekani yatampa Rais Bashar al-Assad muda wa kuvuta pumzi.

Uchaguzi wa Ujerumani

Wahariri wa magazeti leo pia wanatoa maoni yao juu ya uchaguzi mkuu wa Ujerumani.Mhariri wa gazeti la "Saarbrücker "anasema Wajerumani wengi wanaunga mkono serikali ya mseto mkubwa chini ya uongozi wa Kansela Merkel Mhariri huyo anafafanua kwa kusema wafuasi wa kambi ya kihafidhina wamevunjwa moyo na mseto wa CDU,CSU na Waliberali. Na vyama vya upinzani vya SPD na Kijani havina uwezekano mkubwa. Kilichobakia ni kuunda mseto mkubwa chini ya uongozi wa Kansela Merkel, kwani zaidi ya nusu ya Wajerumani wanaiunga mkono ruwaza hiyo.

Kashfa ya Jürgen Trittin
Gazeti la "Nordwest"linazungumzia kashfa inayomkabili kiongozi wa chama cha kijani Jürgen Trittin wakati imebakia wiki moja kufanyika uchaguzi.

Miaka 30 iliyopita Bwana Trittin alishiriki katika kuipitisha ilani juu ya chama kuhalalisha ngono na watoto wadogo.Juu ya kashfa hiyo gazeti la "Nordwest" linasema Bwana Trittin amekiri kufanya makosa, lakini amekiri baada ya miaka 30. Sasa ni juu ya chama cha kijani kutafakari, iwapo kiongozi wao bado anaweza kuaminika !.

Mwandishi:Mtullya Abdu/Deutsche Zeitungen.

Mhariri:Mohammed Abdul-Rahman