Maoni ya wahariri juu ya Siku Kuu ya Wafanyakazi Duniani | Magazetini | DW | 02.05.2013
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Magazetini

Maoni ya wahariri juu ya Siku Kuu ya Wafanyakazi Duniani

Wahariri wa magazeti ya Ujerumani wanatumia wasaa wa sikuu kuu ya wafanyakazi duniani kutoa maoni yao .

Siku Kuu ya wafanyakazi,Mei Mosi Berlin

Siku Kuu ya wafanyakazi, Mei Mosi Berlin

Mhariri wa gazeti la "Nürnberger Nachrichten"anaiangalia Mei mosi kwa kutilia maanani yanayotokea nchini Ujerumani.Anawalaumu wanasiasa.Mhariri huyo anasema kuwa licha ya hatari kubwa ya wastaafu kukumbwa na umasikini,viongozi wanafumba macho.Kazi za ujira wa chini za leo ndizo zinazowanasa wastaafu katika umasikini hapo kesho.

Mhariri huyo anasema mwenendo huo unaweza kusababisha vurumai za kijamii.Na ili kuiepusha hatari hiyo vyama vya wafanyakazi, leo katika siku ya wafanyakazi vinapigania mageuzi. Na kwa hivyo inahalisi kusema kwamba mnamo mwaka huu vile vile,siku kuu ya wafanyakazi duniani haina umuhimu,zaidi ya kuwa kanuni tu ya kila siku.

Gazeti la "Neue Westfälische" linakubaliana na maoni hayo kwa kusisitiza kwamba, pamoja na kutoa kauli za kutaka hali bora kwa wafanyakazi,ipo haja ya kuzifuatilia kauli hizo kwa kufanya udhibiti.Mhariri wa gazeti hilo anaeleza: "Lengo la kuweka kima cha chini katika mishahara litaendelea kupiganiwa mnamo mwaka huu vile vile nchini Ujerumani."

Mhariri wa gazeti hilo anasema kwenye mikutano ya hadhara hotuba kali zitatolewa kudai kima hicho cha chini cha Euro 8,50 kwa saa. Lakini ambaye amefuatilia kwa makini atatambua kwamba utaratibu huo umekiukwa hasa katika sekta ya ujenzi.Kwa hivyo ,kauli tupu za mapambano hazitoshi.Kinachotakiwa ni kufuatilia kwa kufanya udhibiti,ili kuwalinda wafanyakazi dhidi ya dhulma.

Gazeti la "Donaukurier" linatoa maoni juu ya ndege za kivita zisizokuwa na marubani. Mhariri wa gazeti hilo anasema ni wazi kwamba mjadala juu ya ndege hizo unapaswa kuendelezwa. Anasema ndege hizo zinazoitwa "Drones" zina sifa mbaya kwa sababu Marekani inazitumia katika mapambano dhidi ya magaidi nchini Pakistan na katika nchi nyingine.Lakini swali la kuuliza ni iwapo ndege hizo zina tofauti na silaha nyingine za hatari kama vile mabomu yanayotegwa chini ya ardhi?

Wakati dunia inaadhimisha siku kuu ya wafanyakazi ,gazeti la "Lübecker Nachrichten" linamkumbuka mwanasiasa wa Ukraine ,Julia Tymoshenko,aliekuwa Waziri Mkuu wa nchi hiyo ambae sasa anatumikia kifungo cha miaka saba jela. Mhariri wa gazeti hilo anasema kwamba mkasa wa mwanasiasa huyo unathibitisha kuwa Ukraine haistahiki kuwa mwanachama wa Umoja wa Ulaya.

Mhariri huyo aneeleza kuwa nchi ambayo ,polisi wake na mahakama haziheshimu haki za binadamu haina cha kukitafuta katika Umoja wa Ulaya. Hukumu iliyotolewa na Mahakamu Kuu ya Ulaya ya haki za binadamu kuhusiana na Julia Tymoshenko inaonyesha kuwa Ukraine haistahiki kuwamo katika Umoja wa Ulaya. Kwa nini basi Umoja huo unaisogeza karibu nchi hiyo.?

Mwandishi;Mtullya Abdu/Deutsche Zeitungen/

Mhariri:Mohammed Abdul-Rahman