1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maoni ya wahariri juu ya Papa Benedikt

Abdu Said Mtullya12 Februari 2013

Wahariri karibu wote wanauzungumzia uamuzi wa kujizulu wa Papa Benedikt wa 16. Katika sehemu kubwa ya dunia uamuzi wa Baba Mtakatifu umepokewa kwa mshangao lakini pia kwa matumaini ya kuletwa mageuzi

https://p.dw.com/p/17cgd
Mrithi wa Papa Benedikt atatoka wapi?
Mrithi wa Papa Benedikt atatoka wapi?Picha: AFP/Getty Images

Gazeti la "Stuttgarter Nachrichten"linasema katika maoni yake kwamba uamuzi wa Baba Mtakatifu kujiuzulu unaashiria kigezo kipya ambacho ni sahihi.Papa Benedikt wa 16 ameonyesha kuwa ni kiongozi anaeona mbali na anaeyatekeleza maamuzi.

Mhariri wa gazeti la "Neue Osnabrücker"anasema, ikiwa mtu atayaangalia kwa makini majukumu ya kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani,bila shaka atauelewa uamuzi wa Papa Bededikt wa 16.

Mhariri wa gazeti hilo anaeleza kuwa majukumu ya Kiongozi wa Kanisa Katoliki ni pamoja na kuliongoza kanisa linalowaleta pamoja watu wa tamadamuni mbalimbali katika zama hizi zenye utata.Majukumu ya Papa pia ni kuwateua Maaskofu,kukutana na viongozi wa dunia na mara nyingine kufanya safari zinazohitaji juhudi kubwa.

Mhariri anasema Papa Benedikt wa16 mwenye umri wa miaka 85 ameonyesha uadilifu tofauti na wazee wengi wanaong'ang'ania madaraka.Hata hivyo,hatua ya Papa Benedikt wa16,kujizulu inawapa watu wengi matumaini juu ya kufanyika mageuzi katika kanisa katoliki baada ya mrithi wake kuchaguliwa.

Gazeti la "Reutlinger General Anzeiger"linasema uamuzi wa Papa Benedikt wa 16 kujizulu unastahiki heshima kubwa .Uamuzi huo umetoa ishara mpya kwa uongozi wa kanisa. Naye mhariri wa gazeti la "Lausitzer Rundschau"anaiunga mkono tathmini hiyo kwa kueleza Baba Mtakatifu ameonyesha uadilifu wa hali ya juu. Amejiuzulu kwa hiari yake, hakuna aliemkalia rohoni.

Uamuzi wa Baba Mtakatifu unastahiki,kuheshimiwa na kutambuliwa.

Gazeti la "Main Post" linasema hatua ya Papa Benedikt wa 16 ,kujiuzulu inatoa fursa ya kuleta mageuzi katika kanisa katoliki. Mhariri wa gazeti hilo anaeleza:"Kwa muda wa miaka zaidi ya 30 iliyopita kanisa katoliki limekuwa na muhuri wa wahafidhina kiasi kwamba ni vigumu kwa vijana wa leo kufikiria kitu kingine."

Na mhariri wa gazeti la "Dithmarscher Landeszeitungen"anatilia maanani kwamba Baba Mtakatifu amejiuzulu kutokana na sababu ya uzee. Mhariri huyo anasema Benedikt ,au kwa jina lake halisi,Joseph Ratzinger ameamua kujiweka kando ya Ofisi, lakini ataendelea kuwa mwaminifu wa Kanisa.

Mwandishi:Mtullya Abdu./Deutsche Zeitungen/

Mhariri:Mohammed Abdul-Rahman