1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maoni ya wahariri juu ya kuungana tena kwa Ujerumani

Abdu Said Mtullya21 Novemba 2013

Pamoja na masuala mengine wahariri wanatoa maoni juu ya ripoti kuhusu kuungana tena kwa Ujerumani na juu ya biashara ya silaha

https://p.dw.com/p/1ALp3
Aliekuwa Kansela wa Ujerumani Helmut Kohl akisheherekea muungano katika mji wa Erfurt,1990
Aliekuwa Kansela wa Ujerumani Helmut Kohl in akisheherekea muungano ,katika mji wa Erfurt 1990Picha: picture-alliance/dpa

Na tunaanza na maoni ya gazeti la "Lausitzer Rundschau" juu ya ripoti inayotolewa kila mwaka juu ya kuungana tena kwa nchi mbili za Kijerumani. Ripoti hiyo inasema kwa jumla kwamba upande wa mashariki bado upo nyuma ya upande wa magharibi kuhusu mishahara na utajiri, lakini nao pia unasonga mbele.

Juu ya ripoti hiyo mhariri wa gazeti la "Lausitzer Rundschau "anasema sasa ni sahihi kabisa kukiweka kando kigezo cha tofauti baina ya mashariki na magharibi wakati wa kuamua kutoa fedha kwa ajili ya kuleta maendeleo. Kwani katika upande wa Ujerumani magharibi vilevile zipo sehemu zinazohitaji misaada kwa kila hali.


Naye mhariri wa gazeti la "Eisenacher Presse" anasisitiza umuhimu wa kuyaangalia maendeleo ya nchi nzima ya Ujerumani kwa jumla, badala ya kukizingatia kigezo cha tofauti baina ya mashariki na magharibi. Mhariri huyo anasema ,sasa ni muhimu kuyalinganisha maendeleo, majimbo kwa majimbo na miji kwa miji. Lakini mhariri wa gazeti la "Badische Neueste Nachrichten anayo maoni tofauti na anasema kwamba bado yapo mambo mengi ya kufanyika ili kuziondoa tofauti katika maendeleo baina ya pande mbili za Ujerumani. Lakini kwa ajili hiyo njia nyingine zinahitajika. Utaratibu wa mshikamano,yaani wa kutoa mchango maalumu wa fedha, ambao umekuwa unatumika hadi sasa, umeshapitwa na wakati. Upande wa mashariki mwa Ujerumani unahitaji kuwa na mpango wa uchumi usiotegemea kodi maalumu ili kuweza kutekelezwa.

Biashara ya silaha

Serikali ya Ujerumani imechapisha ripoti juu ya biashara ya silaha inayofanywa na Ujerumani katika nchi za nje. Ripoti hiyo inaonyesha kwamba Ujerumani imeuza silaha chache mwaka uliopita. Mauzo yalipungua kwa asilimia 13.

Gazeti la "General Anzeiger"linatoa maoni juu ya ripoti hiyo kwa kusema kwamba hali ya haki za binadamu ndiyo inayoamua iwapo Ujerumani, iuze silaha au la, kwa nchi yoyote husika. Hilo ndilo jambo la msingi. Kwa hivyo kulingana na msingi huo, Ujerumanji hapaswi kuuza silaha kwa Saudi Arabia. Kwa sababu nchi hiyo imo katika orodha ya mataiafa yanayokosolewa.

Mhariri wa "Münchner Merkur" anasema, katika biashara ya silaha, inapasa kuchagua kati ya maslahi ya kiuchumi na wajibu wa kimaadili. Lakini mhariri wa "Nordwest" anasema ni vigumu kuizuia biashara ya silaha. Anaeleza kuwa silaha ni bidhaa maalum zinazotumika katika kuathiri maamuzi ya kisiasa na kijeshi.Ndiyo sababu wakati mwingine inakuwa lazima kwa Ujerumani kuuza silaha kwa Saudi Arabia. Na haifai kujihadaa: popote pale ambapo watu wanataka kuuana, watatafuta njia ya kuzipata silaha,watauana hata bila ya silaha kutoka Ujerumani.

Mwandishi:Mtullya abdu./Deutsche Zeitungen.

Mhariri: Yusuf Saumu.