1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maoni ya wahariri juu ya Komorowski.

Abdu Said Mtullya6 Julai 2010

Wahariri wa magazeti ya Ujerumani leo wanatoa maoni yao juu ya ushindi wa rais mpya wa Poland Bronislaw Komorowski.

https://p.dw.com/p/OBdb
Rais mpya wa Poland Bronislaw Komorowski na mkewe.Picha: AP

Poland imepata rais mpya, Bronislaw Komorowski.Wahariri wa magazeti ya Ujerumani wanatoa maoni yao juu ya mwanasiasa huyo.

Gazeti la Darmstädter linatilia maanani kuwa Komorowski alishinda kwa kura chache jambo lilanothibitisha mgawanyiko uliopo nchini Poland. Hata hivyo, gazeti linasema ushindi wake unawakilisha mabadiliko. Kwani kwa mara ya kwanza, vijana, na wanasiasa wenye mtazamo wa mageuzi na wanaoenda sambamba na matukio ya dunia wana uwezekano wa kuulekeza mustakabal wa Poland bila ya kukwamishwa na watu wanaong'ang'nia siasa za nyakati zilizopita, na ujuvi wa kizalendo.

Mhariri wa gazeti la Frankfurter Neue Presse anawapongeza watu wa Poland kwa kumchagua Komorowski kwani kwa kufanya hivyo watu hao wameunga mkono uchumi wa soko na mshikamano na Umoja wa Ulaya. Gazeti la Frankfurter Neue Presse ,linatilia maanani kwamba ziara yake ya kwanza itakuwa kwenye makao makuu ya Umoja wa Ulaya,na baadae Ujerumani na Ufaransa.Gazeti hilo linasema kwa kutekeleza siasa ya busara rais mpya wa Poland Komorowski ataweza kuuimarisha uzito wa Poland kwenye Umoja wa Ulaya, kwani hadi sasa wananchi wake wanahisi kuwa hawawakilishwi katika msingi wa usawa kwenye Umoja huo.

Mhariri wa gazeti la Nordbayerische Kurie anautathmini ushindi wa rais mpya wa Poland bwana Komorowski kwa kutanabahisha juu ya matatizo yanayoweza kumkabili katika siku za usoni.

Mhariri huyo anaeleza kuwa Rais wa Poland tofauti na wa Ujerumani, anayo mamlaka yenye usemi mkubwa.Lakini ni muhimu kutilia maanani kwamba Poland pia inapaswa kufanya mageuzi katika sekta ya afya ,malipo ya uzeeni na kuimarisha hazina ya serikali.Mhariri huyo anasema hatua hizo hakika hazitawafurahisha wote nchini Poland. Viongozi katika demokrasia mpya za Ulaya mashariki wanaondolewa madarakani haraka na wapiga kura ikiwa hawatimizi matarajio ya wapiga kura wao .Kwa hiyo wapinzani, yaani akina Kaczynski wanasubiri fursa hiyo ili warejee madarakani.

Na gazeti la Nordwest Zeitung linasifu mafanikio yaliyofikiwa na Poland hadi sasa. Linasema kilichofikiwa nchini humo hadi sasa hakika kinastahili sifa.

Gazeti hilo linasema Poland sasa inapitia katika kipindi cha furaha cha historia yake.Taasisi za demokrasia zimeimarika.Maendeleo yake ya uchumi ni ya kutia moyo.

Gazeti la Nordwest Zeitung linasema Poland sasa imekuwa sehemu thabiti ya Ulaya inayostahili kutiliwa maanani.Na gazeti la Reutlinger General -Anzeiger linamkumbusha rais huyo mpya wa Poland Komorowski kwamba sera ya maridhiano na Urusi lazima isonge mbele na ahadi alizozitoa kwa watu wake zinapaswa kutekelezwa la sivyo watu wake watamtoa nje katika uchaguzi wa bunge utakaofanyika mwakani.

Mwandishi/Mtullya Abdu/Deutsche Zeitungen/

Mhariri/Abdul-Rahman