Maoni ya wahariri juu ya J.Kerry | Magazetini | DW | 27.02.2013
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Magazetini

Maoni ya wahariri juu ya J.Kerry

Wahariri wanatoa maoni yao juu ya siasa ya mambo ya nje ya Marekani,kwa usemi mwingine juu ya ziara ya Waziri wa mambo ya nje wa Marekani,John Kerry,ambaye jana alikuwa hapa nchini Ujerumani.

Waziri wa mambo ya nje wa Marekani John Kerry ziarani nchini Ujerumani

Waziri wa mambo ya nje wa Marekani John Kerry ziarani nchini Ujerumani

Gazeti la"Sudwest Presse" linaitilia maanani ziara ya John Kerry nchini Ujerumani na linasema kuwa ziara hiyo inathibitisha kuwa mshikamano thabiti baina ya Marekani na Ujerumani utaendelea kuwa nguzo ya lazima.

Ziara ya nchini Ujerumani ya Waziri wa mambo ya nje wa Marekani,John Kerry, imeonyesha jinsi Marekani inavyoweka mkazo katika kuimarisha uhusiano wake na bara la Ulaya badala ya bara la Asia.

Hayo anayasema mhariri wa gazeti la"Reutlinger General Anzeiger".Hata hivyo mhariri huyo anatahadharisha:"kwa kumteua John Kerry, Rais Obama anakusudia kuweka mkazo katika kuuimarisha uhusiano na bara la Ulaya.Ushahidi ni mwendelezo wa juhudi za kuimarisha biashara huru baina ya Marekani na nchi za Ulaya.Ziara ya Kerry barani Ulaya pia ushuhuda wa sera mpya ya mambo ya nje ya Marekani lakini pia inapasa kutambua kwamba awali ya yote John Kerry atatingwa na mgogoro wa Mashariki ya Kati.

Bara la Asia:

Mhariri wa gazeti la "Westdeutsche" hana uhakika iwapo Marekani,kweli itaibadilisha sera yake ya nje kuhusiana na bara la Asia na kulipa kipaumbele bara la Ulaya. Mhariri huyo anaeleza: Ukweli ni kwamba bara la Ulaya linapoteza umuhimu wake kwa Marekani ikilinganishwa na bara la Asia. Na kwa kweli hakuna kitachobadilika katika hilo,hata ikiwa Waziri wa mambo ya nje wa Marekani,John Kerry,anaimwagia sifa Ujerumani kwa dhima yake ya uongozi barani Ulaya.Sifa hizo ni ujumbe uliojificha wa kuitaka Ujerumani itoe mchango zaidi katika kuitatua migogoro ya kimataifa.

Uchaguzi wa Italia:

Gazeti la"Sächsiche" linazungumzia juu matokeo ya uchaguzi wa bunge wa nchini Italia.Mhariri wa gazeti hilo anasema matokeo hayo ni funzo kwa nchi za Ulaya juu ya kuidhibiti migogoro.Mhariri huyo anasema endapo viongozi wa Ulaya wangelimpongeza Waziri mkuu wa Italia,Mario Monti,kwa mafanikio aliyoanza kuyapata katika sera za mageuzi,pongezi hizo zingelikuwa na maana ya kupuuza jinsi mamilioni ya Wataliani walivyotamauka juu ya sera hizo.Mamilioni ya watu nchini Italia hawapo tayari tena kuubeba mzigo wa madeni kwa njia ya sera za kubana matumizi.

Swali la kuuliza sasa ni jee,kubana matumizi ndiyo njia ya pekee ya kuutatua mgogoro wa madeni barani Ulaya?Swali hilo linapaswa kujibiwa siyo tu na wale watakounda serikali mpya nchini Italia,bali pia na viongozi na wote barani Ulaya.

Mwandishi:Mtullya Abdu /Deutsche Zeitungen/

Mhariri: Josephat Charo