Maoni ya wahariri juu ya Blatter | Magazetini | DW | 03.06.2015
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Magazetini

Maoni ya wahariri juu ya Blatter

Katika tahariri zao wahariri wa magazeti wanazungumzia juu ya kujiuzulu kwa Rais wa FIFA Sepp Blatter. Pia wanatoa maoni juu ya ziara ya Rais Abdel Fattah al.Sisi nchini Ujerumani

Rais wa FIFA Sepp Blatter ang'atuka

Rais wa FIFA Sepp Blatter ang'atuka

Gazeti la "Weser Kurier " linasema kujiuzulu kwa,Sepp Blatter, Rais wa Shirikisho la vyama vya kandanda duniani,FIFA ni hatua ya kwanza tu. Mhariri huyo anesema jambo muhimu ni kuleta mabadiliko ya mfumo uliojengeka wakati wa uongozi wa Blatter. Mfumo wa kupeana zawadi na hisani.


Naye mhariri wa gazeti la "Stuttgarter" anasema Sepp Blatter ameshaondoka lakini mfumo alioujenga bado upo katika FIFA. Mhariri huyo anasema mfumo huo wa kifisadi lazima uondoke, la sivyo wajihi wa FIFA hautabadilika asilani.

Gazeti la "Neue Osnabrücker" linasema kuondoka kwa Blatter kunafungua njia ya kumpata Rais mpya. Fifa inahitaji muundo mpya utakaotokana na mageuzi ya ndani. Shirikisho la soka duniani linapaswa kuitafuta njia ya kuleta uwazi zaidi na kuufagilia mbali ufisadi. Na gazeti la "Nordwest"linataka uchaguzi ufanyike haraka ili mtu mpya apatikane wa kuiongoza FIFA.

Rais wa Misri al-Sisi apokewa kwa heshima licha ya udhalimu nyumbani

Rais wa Misri Abdel Fattah al -Sisi leo anaanza ziara nchini Ujerumani ambayo ni ya utatanishi: kwani Spika wa Bunge la Ujerumani Nobert Lammert amekataa kukutana na Rais huyo. Mhariri wa gazeti la "Nürnberger" analalamika kwamba liicha ya kukiukwa haki za binadamu kuwa jambo la kila siku nchini Misri, Rais Abdel Fattah al - Sisi anapokewa na heshima zote nchini Ujerumani.

Al-Sisi atakutana na Kansela wa Ujerumani Angela Merkel na pia atakutana na Rais wa Ujerumani Joachim Gauck . Mhariri wa "Nürberger anatilia maanani kwamba al-Sisi amejaribu kurejesha utulivu nchini. Lakini utulivu huo ni wa makaburini, kwa kwa sababu watu wengi wanahukumiwa adhabu ya kifo nchini Misri.

Mhariri wa gazeti la "Kölner Stadt-Anzeiger" pia anatilia maanani kwamba kiwango cha kukiukwa haki za binadamu kimevuka mipaka nchini Misri. Lakini anasema serikali ya Ujerumani imeamua kumwalika Rais al-Sisi kwa madai kwamba bila ya kukutana naye haitawezekana kumkosoa.

Mgogoro wa Ugiriki unaendelea

Gazeti la "Mindener Tageblatt" linasema Waziri Mkuu wa Ugiriki Alexis Tsipras na washirika wake katika serikali ya mseto wanajihadaa kwamba wataweza kuendelea kuwashinikiza wadai wao. Lakini Waziri Mkuu huyo anapaswa kutambua kwamba, serikali yake haitafanikiwa katika sera yake ya kutegemea kulipiwa na fedha za walipa kodi wa nchi nyingine za Ulaya.

Mwandishi:Mtullya Abdu/Deutsche Zeitungen.

Mhariri: Yusuf Saumu