Maoni ya wahariri juu mazungumzo kuhusu biashara huru | Magazetini | DW | 10.07.2013
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Magazetini

Maoni ya wahariri juu mazungumzo kuhusu biashara huru

Wahariri wanatoa maoni juu ya mazungumzo baina ya Umoja wa Ulaya na Marekani, matukio ya nchini Misri na ziara ya Baba Mtakatifu katika kisiwa cha Italia cha Lampedusa.

Rais wa Kamisheni ya Umoja wa Ulaya Jose Manuel Barroso

Rais wa Kamisheni ya Umoja wa Ulaya Jose Manuel Barroso

Wajumbe wa Umoja wa Ulaya na wa Marekani wameanza mazungumzo mjini Washington juu ya kufikia mkataba wa biashara huru baina ya pande mbili hizo kwa manufaa ya watu milioni 820. Mkataba huo utakuwa wa eneo kubwa kabisa la kibiashara duniani. Hata hivyo mazungumzo hayo yamegubikwa na kashfa ya upelelezi. Mhariri wa gazeti la "Berliner Morgenpost "anatoa maoni yake.

"Shutuma zinazotolewa barani Ulaya kuhusu kashfa ya upelelezi wa mashirika ya ujasusi ya Marekani hazina maana ya kuwa chuki dhidi ya Marekani." Lakini gazeti linasema ikiwa Marekani itabebeshwa lawama juu ya maovu yote yanayotendeka duniani hiyo ndiyo itakuwa chuki dhahiri. Watu wa mrengo wa shoto nchini Ujerumani wanajaribu kutoa picha hiyo juu ya Marekani.

Juu ya mazungumzo yaliyoanza Washington baina ya Umoja wa Ulaya na Marekani kuhusu kufikia mkataba wa biashara huru,gazeti la "Cellesche" linasema,kuondolewa kwa ushuru na vizingiti vya biashara, kutakuwa chachu ya ustawi pia kwa nchi kama Ujerumani zinazouza bidhaa nje kwa kiwango kikubwa.Na kwa hivyo suala la upelelezi halipaswi kuwa kigingi cha kuyazuia mazungumzo hayo.

Naye mhariri wa gazeti la "Kölner Stadt-Anzeiger" anasisitiza umuhimu wa mazungumzo hayo kwa kusema kwamba mambo mengi yatazingitiwa kwenye mazungumzo hayo, ikiwa pamoja na tunu za utamaduni.Lakini kitovu cha mazungumzo ni biashara itakayoleta ustawi wa uchumi na hivyo kuwezesha kutengwa kwa nafasi za ajira.

Mhariri wa "Donaukurier "anasema mkataba juu ya kuunda eneo la biashara huru ,ndilo jawabu la njama zinazofanywa na China duniani katika sekta ya biashara.

Mhariri wa gazeti la "Reutlinger General-Anzeiger"anazungumzia juu ya hali ya nchini Misri. Anasema hakuna uwezekano wa kuwashirikisha Waislamu wenye itikadi kali katika serikali ya mpito nchini Misri. Na kufanyika kwa uchaguzi mpya wa haraka siyo njia ya manufaa. Misri sasa ina Rais wa kipindi cha mpito lakini haina katiba. Ndiyo kusema Rais huyo punde tu atazifuata nyao za Husni Mubarak.

Gazeti la "Der neue Tag" linatoa maoni juu ya ziara ya Baba Mtakatifu,Francis wa kwanza , katika kisiwa cha Italia, cha Lampedusa ambako wahamiaji, pia kutoka Afrika wamekwama, na hivyo kulazimika kuishi katika hali mbaya.

Mhariri wa gazeti hilo anaeleza kuwa ziara ya Baba Mtakatifu katika kisiwa cha Lampedusa inaonyesha kwamba kiongozi huyo wa Kanisa Katoliki duniani, imeiweka hadhi ya mwanadamu moyoni mwake na kwamba hachoki kuzikumbusha jamii na serikali juu ya maana ya hadhi ya mwanadamu. Baba mtakatifu anajaribu kuwarudisha katika jamii, wale waliowekwa pembeni na jamii hizo.

Mwandishi:Mtullya abdu/Deutsche Zeiutngen.

Mhariri:Mohammed Abdul-Rahman