1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

UN Kongo

Abdu Said Mtullya1 Oktoba 2010

Wakati sasa umefika wa kuwachukulia hatua wote waliotenda uhalifu katika Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo.

https://p.dw.com/p/PSS8
Wanawake mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo wamo hatarini kubakwa wakati wowote!Picha: picture-alliance / Godong

Umoja wa Mataifa umesema leo kwamba uhalifu wa kivita na hata mauaji halaiki huenda yamefanyika katika Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo.Umoja wa Mataifa umesema hayo katika ripoti yake iliyotolewa rasmi leo .

Yafuatayo ni maoni ya mwandishi wetu Ute Schaeffer juu ya ripoti hiyo.


Wakati wa vita vya kwanza katika Kongo ya Mobutu nchi hiyo ilitumbukia katika vurumai na mauaji makubwa. Majeshi kutoka nchi kadhaa jirani yaliingia mashariki mwa Kongo na kupigania raslimali na kupigana dhidi ya utawala wa Kongo.

Majeshi ya Rwanda yaliyoivamia Kongo mnamo mwaka wa 1996 yamelaumiwa na Umoja wa Mataifa kwa mauaji ya maalfu ya wahutu.

Ripoti ya Umoja wa Mataifa inaonyesha jinsi sasa ukweli ulivyomfikia rais Paul Kagame wa Rwanda.

Anasherehekea kuwa mkombozi wa nchi yake-aliikomboa Rwanda kuondokana na mauaji halaiki. Na kwa nini asifanye hivyo-? ama kwa hakika ni watu wa Rwanda wenyewe waliojikomboa.

Kagame pia ambaye wakati huo alikuwa kamanda wa jeshi la waasi wa kitusi pamoja na wapiganaji wa RPF waliyazima mauaji halaiki. Kagame na wapiganaji wa RPF waliingia Rwanda kutokea Uganda na kuyakomesha mauaji ya watusi na wahutu waliokuwa na mtazamo wa ukadirifu. Lakini watu alfu mia nane waliangamizwa.

Na kwa muda wa siku mia moja dunia ilikuwa inatazama tu bila ya kufanya chochote.

Hadi leo Kagame ni maaruf kutokana na kuyazima mauaji hayo. Kagame ni rais aliewarejeshea watu wake mustakabal.Yeye ndiye alieleta amani nchini Rwanda.Wananchi wengi wa nchi yake wana uhakika juu ya hayo. Na ndiyo sababu wamemchagua tena awaongoze. Katika uchaguzi wa rais uliofanyika mnamo mwezi wa agosti walimpa asilimia 93 ya kura.

Lakini Kagame analo doa.!

Ripoti iliyotolewa na Umoja wa Mataifa, katika msingi wa taarifa za watu walioshuhudia, imeonyesha jinsi Kongo ya mashariki ilivyotumbukia katika vurumai na mauaji,jinsi maalfu ya wanawake walivyobakwa na jinsi maalfu kwa maalfu ya watu walivyouawa.

Jeshi la Rwanda lilihusika.Kagame ambaye wakati huo alikuwa waziri wa ulinzi aliyaamrisha majeshi ya Rwanda yaivamie Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo mnamo mwaka wa 1996.

Lengo la uvamizi huo lilikuwa kuwasaka wanaitikadi kali wa kihutu waliokuwa wamejificha mashariki mwa Kongo.Lakini kampeni ya mabavu ya majeshi ya Rwanda haikuwalenga wahutu tu bali pia watoto,wanawake na wazee.

Vita vya karibu miaka 20 vimeacha muhuri wa matumizi ya nguvu. Kutokana hali hiyo mauaji halaiki na matendo ya ubakaji yanatokea mara kwa mara hadi leo.

Ujumbe uliowasilishwa na Umoja wa Mataifa katika ripoti yake unasema,wakati sasa umefika wa kuwachukulia hatua waliohusika na mauji,ubakaji na uhalifu wote katika Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo.

Waliotendewa uhalifu wanastahili kupewa sauti.Wote waliotenda uhalifu katika vita vya Kongo lazima waadhibiwe.

Lakini hakuna dhamira ya kisiasa ya kuwezesha kuchukuliwa hatua hizo:siyo katika nchi jirani, ambazo pia zinahusika, wala katika Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo.

Ripoti ya Umoja wa Mataifa inatilia maanani kwamba hakuna anaejaribu kuyaweka katika safu moja mauaji halaiki ya mwaka 1994 na kukiukwa haki za binadamu za wahutu. Lakini kujaribu kuipotosha historia kama anavyojaribu kufanya Kagame siyo msingi wa amani katika Afrika ya Kati. Huu siyo wakati wa kutazama pembeni-siyo Kigali,Kinshasa,Washington ama London.

Mwandishi/Ute Schaeffer/Afrika/Nahost/

Tafsiri/Mtullya Abdu/

Mhariri/Josephat Charo