Maoni: Ujerumani yataka mdahalo mwengine | Uchaguzi wa Ujerumani 2017 | DW | 24.09.2017
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

MAONI

Maoni: Ujerumani yataka mdahalo mwengine

Ujerumani imeamua kumrejesha Angela Merkel kwenye nafasi yake ya ukansela lakini anasema mhariri mkuu wa DW, Ines Pohl, kuwa uchaguzi huu una ujumbe mmoja wa wazi na wawili walioshindwa: SPD na Angela Merkel. 

Chama cha Social Democrat (SPD) kimevunja rikodi ya kuanguka kwa kupata asilimia 20.8, na chama cha Christian Democratic Union (CDU) cha kansela, kimepoteza takribani asilimia nane na kitu. 

Kushindwa kubaya huku – na katika nyakati za kawaida – kungelikuwa sababu ya kufikiria kujiuzulu.

Lakini hizi si nyakati za kawaida kwa hali ya Ujerumani. Ukweli huu unaakisika, yumkini, kwenye mafanikio ya Chama Mbadala kwa Ujerumani (AfD), ambacho kimejizolea asilimia 13 kwenye Bunge la Shirikisho (Bundestag). 

Na, kwa hivyo, kwa mara ya kwanza tangu kuasisiwa kwa Jamhuri ya Shirikisho la Ujerumani, kinaingia chama cha siasa kali za mrengo wa kulia kwenye bunge la Ujerumani.

Nchi hii imekuwa tafauti

Ni mkato wa kihistoria. Kwa uchaguzi huu wa leo, nchi hii imekuwa nchi tafauti. Huku si kukosekana kwa umakini. Lakini pia si janga. Ni changamoto tu. 

Baada ya yote, hii ndiyo demokrasia. Na kwa kuchukuwa mtazamo mpana wa kilimwengu, kuna sababu njema za kuamini kuwa Ujerumani itaimudu changamoto hii vyema.

Na kwamba itakuwa pia vyema ikiwa bunge kwa mara nyengine tena litalumbana kwa kutumia hoja bora zaidi. Na wala sio kuwa na "zidumu fikra za kansela" kwa kuwa hapana upinzani wa maana.

Huu ndio pia ujumbe usiku huu.

Ines Pohl (DW/P. Böll)

Mhariri Mkuu wa DW, Ines Pohl

Kitu cha msingi ni kuwa vyama vya kidemokrasia havipaswi kuondoshwa kwenye njia ya kidemokrasia kwa andasa za ushindi wa AfD. Vinapaswa, badala yake, kukabiliana na majaribu ya upotoshaji wa siasa kali za mrengo wa kulia na kusaka majibu halisi kwa matatizo yaliyopo.

Na mwisho, wachukulie kwa umakini wasiwasi wa watu wengi juu ya ambavyo wingi wa wakimbizi unaweza kuibadilisha nchi yao wenyewe.

Ujerumani inapaswa kufikiria mdahalo huu. Khofu dhidi ya mambo yachukuliwayo kuwa ni mwiko huimarisha mirengo ya siasa kali. 

Huu ndio pia ujumbe wa uchaguzi huu.

SPD yaenda kwenye upinzani 

Changamoto ya kwanza kubwa itakuwa ni kuunda serikali. Ni jambo linalotilika maanani kwamba hapo hapo SPD ilibainisha wazi kuwa itakwenda kwenye upinzani. Hii ndiyo njia pekee ya kusaka mtazamo mpya na kuanzisha mtazamo wa huko mbeleni. Na zaidi ya hayo, kwa uamuzi huu, ndiyo tu inaweza kuizuia AfD kuongoza upinzani bungeni.

Angela Merkel ameumizwa vibaya kwenye majadiliano haya yanayokanganya. Tayari ana zigo la lawama mabegani mwake kutokana na sera yake ya wakimbizi, ikionekana kuwa sababu ya kushindwa chama chake kufanya vyema sana. 

Na, kwa upande mwengine, ulimwengu mzima unatarajia kwamba licha ya matokeo haya, atabakia kuwa mmoja wa wanasiasa wakuu kwenye ulimwengu wa Magharibi, na ambaye kwa uongozi wake Ujerumani itaendelea kubakia kuwa mshirika wa aliyetangamaa na anayeaminika kwenye majukwaa ya dunia. 

Juu ya yote, la kukumbukwa ni kuwa hii ni nchi ya uwazi na iliyozama kwenye demokrasia. Hilo linaungwa mkono na Katiba ya Ujerumani. Na hilo linawahusu wote, hata AfD. Kifungu cha 1: Heshima ya mwanaadamu haiwezi kuvunjwa.

Mwandishi: Ines Pohl
Tafsiri: Mohammed Khelef
Mhariri: Sylvia Mwehozi
 

Matangazo

Sikiliza Matangazo Yetu

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com