1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

13 Februari 2017

Frank-Walter Steinmeier amechaguliwa kuwa rais wa Ujerumani. Katika hotuba yake, alitaka kuwapa moyo watu wawe majasiri. Katika maoni yake Christoph Strack anasema Steinmeier mwenyewe anatakiwa kuonyesha ujasiri.

https://p.dw.com/p/2XRs5
Berlin Wahl des Bundespräsidenten Antrittsrede Steinmeier
Rais mteule wa Ujerumani, Frank-Walter SteinmeierPicha: picture-alliance/dpa/B. von Jutrczenka

Je, kuna maneno yoyote ambayo yanaweza kutumiwa kama kaulimbiu ya mwanzo wa urais wa Frank-Walter Steinmeier? Kulikuwa na neno moja, neno fupi, lenye nia kubwa, ambalo alilirudiarudia katika hotuba yake baada ya kuchaguliwa kuwa mkuu wa nchi: Neno hilo ni 'Ujasiri'. Steinmeier alihitimisha hotuba yake kwa maneno haya; 'Tuwe majasiri, na kwa hali hiyo, sitakuwa na hofu ya siku za usoni'.

Tarehe 19 Machi Steinmeier atachukuwa rasmi wadhifa wa urais wa Ujerumani, akimrithi Joachim Gauck. Yeye atakuwa rais wa 12 wa Shirikisho la Ujerumani. Kauli mbiu ya Steinmeier, 'Ujasiri', inafuata nyayo za kanuni iliyomuongoza rais Gauck, ambayo ilikuwa, 'Uhuru'. Kwa hiyo Steinmeier anataka kuwapa hamasa watu.

Steinmeier alidhihirisha hali hiyo katika hotuba yake. Alizungumzia kuenea kwa hali ya sintofahamu miongoni mwa watu wa Ujerumani, na wasiwasi kuhusu demokrasia, akisema, 'inaonekana dunia haiendi ipasavyo'.

Strack Christoph Kommentarbild App
Christoph Strack-DWPicha: DW

Ikiwa Steinmeier mwenye umri wa miaka 61 anataka kuwahamasisha watu, hawezi kufanya hivyo tu kwa kupigia debe jamii yenye uwazi. Hapana. Steinmeier pia atalazimika kutoa mchango wake katika kuziba pengo lilolopo kati ya siasa na 'wao', maana yake - wale wanaojisikia kusahauliwa na mfumo wa utawala.

Inawezekana kwa rais wa Ujerumani kuwafikia watu ambao siasa haziwezi kuwafikia tena. Lakini kama anataka kuwa mhamasishaji, itambidi Steinmeier kuchagua maneno yake, kupunguza lugha ya kidiplomasia, apunguze maneno matamu- Ndio, aonyeshe ujasiri zaidi ya aliouonyesha alipokuwa waziri wa mambo ya nchi za nje.

Rais anayeondoka, Joachim Gauck, kama mtu aliyewahi kuwa mchungaji, nguvu zake zilidhihirika, na zinaendelea kudhihirika kupitia kauli yake, ambayo aghalabu huwa ya nguvu, na hunasa kwenye mawazo yako. Huo ni upeo ambao itambidi Steinmeier kuufikia, ikiwa, kama alivyosema kabla ya kuchaguliwa, anataka kutoa mchango katika kunusuru uhalisia wa demokrasia.

Kama anataka kufika katika upeo huo, atalazimika kukaza buti kwa kiwango kikubwa, hususan katika hotuba muhimu za kiofisi. Katika hilo, hatuna zaidi ya kumtakia kuwa jasiri.

Mwandishi: Christoph Strack

Tafsiri: Daniel Gakuba

Mhariri: Mohammed Khelef