1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

maoni: Mvutano wa ushuru kati ya Marekani na Umoja wa Ulaya

Zainab Aziz
1 Juni 2018

Marekani imetimiza ahadi yake ya kuongeza ushuru kwa bidhaa za bati na chuma cha pua kutoka nchi za Umoja wa Ulaya. Mwandishi wa DW Timothy Rooks asema kuna haja ya kutofautisha kati ya vitisho na kutokuwepo na usawa.

https://p.dw.com/p/2yob3
USA Nashville Trump Rally
Picha: picture-alliance/AP Photo/A. Harnik

Biashara ya kimataifa haizingatii haki wala haina usawa. Na mtu yeyote anayesema vinginevyo basi hasemi ukweli au labda haijui historia au safu ya usawa wa kimataifa. Kulinganisha mizani ya usawa ni hatua nzuri lakini haiwezi kupatikana kwa njia ya mapambano.

Hata hivyo ushuru mpya wa Marekani wa asilimia 25 wa kuagiza bidhaa za bati na asilimia 10 kwa bidhaa za chuma cha pua kutoka Umoja wa Ulaya, Canada na Mexico sasa ni rasmi.

Kama ilivyotarajiwa, Marekani haijakubali kushinikizwa na washirika wake. Donald Trump amekataa ushauri wa wizara yake ya ulinzi pamoja na ushauri wa watengeneza magari, bila ya kuwepo na ulazima anaiondoa sehemu kubwa ya ulimwengu kutoka kwenye mchakato huo.

Watu wa Ulaya ya Magharibi wana haki ya kuwa na hasira, na wengi wanataka hatua za haraka za kulipiza kisasi kwa kuongezewa ushuru kwenye vyakula vinazoingizwa Ulaya kutoka Marekani kama vile vinywaji vikali. Lakini  kundi la nchi 28 tofauti yaani Umoja wa Ulaya, kuyasema hayo kwa kauli moja si jambo rahisi.

Umoja wa Ulaya mara nyingi huwa unaogopa na wakati huohuo kutaka kumfurahisha kila mtu. Mexico kwa upande mwingine tayari imeonyesha ujasiri wake kwa kuongeza ushuru kwa baadhi ya bidhaa ilizozichagua kama hatua ya kulipiza kisasi. Na ingawa hakuna mtu anayepata faida kutokana na vita vya biashara, Marekani inaambatana na njia yake ya kwenda peke yake.

Rais wa kamisheni ya Ulaya Jean-Claude Juncker
Rais wa kamisheni ya Ulaya Jean-Claude JunckerPicha: picture-alliance/AP Photo/O. Matthys

Hata hivyo utawala wa Trump unaona mbinu hii ni kama silaha ambayo inaweza kuitumia kumbabaisha mtu yeyote inayomuona kuwa dhaifu, ambayo kwa Wamarekani wengi  ina maana ya kuwa ni kwa kila mtu. Kwa upande wake,Trump anajulikana kwa muda mrefu katika ulimwengu wa biashara kwa vitisho na fujo zake, lakini sasa mbinu hizi zenye uzoefu mdogo wa kanuni za msingi zinapindua kwa makusudi miongo kadhaa ya ushirikiano wa karibu na kwa huzuni zinageuka kuwa ndio utaratibu wa utendaji kazi wa Marekani.

Lakini utafiti mpya wa kituo cha Ujerumani cha Uchumi wa Kimataifa katika taasisi ya Ifo unaonyesha kwamba hakuna usawa katika masuala ya ushuru baina ya Marekani- Umoja wa Ulaya, na kwamba wastani wa ushuru wa kuagiza unaotozwa na Marekani kweli ni wa chini kuliko ule unaotozwa na Umoja wa Ulay. Bila ya kuziangalia taarifa kwa undani Trump kweli yuko sawa.

Wamarekani wanalipa asilimia 10 ya kutuma magari yao Ulaya, wakati Waulaya wanalipa asilimia 2.5 tu kwa kuingiza magari yao Marekani. Licha ya ukweli huu usio pingika kitakwimu, pande zote mbili zinakabiliwa na mashindano na haziwezi kuona njia za wazi zitakazoweza kuokoa haki hiyo, kuziokoa ajira na kuendelea kuingiza na kutoa bidhaa kama kawaida.

Waulaya wanataka kuweka vikwazo zaidi vya biashara na kuipeleka kesi yao mbele ya Shirika la Biashara Duniani (WTO) Marekani nayoinazidi kuwa mkaidi kila uchapo. Hatimaye haijalishi kama vitendo hivi vinafuata sheria au vinakiuka sheria za WTO. China inaweza kuingia kwa urahisi kujaza pengo kama linavyofanya huko nchini Iran.

Mwandishi:Zainab Aziz/Rooks, Timothy

Mhariri:Mohammed Abdul-Rahman