Maoni: Museveni ishara mbaya kwa demokrasia | Uganda Yaamua 2016 | DW | 01.02.2016
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Uchaguzi Mkuu Uganda 2016

Maoni: Museveni ishara mbaya kwa demokrasia

Imetimia miaka 30 tangu rais wa Uganda, Yoweri Museveni, alipoingia madarakani. Mkuu wa Idhaa ya Kiswahili, Andrea Schmidt, anasema Museveni amebadilika kutoka mpigania uhuru hadi mtawala wa kibabe.

Museveni amefanikiwa kufanya jambo ambalo viongozi wenzake wa barani Afrika, kama vile rais wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo, Joseph Kabila na Pierre Nkurunziza wa Burundi hawajafanikiwa: Amekaa madarakani kwa miaka 30 na hakuna ishara kwamba utawala wake utakwisha hivi karibuni, kwani alibadili katiba ya nchi yake na hivyo kumpa nafasi ya kugombea tena katika uchaguzi wa Februari 18.

Wakitumia kisingizio kwamba wao tu ndio wanaoweza kuhakikisha uthabiti wa nchi zao, viongozi wenye uchu wa madaraka wanagandamiza wapinzani nchini mwao, bila kujali kwamba kwa kufanya hivyo wanaongeza hatari ya vita vya wenyewe kwa wenyewe. Hilo sasa linashuhudiwa nchini Burundi. Viongozi kama Museveni wanatumia mali za nchi kwa maslahi yao wenyewe, ikiwa ni pamoja na kufadhili kampeni zao za uchaguzi. Aidha, wanadhibiti haki za asasi za kiraia. Uhuru wa habari nao umepunguzwa vikali. Inadaiwa kwamba vyombo vinavyoshughulikia uchaguzi nchini Uganda vinafanya kazi kwa uhuru na kwa kujitegemea, wakati wizi wa kura unaonekana kupewa nafasi kubwa.

Hakuna wa kuchukua nafasi ya Museveni?

Schmidt Andrea Kommentarbild App

Mkuu wa Idhaa ya Kiswahili ya DW, Andrea Schmidt

Museveni ni mmoja wa viongozi wa muda mrefu Afrika, ambao awali walisimama kupigania ukombozi wa wananchi, lakini baada ya kulewa madaraka, wakapoteza lengo lao. Museveni alipoingia madarakani mwaka 1986, alisema kwamba tatizo la Afrika ni kuwa viongozi wake wanatawala kwa muda mrefu mno na hivyo kuruhusu rushwa kunawiri na baadhi ya watu kuweza kukwepa mkono wa sheria. Leo, kiongozi huyo mwenye miaka 71 ana mtazamo tofauti. Anaamini kwamba yeye tu ndiye anaweza kuhakikisha ukuaji wa kiuchumi na amani katika nchi yake. Anadhani kwamba hakuna mwanasiasa mwingine anayeweza kuitawala nchi yake. Museveni hajali kuhusu kutanda kwa rushwa, ukiukwaji wa haki za binadamu, umaskini na ukosefu wa ajira.

Sehemu kubwa ya raia wa Uganda ni vijana na wengi wao hawajawahi kumfahamu rais mwingine zaidi ya Museveni. Ingekuwa vizuri kama wao wangepata nafasi ya kujikomboa na kuleta mabadiliko kutoka kwa utawala wa kibabe hadi utawala wa demokrasia.

Mwandishi: Andrea Schmidt

Tafsirir: Elizabeth Shoo

Mhariri: Daniel Gakuba

Matangazo

Sikiliza Matangazo Yetu

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com