1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maoni: Moyo wa jiwe wa Ulaya

Bernd Riegert/Mohammed Khelef10 Machi 2016

Kwa ujumla, kitu pekee inachokifanya sasa Umoja wa Ulaya kwenye suala wa wakimbizi ni kujaribu kulikumbiza tatizo hilo mbali kabisa ya mipaka yake jambo ambalo linaufukuza pia ubinaadamu, anaandika Bernd Riegert.

https://p.dw.com/p/1IAFs
Mkimbizi mtoto mdogo kwenye mji Idomeni nchini Macedonia.
Mkimbizi mtoto mdogo kwenye mji Idomeni nchini Macedonia.Picha: Getty Images/AFP/L. Gouliamaki

Kura ya turufu ya Ujerumani kwenye mkutano maalum wa kilele wa Umoja wa Ulaya hapo Jumatatu ilipelekea masaa kadhaa ya kupigania juu ya kauli ikiwa ama njia ya Balkan inafungwa moja kwa moja au bado.

Bado akiendelea kupigania suluhisho tafauti la Ulaya, Kansela Angela Merkel alitaka kuwe na maneno mepesi kidogo kwenye tamko la mwisho. Lakini masaa 24 tu baadaye, mataifa wanachama wa Umoja wa Ulaya – Slovania na Croatia – yakaumba ukweli mpya kwa kuifunga rasmi na moja kwa moja mipaka yao. Maana yake ni kuwa hakuna hatua ya pamoja.

Ni wazi kabisa kuwa Angela Merkel amepoteza mamlaka yake aliyokuwa nayo Ulaya. Je, hii bado ndiyo Ulaya yako, Bibi Merkel?

Funga na rudisha nyuma, kwa muhtasari hiyo ndiyo kaulimbiu ya makubaliano na Uturuki. Ndivyo ilivyokuwa dhahiri kwenye Bunge la Ulaya, jana Jumatano. Baraza la Umoja wa Ulaya – ambalo linaundwa na wakuu wa serikali na dola – na Kamisheni ya Umoja huo hawakutuma wakuu wao, bali manaibu ambao walizimwa kirahisi. Kulikumbizia tatizo la wakimbizi kwa Uturuki na kukamilisha matengenezo ya ngome ya Ulaya kukawasilishwa kama ndiyo “suluhisho la Ulaya.”

Mwandishi wa DW kwa masuala ya Ulaya, Bernd Riegert.
Mwandishi wa DW kwa masuala ya Ulaya, Bernd Riegert.

Jambo hili linatia uchungu sana, si la kibinaadamu. Watu ambao tayari wametelekezwa nchini Ugiriki mbele ya milango iliyotiwa makomeo ya Ulaya, hata hawakutajwa kwenye matamko rasmi.

Mwanasiasa wa mrengo wa shoto, Gabi Zimmer, alikuwa pekee aliyetaka Idomeni, mji wa mpakani unaoashiria jaala ya wakimbizi, akiikosoa biashara ya wakimbizi na urudishwaji wa lazima wa maelfu ya watu kulikokubaliwa baina ya Uturuki na Umoja wa Ulaya.

Ugiriki haina uwezo wowote wa kushughulikia msiba huu wa kibinaadamu kwenye mpaka wake. Fedha zilizoahidiwa kutolewa na Umoja wa Ulaya zitapatikana tu miezi kadhaa ijayo, wakati Ugiriki yenyewe inahitaji marekebisho ya kwanza ya sheria ya bajeti yake. Kamisheni ya Umoja wa Ulaya haijaanzisha mpango wowote wa dharura kuwasaidia maelfu ya wahamiaji waliotelekezwa nchini Ugiriki, licha ya kuwa na nguvu za kufanya hivyo. Lakini kwa nini?

Akizungumza mbele ya Bunge la Strasbourg, Kamishna wa Shirika la Wakimbizi la Umoja wa Mataifa aliutuhumu Umoja wa Ulaya kwa kupanga kuvunja sheria, na kuchagua njia ya kishenzi. Umoja huo na mataifa yanayotaka kujiunga nayo kwenye eneo la Balkan kwa makusudi kabisa wanatengeneza janga kwa watu walio mpakani mwa Ugiriki na Macedonia. Hivi kipi chengine kinapaswa kutokea ili roho ya imani iwaingie wakuu wa serikali na dola barani Ulaya?

Mwandishi: Bern Riegert
Tafsiri: Mohammed Khelef
Mhariri: Iddi Ssessanga