1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Magaidi wa "Daesh" wakaribia kusambaratika?

29 Machi 2016

Mji wa Palmyra umekombolewa na majeshi ya serikali ya Syria. Katika maoni yake mhariri mkuu wa DW Alexander Kudascheff anasema tukio hilo lina maana zaidi ya kuurudisha tena mji huo katika mikono ya serikali.

https://p.dw.com/p/1ILEp
Mji wa Palmyra wakombolewa
Mji wa Palmyra wakombolewaPicha: picture-alliance/dpa/V.Sharifulin

Ni jambo linaloonekana dhahiri sasa. Magaidi wanaojiita dola la kiislamu wanarudi nyuma. Mji wa Palmyra maarufu kwa turathi za kale sasa umo tena katika mikono ya serikali.

Ni ishara muhimu, lakini pia kijeshi ni hatua ya manufaa. Sasa majeshi ya Rais Bashar al-Assad yanaweza kusonga mbele hadi kwenye kitovu cha magaidi wa "dola la kiislamu" katika mji wa Raqqa.

Wakati huo huo majeshi ya Iraq yanajiandaa kuingia katika mji wa Mosul na ikiwa hatua hizo zitafanikiwa, wigo wa Waislamu hao wenye itikadi kali utazidi kunywea.

Hata hivyo hiyo haina maana kwamba bara la Ulaya halitaendelea kukabiliwa na hatari ya kushambuliwa na magaidi. Kwani huenda hatari ya mashambulio ikaongezeka kutokana na magaidi wa "Daesh" kutimuliwa kutoka kwenye maeneo waliyokuwa wanayadhibiti na kuyatumia kama kambi zao. Lakini sasa kambi hizo zimebanwa kiasi kwamba magaidi wa "dola la kiislamu" wanatapatapa.

Mhariri Mkuu wa DW Alexander Kudascheff
Mhariri Mkuu wa DW Alexander KudascheffPicha: DW

Jambo moja ni wazi,kwamba wauaji hao sasa wamebanwa sana kijeshi na ndiyo sababu kwamba ni wapiganaji wachache wanaoenda kujiunga nao.

Faraja kwa watu wa Syria na Iraq

Kutokomea kwa "dola la kiislamu", kukomeshwa unyama wa kila siku unaofanyika kwa kuitumia dini ya kiislamu, ni jambo la faraja kwa watu wa Syria na Irak waliosibika chini ya Waislamu hao wenye itikadi kali.

Kutokana na ushindi wa majeshi ya Assad katika mji wa Palymra kutokana na msaada wa Urusi, urari wa kijeshi umebadilika katika kanda inayozijumuisha Syria na Irak. Mamlaka ya Assad yamethibiti kuwa jambo la uhakika. Yeyote anaetaka amani au anaetaka kuvimalizika vita vya nchini Syria lazima apige hodi kwa Assad.

Hata hivyo ukweli huo unauma kwa wapinzani waliopo nje ya Syria wanaopigania demokrasia nchini mwao. Lakini hiyo ndio hali halisi ya kisiasa iliyopo sasa nchini Syria. Assad sasa ni mtu muhimu, licha ya kuendesha vita vya miaka mitano vilivyosababisha vifo vya watu robo Milioni. Assad amethibiti kuwa mtu muhimu tena katika siasa za Mashariki ya Kati.

Lakini pia Urusi inapaswa kuzingatiwa kuwa mshiriki mwenye uzito kwenye meza ya mzungumzo. Urusi imewezesha kupatikana ushindi dhidi ya magaidi wa "dola la kiislamu. Marekani inaangalia , tu, kutokana na kutingwa na shughuli za uchaguzi, licha ya juhudi thabiti zinazofanywa na waziri wake wa mambo ya nje John Kerry. Ulaya inashiriki kwenye mazunguzo, lakini haina uzito wa kupitisha maamuzi.

Magaidi wa "Dola la kiislamu" wanakaribia kusambaratika lakini ugaidi utaendelea nchini Pakistan,Nigeria na barani Ulaya. Uhasama baina ya Washia na Wasuni pia utaendelea kwani jamii hizo mbili zinaendelea kuwania ushawishi katika Mashariki ya Kati na kwingineko.

Mwandishi:Kudascheff,Alexander

Mfasiri:Mtullya abdu.

Mhariri:Iddi Ssessanga