1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maoni: Kwa nini thuluthi moja tu ya Zimbabwe ikapiga kura ya maoni?

18 Machi 2013

Watu wa Zimbabwe wameshiriki katika kura ya maoni ili kuamua juu ya katiba mpya ya nchi yao likiwemo suala muhimu la kuweka utararibu wa mihula miwili tu ya urais, lakini hilo haliwezi kumzuia Rais Robert Mugabe.

https://p.dw.com/p/17zmB

Je, watu wa Zimbabwe walikuwa wanajua tokea mapema ukweli huo na je walikuwa na hofu ya historia kujirudia? Kwani ni theluthi moja tu ya waliostahiki kupiga kura hiyo ndio walioshiriki katika kupiga kura ya maoni kuamua juu ya mswada wa katiba mpya inayozingatiwa kuwa ya kihistoria.

Hata hivyo, wananchi wengi wamelalamika kuwa hawaujui mswaada huo wa kurasa mia moja kwani baina ya kuchapishwa na kuupigia kura, palikuwa na muda wa mwezi mmoja tu.

Baadhi ya watu walijiweka mbali na upigaji kura, kwa sababu ya kupinga hatua ya vyama vya kisiasa bungeni kuishughulikia hati hiyo muhimu peke yao.

Mkuu wa Idara ya Afrika, Claus Stäcker.
Mkuu wa Idara ya Afrika, Claus Stäcker.Picha: DW

Asasi za kiraia ambazo kwa muda wa miaka 15 zimekuwa zinaipigania kwa moyo wote katiba hiyo mpya, ziliwekwa pembeni kabisa. Mchakato wote wa miaka mitatu juu ya katiba hiyo ulitekwa nyara na mawakala wa chama cha kisiasa cha Rais Mugabe.

Katiba ya Mugabe?

Kwa hiyo mswada huo wa katiba mpya sio ishara ya mabadiliko, sio ishara ya mapambazuko ya demokrasia halisi. Ni mswaada wa katiba dhaifu utakaopunguza kidogo tu mamlaka ya Rais Mugabe anayemanika kushindwa katika uchaguzi mkuu wa mwaka wa 2008.

Mugabe, ambaye sasa umri wa miaka 89, ataendelea kuwa kama ambavyo amekuwa. Kabla hata hawajafika vizuri nyumbani kutoka kwenye vituo vya kupigia kura, baadhi ya wapiga kura tayari waliuona mkono wa askari kanzu wa Mugabe.

Maafisa wa usalama waliipekuwa ofisi ya Waziri Mkuu Morgan Tsvangirai aliyemo katika serikali ya mseto kwa shingo upande. Watu watano kutoka kambi yake walitiwa ndani, ikiwa pamoja na mshauri mwandamizi na wakili mashuhuri Beatrice Mtetwa.

Watu wanakamatwa kwa mara nyingine tena kwa wingi. Watu wa Zimbabwe wanajua kwamba tokea miaka mingi chaguzi nchini mwao huandamana na ghasia. Serikali nchini Zimbabwe ina sura moja tu. Nayo ni ya Mugabe.

Kwa kutumia kampeni ya uzalendo, Mugabe ameweza kurudi tena katika uongozi wa nchi yake. Kampeni hiyo maana yake ni kuyachuka makapuni ya nje.

Hakuna mbadala wa katiba mpya Zimbabwe

Licha ya mapungufu yaliyomo katika mswada wa katiba mpya, hakuna njia mbadala ya kufikia kwenye demokrasia nchini Zimbabwe. Mnamo mwezi wa Julai ama baada ya hapo, uchaguzi wa rais na bunge utakaofanyika nchini Zimbabwe ndio utakuwa kipimo cha mswada huo.

Vikwazo dhidi ya Mugabe havikufua dafu. Ni nchi jirani za Jumuiya ya Mandeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC), hasa Afrika ya Kusini, inayoweza kumuweka sawa Mugabe zikitaka. Vyenginevyo, Mugabe hatabadilika na hakuna anaejua zaidi kuliko yeye wenyewe. Na ndiyo sababu kwamba idadi kubwa watu - theluthi mbili hawakushiriki katika kupiga kura.

Mwandishi: Claus Stäcker
Tafsiri: Abdu Mtullya
Mhariri: Mohammed Khelef