Maoni: Kusonga mbele bila Trump | Matukio ya Kisiasa | DW | 02.06.2017
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Maoni: Kusonga mbele bila Trump

Donald Trump ameiondoa Marekani katika Mkataba wa Mazingira wa Paris, akikinzana na maoni ya kila mwenye busara. Dunia itasonga mbele bila Marekani, na Ujerumani itatoa mchango muhimu. Maoni ya Jens Thurau wa DW.

Kilichotarajiwa kimetokea: Trump amechukua hatua inayokinzana na ushauri kutoka kwa wadau mbalimbali waliomtaka aibakishe Marekani katika Mkataba wa Paris wa Kutunza Mazingira. Marekani iko nje ya mkataba huo, kinyume na maoni ya wataalamu wengi wa masuala ya uchumi na mazingira. Na inavyodhihirika, Trump hang'amui, au hata hajali, jinsi alivyojiweka katika hali ya kutengwa. Kansela Angela Merkel wa Ujerumani amekuwa akizungumzia namna mkutano wa kilele wa nchi za G7 ulivyokuwa wa kukatisha tamaa, ambapo nchi sita zilisimama pamoja, dhidi ya moja, ambayo ni Marekani.

Kujiondoa kwa Marekani kunaleta nchi nyingine pamoja

Tofauti na ilivyokuwa siku za nyuma, mara hii msimamo wa Marekani unazileta nchi nyingine pamoja. Siku za nyuma haikuwa hivyo, pale Marekani iliposita kuhusika, China na India pia zilijiweka pembeni. Lakini sasa nchi hizo za bara la Asia zinapiga hatua zaidi katika kupunguza utoaji wa gesi chafu. Na ni jambo lenye ujumbe mzito, kwamba mnamo wiki ambayo Marekani imezipa kisogo juhudi za kulinda mazingira, viongozi wa serikali za China na India walikuwa mjini Berlin. Viongozi hao sasa watasaidiana na Ulaya kulisukuma gurudumu.

Thurau Jens Kommentarbild App

Mtaalamu wa Mazingira wa DW, Jens Thurau

Mshikamano wa mataifa makubwa, hata kama Marekani haimo, katika kuunga mkono Mkataba wa Paris ni habari njema kwa utunzaji wa mazingira. Hiyo lakini haimaanishi kwamba ujinga wa mwendawazimu mmoja katika Ikulu ya White House hauumizi ulinzi wa mazingira: Kwanza, kwa sababu wanasayansi wanasema hatua za kupunguza athari za mabadiliko ya tabianchi zinapaswa kuanza mnamo miaka michache ijayo, na pili, kwa sababu tayari mataifa mengi, na pia baadhi ya majimbo ya Marekani, yameitikia wito wa kuhamia katika matumizi ya nishati endelevu.

Kujitosheleza katika nishati endelevu

Lakini bado ipo mitambo mingi ya kuzalisha nishati ya mafuta na makaa ya mawe. Ili kufikia enzi ya nishati ya jua, hatua za kupunguza matumizi ya mafuta na makaa ya mawe zinapaswa kuchukuliwa, lakini sasa hatua hizo hazitachukuliwa tena na Marekani.

Ingawa hakuna wamiliki wa viwanda wenye uelewa ambao watawekeza zaidi katika nishati ya makaa ya mawe, hata nchini Marekani, lakini kiunzi kimewekwa katika njia ya mchakato wa kuhamia katika matumizi ya nishati rafiki kwa mazingira.

Kansela Angela Merkel alitoka katika mkutano wa kilele wa G7 akizungumzia ''Ulaya kujitwisha majukumu ya mustakabali wake'', kwa kuwa haiwezekani tena kuitegemea Marekani. Hatua za utunzaji wa mazingira sasa zinaweza kutekelezwa haraka, kwa ushirikiano na Ufaransa ndani ya Umoja wa Ulaya, na pia Uingereza kwa sababu pande hizo zina maoni sawa. Na kisha kwenda Afrika na Asia, na kutoa utaalamu katika miradi ya kutunza mazingira. Hali kadhalika, sio vyema kupoteza mawasiliano na miji na majimbo nchini Marekani.

Haina maana tena kwa Donald Trump kuzungumzia suala la mazingira. Ataiumiza nchi yake, lakini juhudi za kimataifa za kuyatunza mazingira, zitaendelea.

Mwandishi: Jens Thurau
Tafsiri: Daniel Gakuba
Mhariri: Mohammed Khelef

 

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com