1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maoni: Hakuna suluhisho la haraka la wakimbizi

Bernd Riegert/Mohammed Khelef7 Machi 2016

Mgawanyo wa wakimbizi na wahamiaji ndani ya Umoja wa Ulaya unaonekana kutofanya kazi na badala yake Umoja huo unategemea zaidi kwenye hoja ya kufunga mipaka yake, anaandika Bernd Riegert.

https://p.dw.com/p/1I8LR
Sanamu la "Hatua Moja" mjini Brussels, Ubelgiji.
Sanamu la "Hatua Moja" mjini Brussels, Ubelgiji.Picha: DW/B. Riegert

Kansela Angela Merkel wa Ujerumani alianzisha mageuzi kwenye sera ya wakimbizi kitambo kidogo. Mageuzi hayo yamefanyika kwenye mkururo wa hatua ndogo ndogo, yumkini kwa wakati muafaka ili kuepuka balaa kwenye chaguzi za majimbo matatu Jumapili ijayo.

Wakimbizi na wahamiaji ambao Kansela Merkel aliwaalika kwa mara ya kwanza majira ya mapukutiko yaliyopita, akisema kusingelikuwa na ukomo wa idadi, sasa wanatakiwa wabakie nchini Ugiriki – ama kwa usahihi zaidi, nchini Uturuki.

Kuna nafasi ya kutosha Ugiriki, ndivyo asemavyo sasa Kansela huyo, na hakuna haja ya kubahatisha maisha kwa kuvuka bahari ya Aegean.

Mpaka kati ya Ugiriki na Macedonia takribani umeshafungwa rasmi, kama alivyosema Rais wa Baraza la Ulaya, Donald Tusk: “Tunaifunga njia ya Balkan", akiizungumzia hatua hiyo baada ya kukutana na Kansela Merkel.

Mwandishi wa DW kwa masuala ya Ulaya, Bernd Riegert.
Mwandishi wa DW kwa masuala ya Ulaya, Bernd Riegert.

Haraka haraka Tusk akaiambatanisha kauli hiyo na ombi lake kwa wakimbizi kuwataka wabakie makwao. Ile hatua ya kupunguza wakimbizi iliyotabiriwa na Kansela Merkel na ikangojewa kwa muda mrefu, sasa inatekelezwa. Austria na mataifa ya Balkan yamelifanya hilo liwezekane kwa kuwekwa ukomo, bila kuizingatia Ugiriki.

Kansela Merkel hawezi kuwa hakufurahishwa sana na hili, licha ya kuwa bado anaendelea kusema ni uamuzi wa upande mmoja. Anakataa kukubali kuwepo kwa ukomo kwa nchi yake, kwa kuwa kauli hiyo inachukiza kisiasa, naye asingelipenda kuaibika.

Lakini kivitendo tayari ukomo umeshawekwa na unatekeleza, kwa sababu serikali kuu mjini Berlin nayo pia inakataa kutafuta njia ya kuwasaidia wakimbizi walioko kwenye mataifa ya Balkan na kuwaleta wakimbizi Ujerumani.

Sera ya kuwahamisha watu sasa imegeuka kuwa sera ya kuwafukuza. Wakimbizi na wahamiaji watasukumwa nje ya mipaka ya Ulaya. Na huko ni kugeuka nyuma.

Katika majira ya mapukutiko ya mwaka jana, Angela Merkel na Rais Francoise Hollande wa Ufaransa walitangaza kwamba kanuni za kuomba hifadhi za Umoja wa Ulaya zimepitwa na wakati kwa sababu sheria hizo zilizotungwa mjini Dublin miaka kadhaa iliyopita hazifanyi tena kazi.

Sasa kanuni itafanya kazi tena, ambapo nchi ambayo mhamiaji aliingia kwa mara ya kwanza itakuwa na jukumu la kushughulikia maombi yake ya hifadhi.

Kigeugeu kinatendeka, na Ugiriki na Italia sasa zitalazimika kuratibu, kuwarejesha au kuwakatalia wakimbizi wote wanaotua mguu kwenye fukwe zao. Na kuizuia isizame kwenye machafuko, Ugiriki itaanza tena kupokea msaada wa kifedha na kitaasisi kutoka Umoja wa Ulaya.

Mwandishi: Bernd Riegert
Tafsiri: Mohammed Khelef
Mhariri: Iddi Ssessanga