1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maoni: EU laazima iepuke majaribu

Andreas Noll24 Februari 2014

Kwa miaka kadha Umoja wa Ulaya umejaribu kuisogeza karibu Ukraine, lakini Viktor Yanukovych alikuwa akisita. Lakini sasa karata zimebadilika, na umoja huo unapaswa kucheza kwa tahadhari, anasema Christoph Hasselbach.

https://p.dw.com/p/1BELS
Christoph Hasselbach, mkuu wa ofisi ya DW mjini Brussels.
Christoph Hasselbach, mkuu wa ofisi ya DW mjini Brussels.Picha: DW/P. Henriksen

Hakuna alietarajia mambo kubadilika kwa haraka namna hiyo, na hasa Umoja wa Ulaya. Siku ya Ijumaa mawaziri wa mambo ya kigeni ya Ujerumani, Poland na Ufaransa walifanikiwa kumshawishi rais wa Ukraine ambaye hivi sasa amepinduliwa, Viktor Yanukovych, kukubaliana na mageuzi kadhaa, wakati wenzao mjini Brussels walikuwa wakiidhinisha vikwazo.

Siku moja baadaye, Yanukovych hakuwa anaonekana tena katika uwanja wa siasa na bunge lilitangaza kumvua madaraka yake. Yulia Tymoshenko, kiongozi wa upinzani ambaye nchi za magharibi zilimpigania sana akiwa jela, alikuwa huru. Bunge la Ukraine limetangaza kufanyika kwa uchaguzi mkuu mwishoni mwa mwezi Mei. Njia ya Ukraine kuelekea katika demokrasia, na kukaribiana na Umoja wa Ulaya imekuwa wazi tena.

Pamoja na hisia hizo za ushindi, Umoja wa Ulaya unapaswa kujihadhari na majaribio kadhaa. Umoja huo unapaswa kuepuka kwa njia yoyote ile, kuegemea upande mmoja wa kisiasa. Yanukovych na wafuasi wake, na pia rais Urusi Vladmir Putin wamekuwa wakisema umoja huo unaegemea upande, na wana sababu za msingi. Tymoshenko na bingwa wa zamani wa ndondi aliegeuka mwanasiasa Vitali Klitschko ndiyo vipenzi vya Umoja wa Ulaya, lakini chama cha Yanukovych na wafuasi wake lazima wawe na jukumu la kisiasa huko mbeleni, vinginevyo taifa hilo halitakuwa na utulivu.

Kwa wakati huu Umoja wa ulaya haupaswi kutia chumvi jukumu lake nchini Ukraine, kwa sababu uko huko kuisindikiza nchi hiyo kisiasa na si kuielekeza nini inapaswa kufanya. Dhana za mataifa ya Ujerumani, Ufaransa au Sweden kuhusu demokrasia haziwezi kutumika moja kwa moja. Ukraine inapaswa kutafuta njia yake yenyewe.

Pengine cha muhimu zaidi ni kwamba Umoja wa Ulaya unapaswa kuendeleza majadiliano na utawala mjini Moscow. Kosa kubwa zaidi lingekuwa kwa Brussels kupuuza maslahi ya Urusi na kuigeuza Ukraine kama taifa la kupunguza nguvu ya Urusi. Hilo halitaigawa tu Ukraine, lakini pia linaweza kusababisha mgogoro mkubwa na Urusi ambao unaweza kuwa na madhara makubwa sana.

Yeyote atakayechukuwa madaraka nchini Ukraine baadaye, atakuwa na kazi kubwa ya kushughulikia matatizo ya kifedha na kiuchumi, ambayo yanaweza kuharibu hatua zozote zilizopigwa kuelekea demokrasia. Kwa hivyo Umoja wa Ulaya unapaswa kuongeza msaada zaidi kwa Ukraine kuliko sasa. Bila shaka msaada huo haupaswi kuwa bila masharti, na usiwe na lengo la kushindana na Urusi, lakini ahadi zote zinazotolewa hadi sasa zinaonekana kuwa ndogo sana.

Lazima tukumbuke kuwa fursa ya kuivutia nchi hii kubwa na muhimu upande wa magharibi inaweza isije haraka. Huu siyo wakati wa kuwa wachoyo. Na hatua nyingine ambayo inaweza kuuweka Umoja wa Ulaya katika nafasi nzuri ni kuwarushusu raia wa Ukraine kusafiri. Wanapaswa kupewa matumaini ya kusafiri barani Ulaya bila kuhitaji viza.

Nchini Urusi, na hata katika nchi za magharibi kunazungumziwa mapambano ya eneo la kimkakati yanayoendelea nchini Ukraine. Watu hawa wanapaswa kufikiria upya. Ukraine haitaki kuwa kitu cha kushindaniwa. Ikiwa raia wake wangeweza kuchagua kwa uhuru zaidi, wasingependa kujifunga kwa ama Urusi au Umoja wa Ulaya. Na hawapaswi kufanya hivyo. Ikiwa Ukraine inataka kuwa daraja kati ya mashariki na magharibi, basi watu wake wakaribishwe katika maeneo yote.

Itakuwa vigumu kumshawishi Putin juu ya hili kwa sababu anaonekana bado amenasa katika mtego wa vita baridi, lakini ukweli ni kwamba Ukraine tulivu na yenye ushirikiano wa kiuchumi na pande zote iko katika maslahi ya Urusi. Na hapa lazima isemwe kwamba wasiwasi wa Putin unaweza kuwa unatokana na hofu yake kuwa cheche hizo za demokrasia zinaweza kufika nyumbani kwake. Lakini hilo siyo tatizo la Umoja wa Ulaya.

Mwandishi: Christoph Hasselbach
Tafsiri: Iddi Ismail Ssessanga
Mhariri: Daniel Gakuba