1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maoni: Erdogan anapambana kubaki madarakani

Bruce Amani
25 Oktoba 2021

Rais wa Uturuki Recep Erdogan anataka kuwafukuza nchini mabalozi 10 kuhusiana na mwanaharakati Osman Kavala. Katika kufanya hivyo, kwa mara nyingine anajaribu kuyafunika matatizo ya ndani ya nchi, anasema Erkan Arikan

https://p.dw.com/p/428Fd
Türkei Recep Tayyip Erdogan in Eskisehir
Picha: Murat Cetinmuhurdar/Turkish Presidency/AA/picture alliance

Kila mara kuna tatizo jipya kwenye uchumi wa Uturuki – hakika kila mara Uturuki inakuwa kwenye vichwa vya habari kwa sababu yoyote ile – haichukui muda mrefu kabla ya Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan kuibuka na jibu lisiloeleweka kabisa.

Jumamosi, Erdogan alitangaza kuwa ameiagiza Wizara ya Mambo ya Kigeni kuwatangaza mabalozi 10 kuwa "wasiohitajika nchini humo”, hatua ya kwanza kabla ya kufukuzwa, baada ya kutoa wito wa kuwachiliwa huru mwanahisani na mwanaharakati Osman Kavala.

Ni wazi kuwa Erdogan hapendi tu kuanzisha mzozo na nchi za Magharibi, lakini pia anauhitaji. Baada ya yote, ni vipi anaweza kuwachokoza washirika wake muhimu Zaidi wa NATO, Marekani, Ufaransa, na juu ya yote, Ujerumani? Na hili, ni chini ya wiki moja baada ya Angela Merkel kufanya ziara yake ya mwisho mjini Istanbul kama Kansela wakati viongozi hao wawili walisifu ushirikiano wa Ujerumani na Uturuki. Sifa hiyo inaonekana kuwa ilikuwa yam domo tu, angalau kwa upande wa Erdogan.

Nchi za magharibi kawaida kulaumiwa

Erkan Arikan ni mkuu wa idhaa ya Kituruki ya DW
Erkan Arikan ni mkuu wa idhaa ya Kituruki ya DWPicha: DW/B. Scheid

Rais wa Uturuki kwa mara nyingine anatumia mbinu aliyoijaribisha na inayofanya kazi kuepusha lawama kwa matatizo yanayomkabili. Uchunguzi wa karibuni unaonesha kuwa chama cha Erdogan cha AKP kimepoteza uungaji mkono, huku chini ya asilimia 30 wakisema watamuunga mkono katika uchaguzi. Erdogan alijibu habari hii mbaya kwa kutoa matusi yaliyoelekekezwa kwa vyama vya upinzani.

Kisha Alhamisi, Shirika la Kimataifa la Kupambana na Utakatishaji Fedha lenye makao yake mjini Paris la Financial Action Task Force – FATF likatangaza kuwa linaiweka rasmi Uturuki kwenye orodha mbaya kwa kushindwa kupambana na utakatishaji fedha na ufadhili wa ugaidi. Hatua hiyo ilisababisha kuyumba kiasi kwa soko la hisa la Istanbul.

Kiongozi wa kibabe katika hali ngumu

Hii sio mara ya kwanza kwa Erdogan kuzishambulia nchi za Magharibi. Lakini mara hii amekwenda mbali sana. Baada ya Kavala kufungwa jela kwa mashitaka hafifu mwaka wa 2017, alituhumiwa kwa kuunga mkono maandamano ya bustani ya Gezi ambayo yalichochea maandamano ya kitaifa mwaka wa 2013.

Alifutiwa mashitaka haya na mahakama moja, lakini saa chache baadaye mahakama nyingine ikamhukumu kwa kuwa kiongozi wa jaribio la mapinduzi ya mwaka wa 2016. Ni wazi kuwa tuhuma hizi hazina msingi. Mahakama ya Ulaya ya Haki za Binaadamu pia ilitoa uamuzi kuwa hakuna misingi ya kuendelea kumzuilia Kavala, na ikataka aachiwe huru maramoja. Erdogan alikataa uamuzi huo, na ndio maana mahakama ya Uturuki pia ilibaki na uwamuzi wake – ikidhibitisha kwa mara nyingine tena kuwa mahakama za Uturuki zinatoa tu maamuzi kulingana na maagizo ya rais.

Ukosefu wa ajira, wakimbizi wanaoishi Uturuki wanaonekana kuwa kitisho – na rais anayeonekana wazi kuwa katika hali mbaya kiafaya haonekani tena kama shujaa. Kama vyama vya upinzani vitaendelea kuwa na umoja hadi uchaguzi ujao wa rais mwaka 2023, Erdogan atakuwa na wakati mgumu sana kuchaguliwa tena. Kama, hata hivyo, upinzani utagawika, hilo litamfaidi Erdogan. Vyovyote itakavyokuwa katika siku za usoni, kwa sasa Erdogan bado ana ana kazi nyingi ya kujaribu kuwakasirisha hata Zaidi washirika wa Magharibi

Maoni haya yalitafsiriwa kutoka kwa Kijerumani

Mwandishi: Bruce Amani