Maoni: Demokrasia Afrika ni hadithi | Matukio ya Afrika | DW | 16.06.2015
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Afrika

Maoni: Demokrasia Afrika ni hadithi

ICC ilitaka rais al-Bashir wa Sudan akamatwe kwa kuhusika na mauaji ya kimbari. Mwandishi wa DW Ludger Schadomsky anasema Bashir kuruhusiwa kuondoka Afrika Kusini bila kutiwa nguvuni ni aibu.

Julai 16 mwaka 2013 kulikuwa na taarifa kama hizi tunazozisikia sasa: Omar al-Bashir atoroka mkutano mkuu wa Umoja wa Afrika. Miaka miwili iliyopita, rais huyo wa Sudan, anayesakwa na ICC, alikimbia kitisho cha kukamatwa na vyombo vya sheria nchini Nigeria ambapo mkutano ulikuwa unafanyika. Wakati huo, Afrika Kusini iliapa kumkata Bashir iwapo atakanyaga ardhi ya nchi hiyo.

Bashir juzi akathubutu kwenda Afrika Kusini kuhudhuria mkutano wa kilele mjini Johannesburg. Na bila kujali amri ya mahakama ya kukamatwa kwake, akapanda ndege kwenye kambi moja ya jeshi na kurudi kwenye mji mkuu wa nchi yake Sudan, Khartoum.

Haishangazi kuona Bashir akiupima mshikamano wa nchi za Kiafrika. Wala si jambo la ajabu kwa serikali ya Afrika Kusini, kinyume na ahadi zake, kumruhusu aondoke bila kukamatwa. Waziri wa mambo ya nje wa Afrika Kusini aliwahahakikishia viongozi wote watakaohudhuria mkutano mkuu, haki ya kutokamatwa. Kwa hatua hiyo, Afrika Kusini imeipa demokrasia kisogo.

Afrika yaelekea pabaya

Mwandishi wa DW, Ludger Schadomsky

Mwandishi wa DW, Ludger Schadomsky

Kisa cha Bashir kinabeba ujumbe wa hatari: Nigeria na Afrika Kusini, ambazo ndizo nchi zenye nguvu kubwa ya kiuchumi barani Afrika, zinapingana na mahakama ya kimataifa ya uhalifu, tena inayoongozwa na Mwafrika mwenzao.

Matamshi kwamba Afrika ni bara linaloinukia, tena linaloshuhudia ukuaji wa kasi wa kiuchumi na kuongezeka kwa demokrasia, yatabaki kuwa hadithi. Uchumi haukui kama ilivyotabiriwa. Pamoja na hayo, migogoro iliyotapakaa kuanzia Mali hadi Somalia inatoa picha ya kusikitisha ya bara hili. Na kama huko Nigeria jenerali aliyeongoza mapinduzi ya serikali sasa amechaguliwa kuwa rais basi ni dhahiri bara hili linapoelekea.

Tabia ya kung'ang'ania madaraka pia bado ni tatizo sugu. Marais wa Burundi, Rwanda na Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo wote wametibua hasira za wananchi wao kwa kutaka kuongoza muhula wa tatu, wakati katiba zao zinaruhusu mihula miwili tu. Rais mkongwe wa Zimbabwe, Robert Mugabe, ambaye mwenyewe yuko madarakani kwa kipindi cha saba sasa, ndiye aliyesimama na kuwashauri viongozi wenzake waheshimu matakwa ya raia na kuachia madaraka baada ya vipindi viwili. Hii inaonyesha wazi jinsi Afrika ilivyo katika hali mbaya.

Mwandishi: Ludger schadomsky

Tafsiri: Elizabeth Shoo

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman