1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Bernie Sanders kubwaga manyanga .

Miodrag Soric/Sylvia Mwehozi10 Juni 2016

Wanachama wa chama cha Democrat nchini Marekani wanaanza kuwa na nguvu ya pamoja na huenda kumesalia muda kidogo kabla ya Bernie Sanders hajabwaga manyanga katika mbio za kuwania uteuzi wa chama hicho.

https://p.dw.com/p/1J4MT
USA Hillary Clinton und Barack Obama PK in Chicago
Picha: Getty Images/AFP/J. Watson

Wanachama wa chama cha Democrat nchini Marekani wanaanza kuwa na nguvu ya pamoja na huenda kumesalia muda kidogo kabla ya Bernie Sanders hajabwaga manyanga katika mbio za kuwania uteuzi wa chama hicho. Hii inaweza kumsaidia Hillary Clinton kucheza karata zake vizuri na kuwavuta wafuasi waliokuwa wakimuunga mkono Sanders.

Chama cha cha Democrat kinaonyesha heshima. Bernie Sanders amekaribishwa ikulu na Raisa Barack Obama na Hillary Clinton amekuwa akitoa kauli nzuri dhidi ya mpinzani wake kwa sasa.

"Bernie" kama ambavyo anajulikana na wengi, ataingia ulingoni kutupa karata zake za mwisho hapo Jumanne,katika kura za mchujo jijini Washington. Hata kama atashinda katika jiji hilo kuu la nchini Marekani,haitaweza kubadili hesabu.

Hillary Clinton ameshinda uteuzi wa Democrat. Hilo ndilo linaweza kuwa hitimisho baada ya Rais Obama kumuunga mkono wazi wazi.

Obama alichukua muda mrefu kufanya hivyo, na akaonyesha msimamo wa kati baina ya wagombea wote wa Democrat, na hii ni mbinu ambayo Sanders mwenyewe na wafuasi wake wameiheshimu.

Clinton si mzungumzaji mzuri

Kwa sasa Obama anasubiri kuwepo katika kampeni za uchaguzi, kwa sababu anajua uwezo wake kwa maana ya udhaifu na nguvu aliyonayo Clinton kuliko mtu yeyote.

Clinton si mzungumzaji mzuri katika hadhara, tofauti na Obama ambaye ni tajiri wa maneneo na mzungumzaji mwenye kipaji.

Kiwango cha uaminifu na umaarufu wa Clinton kwa sasa si kikubwa sana, ingawa anafaidika na msaada mkubwa wa Rais Obama.

Mwandishi wa DW Miodrag Soric nchini Marekani
Mwandishi wa DW Miodrag Soric nchini Marekani

Obama anaweza kutumia nafasi hiyo kama mtaji wa kisiasa hadi siku ya kupiga kura. Hakika hatafanya hivyo pasipo kujinufaisha mwenyewe. Anataka kuimarisha urithi wake wa kisiasa.

"Ikiwa Donald Trump atakuwa rais, atataka kurudisha nyuma mageuzi ya afya, kupinga makubaliano ya soko huria na kupunguza jukumu la Marekani kama walinzi wa kimataifa", ndiyo kampeni kubwa dhidi ya bilionea Trump, mgombea mtarajiwa wa Republican, inavyokwenda.

Kwa mujibu wa Democrat, mambo hayo hayawezi kutokea na lazima Trump azuiwe kuwa rais. Obama, Clinton na Sanders wote wamekubaliana juu ya hili.

Ni suala la siku, pengine wiki kadhaa tu zilizosalia kabla ya wale wana-Democrat waliokuwa wakimpinga Clinton kuanza sasa kuunga mkono kampeni zake.

Kujiondoa kwa Sanders katika mbio hizo kutatokea tu kulingana na muda. Seneta huyo wa Vermont atapaswa kuheshimu mamilioni ya wafuasi wake. Wengi wameonyesha mapenzi ya kweli na bado wanayo licha ya kwamba mgombea wao hajaweza kupita.

Lakini kitu muhimu ambacho watakifurahia zaidi wafuasi hao, ni namna mgombea wao alivyomlazimisha Clinton kuchukua baadhi ya sera zake ikiwemo ile ya fedha zaidi kwa ajili ya elimu na afya, uwekezaji mkubwa wa mabilioni katika miundombinu, kodi kubwa kwa matajiri na nguvu ya udhibiti wa soko la hisa.

Clinton sasa atapaswa kuhama kidogo kutoka misimamo yake, ingawa yeye mwenyewe anajua kwamba kijadi uchaguzi wa Marekani unashindaniwa katikati ya wigo wa kisaisa. Japo ni hatari kubwa, lakini atapaswa kufanya hivyo, ikiwa anataka kuwavuta wafuasi wa Sanders.

Kama sivyo, inamaanisha chama chake cha Democrat hakitakuwa na nguvu kufikia mwishoni mwa uteuzi wa mgombea, na pengine kitapoteza uchaguzi mkuu wa Novemba kwa bilionea mwenye misimamo yenye utata, Donald Trump.

Mwandishi: Miodrag Soric/Sylvia Mwehozi/DW

Mhariri: Mohammed Khelef