Maoni: Aliyeshinda na aliyeshindwa Nigeria wote wabaya | Matukio ya Afrika | DW | 27.02.2019
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

NIGERIA

Maoni: Aliyeshinda na aliyeshindwa Nigeria wote wabaya

Licha ya Muhammadu Buhari kumshinda Atiku Abubakari kwenye uchaguzi, Thomas Mösch wa Idhaa ya Kihausa ya DW anasema aliyeshinda na aliyeshindwa wote ni wabaya na sasa wanachoweza kufanya ni kuitendea mema Nigeria.

Ushindi wa Muhammadu Buhari umekuwa mkubwa zaidi ya ilivyotazamiwa. Amemshinda mpinzani wake Atiku Abubakar kwa tafauti ya takribani kura milioni nne.

Kwenye uchaguzi wa mwisho, Buhari alimshinda aliyekuwa rais wa wakati huo, Goodluck Jonathan, kwa kura zisizozidi milioni mbini unusu. Kwa kuangalia tafauti hii kubwa ya kura, ni shida kuelewa kwa nini Abubakar hataki kuyatambua matokeo haya.

Ni kweli kwamba kulikuwa na makosa makubwa ya kuandaa uchaguzi. Tume ya uchaguzi, INEC, haikufanya kazi ya kupongezwa. Haikuchukuwa fursa ya ucheleweshwaji kura kwa wiki nzima kujirekebisha.

Vituo vingi vilifunguliwa masaa kadhaa baada ya muda na vyengine hadi siku ya pili yake. Kuna baadhi ya maeneo, mashine za kura hazikusoma kabisa.

Moesch Thomas Kommentarbild App

Thomas Moesch wa Idhaa ya Kihausa ya DW

Kwenye maeneo kadhaa, hasa kwenye mji mkuu wa kiuchumi, Lagos, na maeneo ya kusini mashariki, makundi yenye silaha yaliwazuwia wapigakura kufika vituoni au hata kuvichoma moto kabisa vituo vyenyewe. 

Uchaguzi haukuwa mbaya sana

Lakini kwa upande mwengine, hakukuwa na ripoti nyingi za makosa mashuhuri kwenye chaguzi za huko, kama vile wapigakura wasiofikia umri au maboksi yaliyokwishapigwa kura kwenye vyumba vya wanasiasa.

Kwa hivyo, hakuna sababu ya kudhani kwamba makosa ambayo yamekuwa mashuhuri katika siku za karibuni ndiyo yaliyopelekea ushindi wa Buhari. Ni bahati mbaya kwamba Atiku Abubakar ameshindwa vibaya, lakini si zaidi ya hapo. Ameshindwa kwa kuwa alishindwa kuwashawishi vya kutosha Wanigeria.

Majimbo ambayo alikuwa anaongoza, takribani nusu ya majimbo yote 36, ni yale yaliyokuwa na idadi ndogo ya waliojitokeza kupiga kura. Na hata hivyo, mpinzani huyu amepata kura si haba na haya ni mafanikio ya kumfanya aheshimiwe: Ameweza kushinda jimbo lake la Adamawa na mengine kadhaa ya kusini magharibi, ambako miaka minne iliyopita yalimpa ushindi Buhari.

Si Buhari wala Abubakar aliyewavutia

Hii nayo inasema kuwa Muhammadu Buhari kumbe sio tena nyota inayong’aa kama alivyokuwa miaka minne iliyopita pale alipofanikiwa kumng’oa rais aliye madarakani. Kiwango kidogo kabisa cha waliojitokeza kupigakura zao, chini ya asilimia 36, kinaonesha kwamba si yeye wala Abubakar walioweza kuwavutia wapigakura wa Nigeria.

Hata hivyo, Buhari alifaidika kutokana na ukweli kwamba wafuasi wake upande wa kaskazini bado wanampenda na walijitokeza kwa wingi vituoni. Lakini wengi wao yawezekana ni wale waliojiondoa kwa Atiku Abubakar.

Kaskazini mwa nchi hiyo bado kuna kiwango kikubwa cha tafrani na sehemu kubwa inateseka na mauaji ya kila siku na umasikini unaoongezeka. 

Kipi anachoweza kukibadili ndani ya miaka minne ijayo, kwa kweli hakuna mwenye jawabu, lakini angalau wapigakura waliamuwa kwenda na zimwi liwajuwalo, ambalo yumkini halitawala likawesha.

Mwandishi: Thomas Mösch
Tafsiri: Mohammed Khelef
Mhariri: Yusuf Saumu