1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

"Mantiki rahisi hayatekelezwi"

Maja Dreyer12 Juni 2007

Ni masuala mawili ambayo leo hii yamezingatiwa hasa na wahariri wa humu nchini. Kwanza ni gharama za kijeshi kulingana na ripoti mpya iliyotolewa jana na shirika la Sweden linalochunguza amani duniani, SIPRI, na pili ni ubishi unaoendelea kati ya vyama vikubwa vilivyomo ndani ya serikali ya mseto ya Ujerumani.

https://p.dw.com/p/CHSj
Kifaru kinachotengezwa nchini Ujerumani
Kifaru kinachotengezwa nchini UjerumaniPicha: dpa

Kwanza ni gazeti la Thüringer Allgemeine juu ya matumizi ya kijeshi:

“Afadhali taasisi hii ya Sweden SIPRI ingechapisha ripoti yake hii kuhusu gharama za kijeshi wakati viongozi wa nchi nane tajiri wa kundi la G8 walipojadiliana juu ya fedha watakazozilipa kama msaada kwa bara la Afrika. Dola Billioni 25 ambazo zimependekezwa na nchi hizo haitakuwa tena ishara ya ukarimu tukilinganisha na Dola Billioni 707 ambazo nchi hizo nane tu zinazitumia kama gharama za kijeshi. Tena Dola Billioni 15 ambazo zinahitajika kufikia lengo la Millenia la kumuwezesha kila mtoto kwenda shuleni ni idadi ndogo ikilinganishwa na gharama za kijeshi. Hata hivyo, nchi tajiri zinataka kupewa muda hadi mwaka 2015 kufikia lengo hilo – kwa sababu fedha zinakosekana!”

Ni uchambuzi wa gazeti la “Thüringer Allgemeine”. Mhariri wa “Recklinghäuser Zeitung” analinganisha pia ghamara za kijeshi na umaskini katika sehemu kubwa ya dunia. Ameandika:

“Ripoti ya taasisi ya SIPRI inasema kuwa mwaka uliopita Euro Billioni 900 zimetumika kugharamia matumizi ya kijeshi, maana yake ni Euro 137 kwa kila mtu mmoja ulimwenguni. Lakini sehemu ndogo tu ya fedha hizo ingeweza kupunguza shida na kuondosha njaa duniani. Ingesaidia kuzuia watoto wengi kufa barani Afrika na kuupiga vita ukimwi na maradhi mengine. Lakini katika dunia hii, mantiki rahisi hayatekelezwi.”

Na hatimaye juu ya suala hilo, gazeti la “Wiesbadener Kurier” linaangalia jukumu la Ujerumani katika biashara ya silaha. Tunasoma:

“Nchi yetu sasa inachukua nafasi ya tatu kwenye orodha hii ya nchi zinazouza silaha nyingi duniani ikitanguliawa na Marekani na Urusi. Pia mauzo ya vifaa vya kijeshi yamezidi mara mbili katika muda wa mwaka mmoja. Serikali yetu basi inapaswa kubadilisha sura hii ili kujipatia uaminifu kuhusiana na sera zake za amani.”

Tukibakie basi nchini humu sasa ambapo kumezuka mabishano kati ya vyama vya Social Demokrats, SPD, na Christian Demokrats, CDU, vinavyounga serikali ya mseto hapa Ujerumani. Suali sasa ni muungano huu una mustakabali gani? Gazeti la “Nürnberger Nachrichten” linamkosoa Kansela Angela Merkel:

“Kwa upande mmoja, Bi Merkel anajionyesha kama kiongozi wa taifa anayeongoza mikutano ya kilele, kwa upande mwingine lakini kama kiongozi wa serikali ya muungano hatoi muelekeo. Badala yake anaangalia kutokea mbali na anasubiri kuchukua hatua. Pande zote mbili za serikali hiyo lakini hazipaswi kutochukua hatua yoyote na kuanza kampeni ya uchaguzi mapema mno.”

Anayekosolewa hasa lakini kwa kuanzisha mvutano huu ni mwenyekiti wa SPD, Bw. Kurt Beck. Hivi karibuni, Kurt Beck aliikosoa sera ya kiliberali ya chama cha CDU. Onyo la gazeti la “Kölner Stadt-Anzeiger” ni lifuatalo:

“Mwanasiasa huyu anazungumza kama yu upande wa upinzani. Ikiwa ataendelea hivyo, basi chama chake cha SPD hatimaye kitafika kule kule yaani upande wa upinzani.”