1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maneno makali bungeni:Merkel anaufuata mkondo wa sawa?

16 Septemba 2010

Viongozi wa Ujerumani wamerushiana maneno makali bungeni wakati wa mjadala wa bajeti ya mwaka ujao.

https://p.dw.com/p/PDZ1
Kansela Merkel akijitetea bungeniPicha: AP

Kansela wa Ujerumani, Angela Merkel, na kiongozi wa chama cha upinzani cha Social Democratic, SPD, Sigmar Gabriel,walirushiana maneno makali bungeni. Kwa upande wake, Bibi Merkel aliipongeza serikali yake kwa kufanikiwa kujinyanyua hata baada ya kusukwasukwa na mtikisiko wa kiuchumi uliougubika ulimwengu mzima miaka miwili iliyopita. Kwa upande wa pili, chama cha upinzani cha SPD hakijaona mafanikio yoyote, na badala yake kimesema Wajerumani hawana imani tena na wanasiasia wake.

Hawajui wanachokifanya

Akiufungua mjadala huo mkali bungeni hapo jana, Kiongozi wa chama cha upinzani cha Kisoshalisti, SPD, Siegmar Gabriel, hakuwa na kauli zozote nzuri kwa wanasiasa hao. Kiongozi huyo aliikosoa serikali ya Ujerumani na kusisitiza kuwa kuna hali ngumu ya kisiasa. Kwa mtazamo wake, Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani, Guido Westerwelle, kamwe hajafanikiwa kuandaa mkakati maradufu. Uongozi umeshindwa kuibadili sura ya Ujerumani katika ulimwengu.

Hata hivyo, Kansela Merkel alimlaumu Siegmar Gabriel kwa kujikita zaidi katika malumbano ya kisiasa badala ya kuyapongeza mazuri yaliyopo. Kansela Merkel amefanikiwa kuyashughulikia masuala ya kodi, afya, kadhalika nishati, jambo analolipinga kiongozi wa SPD Siegmar Gabriel,"Hawafahamu chochote kilicho na manufaa kwa Ujerumani. Hali hii haijawahi kushuhudiwa, kwamba serikali yoyote ile inayaunga mkono zaidi mashirika makubwa,"alieleza.

Mamilionea wameongezeka

Wakati huohuo, kiongozi wa chama cha mrengo wa Shoto bungeni, Die Linke, Gregor Gysi, ana mtazamo huohuo. Kwa mujibu wa mwanasiasa huyo wa mrengo wa shoto, Bibi Merkel si kansela wa wanyonge ambao ni wafanyakazi wa kawaida, watu waliostaafu au wapokeaji wa msaada wa kijamii. Angela Merkel ni kansela wa wanaharakati ambao wanayatetea maslahi yao hasa katika sekta za makampuni ya kutengeneza madawa, nishati na huduma za usalama. Aliendelea kueleza kuwa mzigo mkubwa uliosababishwa na mtikisiko wa kiuchumi umewaangukia zaidi wafanyakazi wanaopata mshahara wa kima cha chini na wasiokuwa na ajira kabisa. Kwa sababu hiyo serikali inaweza kujihifadhia fedha badala ya mabenki ambayo hayakuwajibika.

Kadhalika matajiri wa Ujerumani hawalazimiki kuchangia pakubwa ili kuupunguza mzigo uliosababishwa na athari za mtikisiko wa kiuchumi,badala yake,''Idadi ya matajiri walio na mamilioni ya fedha imeongezeka kwa alfu 51 tangu mwaka uliopita. Kamwe hawalazimiki kulipa hata senti moja ili kuchangia kulimaliza tatizo hilo ijapokuwa ni matajiri wa kupindukia. Kwa kweli hilo halieleweki,"alilalamika.

Nishati na ajira

Matamshi hayo makali yamemlazimu Kansela Merkel kujitathmini upya. Serikali yake imejipongeza kwa kuweza kuunyanyua uchumi wa Ujerumani, vilevile kuipunguza idadi ya watu wasiokuwa na ajira hata baada ya kusukwasukwa na mtikisiko wa kiuchumi na akakumbusha kuwa,''Kuna umuhimu wa kuitathmini hali ilivyokuwa na ya sasa. Tangu nilipoushika wadhifa wa Kansela wa Ujurumani kwa kipindi cha miaka mitano iliyopita, tumefanikiwa kuipunguza idadi ya watu wasiokuwa na ajira kwa kiasi ya milioni 3. Uongozi uliopita haukuweza kulitimiza hilo. Hayo ndiyo mafanikio ya utekelezaji si tu wa majukumu yetu, bali pia wa muungano wa vyama vya kikristo na kiliberali."

Suala la msingi ambalo lilizua mitazamo tofauti bungeni ni mjadala kuhusu nishati. Wanasiasa wa upinzani wanaukosoa uamuzi wa serikali wa kuuongeza muda wa vinu vya nuklia kufanya kazi. Vinu hivyo vitaendelea kutengeza nishati kwa kipindi cha miaka 12 ijayo.

Mwandishi:Mwadzaya,Thelma-ZPR-Marx,Bettina

Mhariri: Miraji Othman