1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mandela bado yuko mahtuti

Admin.WagnerD25 Juni 2013

Nelson Mandela amekaa kwa siku ya pili hospitalini akiwa mahututi, huku hofu ikizidi kuwa shujaa huyo wa mapambano dhidi ya utawala wa ubaguzi wa rangu huenda akapoteza mapambano yake ya mwisho.

https://p.dw.com/p/18vWY
Mandela get well soon.
Mandela get well soon.Picha: Reuters

Licha ya jitihada za kila aina kutoka kwa madaktari katika hospitali ya Mediclinic ya mjini Pretoria, hali ya mpambanaji huyo mwenye umri wa miaka 94 imeendelea kudorora katika siku za hivi karibuni. Raia wa Afrika Kusini wamekuwa wanapita karibu na nyumba ya Mandela mjini Johannesburg na kusema wanamuombea, baada ya rais Jacob Zuma kutoa wito kwa taifa hilo kumuombea Mandela ambae alimuita baba wa demokrasia.

Kansela wa Ujerumani, Angela Merkel alipomtembelea Mandela mjini Johannesburg, 6.10.2007
Kansela wa Ujerumani, Angela Merkel alipomtembelea Mandela mjini Johannesburg, 6.10.2007Picha: Axel Sschmidt/AFP/Getty Images

Siku ya Jumatatu, rais Zuma aliuambia umma uliokuwa na shauku kubwa katika hotuba iliyotangazwa moja kwa moja kupitia Televisheni, kuwa Mandela anaendela kuwa katika hali mbaya sana hospitalini, na kuongeza kuwa madaktari walikuwa wanafanya kila liwezekanalo kuhakikisha ustawi wake. Mke wake wa zamani Winnie Mandela, ambae pia alitoa mchango mkubwa katika mapambano dhidi ya ubaguzi wa rangi, mabinti zake Zindzi Mandela-Motlhajwa na Zenani Mandela-Dlamini, na maafisa kadhaa wa serikali walikwenda hosptiali jana Jumatatu kumjulia hali.

Hofu yazidi kutanda

Ziara hizi za jamaa zake Mandela, licha ya kuwa za kawaida tangu alipolazwa siku 18 zilizopita, zinakuja huku kukiwa na hofu zaidi kuhusu hali ya afya yake. Binti yake mkubwa Makaziwe amesema baba yake yuko katika amani na nafsi yake, huku akilalamika juu ya kile alichokiita wazimu wa vyomba vya habari kuhusu hali ya baba yake. Gazeti la Sowetan la mjini Johannesburg, limeripoti leo kuwa wanafamilia wameitisha kikao cha dharura kijijini kwao kujadili matatizo ya kiafya ya Mandela.

Rais wa Afrika Kusini Jacob Zuma.
Rais wa Afrika Kusini Jacob Zuma.Picha: Reuters

Ujumbe wa kumtakia ahueni Mandela umetoka pia ng'ambo. Mjini Washington, ikulu ya Marekani ilisema inamuombea Mandela. Rais wa Marekani Barack Obama kesho Jumatano anaanza ziara yake ya bara la Afrika, itakayomfikisha nchini Afrika Kusini, Senegal na Tanzania. White House ilisema inafuatilia hali ya afya ya Mandela, na haijasema iwapo kuzidi kudorora kwa afya hiyo kutaathiri ziara hiyo. Mandela atatimiza miaka 95 ya kuzaliwa Julai 18.

Mwandishi: Iddi Ismail Ssessanga/ape,afpe
Mhariri: Saum Yusuf