1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Manchester City yaendelea kutamba

Bruce Amani
6 Novemba 2017

Manchester City wanajidai kileleni mwa Premier League na pengo la pointi nane baada ya nambari mbili Manchester United kupewa kichapo cha moja bila ugenini dhidi ya mabingwa Chelsea siku ya Jumapili.

https://p.dw.com/p/2n6uK
Fußball England Manchester City v Liverpool Premier League Etihad Stadium Manchester City s Leroy Sane celebrate
Picha: Imago/PA Images/N. French

Kichapo hicho kilikuja saa chache tu baada ya viongozi wa ligi City kuwachabanga Arsenal tatu moja. Ushindi wa Chelsea kupitia bao safi la kichwa la Alvaro Morata, umewaacha katika nafasi ya nne, pointi tisa nyuma ya City. Ni ushindi uliohitajika sana kwa Chelsea na kocha wao anayekabiliwa na shinikizo Antonio Conte kufuatia kichapo cha katikati ya wiki katika Champions League dhidi ya Roma nchini Italia. Huyu hapa Conte "Kuonyesha mchezo wa aina hii na kuona ari ya timu kwa kweli nafurahi. Nnafurahi sana kuhusu hilo. Ni kitu kizuri kwangu, kizuri kwa wachezaji, kizuri kwa klabu. Lakini pia ni kizuri kwa mashabiki wetu kufurahia ujasiri huu na shauku ya wachezaji".

Mwenzake Mourinho alionekana kuwa mwenye kujiamini licha ya kichapo hicho, wakati Manchester City wakiendelea kuwaangamiza wapinzani kila wiki "Tuna wasiwasi lakini, kuna timu 17 zenye wasiwasi zaidi kuliko sisi. Kuna timu 18 zenye wasiwasi zaidi kuliko sisi kwa sababu tuko katika nafasi ya pili. Hivyo pointi nane kwenye premier league sio sawa na pointi nane katika ligi ya Ureno, La Liga, Bundesliga, sio sawa. pointi nane katika Premier League zina maana kuna mechi nyingi za kuchezwa".

Kwingineko, Tottenham Hotspur, ilipata ushindi wa moja bila dhidi ya washika mkia Crystal Palace na kujiimarisha katika nafasi ya tatu kwenye ligi japo ina pointi 23 sawa na MANCHESTER United. Liverpool wanafunga ukurasa wa tano bora na pointi 19 baada ya kuirarua West Ham mabao manne kwa moja

Fussball UEFA Champions League - Tottenham vs Real Madrid - Trainer Zinedine Zidane
Kocha Zinedine Zidane anakabiliwa na shinikizoPicha: Getty Images/AFP/IKimages/I. Kington

Real Madrid waibuka na ushindi

Nchini Uhispania, Real Madrid imeyatuliza mazungumzo ya kuwepo mgogoro baada ya kushindwa mechi mbili mfululizo. Hii ni baada ya Los Blancos kupata ushindi wa tatu bila dhidi ya Las Palmas katika uwanja wa Santiago Bernabeu. Ni matokeo yaliyompa ahueni kocha Zinedine Zidane "Ndiyo, naada ya kilichotokea katika mechi mbili zilizopita, ilikuwa muhimu kushinda. Tulifunga mabao matatu na hatukufungwa bao hivyo ushindi huo ulikuwa muhimu. Ni kitu tulichohitaji".

Ushindi huo unapunguza kwa pointi nane pengo kati yao na Barcelona kileleni mwa ligi. Lakini ulikuwa usiku mwingine mgumu kwa washambuliaji wa Madrid wakati Cristiano Ronaldo na Karim Benzema walishindwa kutikisa nyavu na badala yake kazi hiyo ikafanywa na Casemiro, Isco na Marco Asensio. Zidane alimtetea CR7 akisema kuwa myota huyo mreno yuko sawa kabisa

"sote tunajua kuwa Cristiano anapenda kufunga magoli, hilo ni wazi. Hufurahi sana anapofunga magoli, hilo ni kweli, lakini mimi, yeye, kila mtu anafahamu kuwa yeye huwa muhimu. Kwa sasa hafungi magoli katika La Liga lakini anafanya mambo mengine vile vile. Anaisaidia sana timu. Cristiano kawaida huwa mtu anayeleta tofauti uwanjani.

Barcelona waliwazaba Sevilla mbili moja na kujiimarisha kileleni na pointi 31, mbele ya Valencia ambao wana pointi 27 wakifuatwa na Real Madrid na Atletico Madrid ambao wote wana pointi 23.

Mwandishi: Bruce Amani/AFP/DPA
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman