1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mamilioni wakabiliwa na njaa duniani

Saumu Mwasimba
5 Mei 2021

Takriban watu milioni 155 wakabiliwa na njaa mnamo mwaka uliopita,2020 ikiwa ni ongezeko la watu milioni 20 ikilinganishwa na 2019,migogoro ya vita na kiuchumi ni miongoni mwa sababu zilizochangia

https://p.dw.com/p/3t0FL
eco@africa Mali erneuerbare Energien
Picha: DW

Idadi ya watu wanaokabiliwa na ukosefu mkubwa wa chakula duniani imepindukia kiwango kilichoshuhudiwa miaka mitano iliyopita. Ripoti ya Umoja wa Mataifa inasema watu wasiopungua milioni 155 walitumbukia kwenye ukosefu wa chakula mwaka 2020.

Shirika la Umoja wa Mataifa la Kilimo na Chakula, FAO linasema  kiasi watu milioni 155 walitumbukia kwenye hali ya ukosefu wa chakula mwaka jana, 2020, ikiwa ni ongezeko la hadi watu milioni 20 ikilinganishwa na mwaka kabla ya hapo.

Kilichotajwa kusababisha hali hiyo ni migogoro ya vita, ya kiuchumi na janga la virusi vya corona sambamba na matukio ya hali mbaya ya hewa. Kwa mujibu wa ripoti iliyotolewa na muungano wa mashirika ya kimataifa ya Umoja wa Mataifa, Umoja wa Ulaya, ya kiserikali na yasiyokuwa ya kiserikali, watu katika nchi 55 hawakuwa na chakula cha kutosha kuweza kuendelea kuziweka sawa afya zao katika kipindi cha mwaka 2020.

eco@africa Mali erneuerbare Energien
Picha: DW

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Gutteres akitowa muhtasari wa ripoti hiyo amefahamisha kwamba migogoro ya vita na njaa ni mambo yanayokwenda sambamba na kwa hivyo ulimwengu unahitaji kutafuta ufumbuzi wa masuala yote hayo ili ufanikiwe kupata suluhisho la yote. Gutteres pia ameongeza kusema ulimwengu unapaswa kuchukua hatua zote zinazowezekana kumaliza mzunguko huu na kwamba hakuna nafasi ya kuruhusu ukosefu wa chakula na njaa katika karne ya 21.

Tahadhari

Ripoti imetoa tahadhari kubwa kuhusu hali inayotia wasiwasi ya ukosefu mkubwa wa chakula ambao umekuwa ukiongezeka tangu mwaka 2017. Kwa mujibu wa ripoti hiyo, hali mbaya zaidi imetajwa kuzikabili hasa Burkina Faso, Sudan Kusini na Yemen, wakati pia hali ya wasiwasi mkubwa ikiweko Afghanistan, Syria na Haiti.

Jemen Landwirtschaft Jemenitische Bauern
Picha: Mohammed Huwais/AFP/Getty Images

Aidha ripoti hiyo ya mashirika ya kimataifa imeonya kwamba hali haitarajiwi kuimarika mwaka huu kutokana hasa na vita lakini pia kutokana na hatua zinazochukuliwa zinazofungamana na harakati za kudhibiti janga la Covid-19 ambazo zinachangia ongezeko la hali hiyo. Na ripoti hiyo inakwenda zaidi ikionesha kwamba watu wawili kati ya watatu walioathirika na ukosefu wa chakula mwaka jana walikuwa barani Afrika ingawa sehemu nyingine za dunia pia hazikunusurika.

Kwa ujumla ripoti hiyo inaonesha kwamba watoto wengi wa umri mdogo tayari wameathirika na ukosefu wa vyakula vyenye virurubisho stahiki katika kipindi cha mwanzo kabisa cha ukuaji wao. Imeelezwa kwamba katika nchi 55 zilizoangaliwa kwenye ripoti hiyo kiasi watoto 90 milioni wa chini ya umri wa miaka 5 aidha wana vimo vifupi sana au ni wemekondeana mno.

Mwandishi: Saumu Mwasimba

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo