Mamia ya taarifa binafsi za wanasiasa zadukuliwa Ujerumani | Matukio ya Kisiasa | DW | 04.01.2019
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Mamia ya taarifa binafsi za wanasiasa zadukuliwa Ujerumani

Nyaraka za ndani za vyama vya siasa vya Ujerumani sambamba na taarifa binafsi za wanasiasa zimedukuliwa na kuanikwa kwenye mtandao wa Twitter. Vyama vyote katika bunge la Ujerumani vimeathirika isipokuwa chama cha AfD. 

Kituo cha redio cha umma, RBB, kilichoko mjini Berlin kimeripoti udukuzi wa nyaraka za ndani za vyama na mamia ya taarifa binafsi za wanasiasa na kisha taarifa hizo kuchapishwa kwenye mtandao wa Twitter. Udukuzi huo uliwalenga wanachama kutoka vyama vyote vya siasa ambavyo hivi sasa vina wawakilishi katika bunge la shirikisho, isipokuwa chama cha mrengo mkali wa kulia cha AfD. Wanasiasa pia katika ngazi ya majimbo wote wameathirika.

Msemaji wa chama cha Die Linke amelieleza shirika la habari la Reuters kwamba chama chake ni miongoni mwa waathirika. "Ninathibitisha kwamba kumekuwepo na tukio hilo", amesema msemaji wa Die Linke akiongeza kwamba kiongozi wa kundi la chama Dietmar Bartsch, kwenye bunge la chini ni miongoni mwa walioathirika.

Kuvuja kwa nyaraka hizo, kuligunduliwa kwa mara ya kwanza siku ya Alhamis jioni, kwa mujibu wa kituo cha redio cha RBB. Hata hivyo, nyaraka hizo zinaonekana kwamba ziliwekwa mtandaoni mapema tangu Desemba mwaka jana, katika akaunti ya Twitter iliyoko mjini Hamburg na kisha zikaanza kuachiliwa katika mtindo wa kalenda. Akaunti hiyo ya Twitter imejieleza yenyewe kuhusika na utafiti wa usalama, sanaa na dhihaka.

Symbolbild Cyber Security

Picha inayoonyesha mfano wa shambulio la udukuzi

Taarifa nyingi zilizovuja ni pamoja na anuani na namba za simu. Hata hivyo taarifa nyingi binafsi kama vile taarifa za kibenki na kifedha, vitambulisho na mazungumzo binafsi, barua, vyote hivyo pia vilianikwa mtandaoni. Kati ya nyaraka hizo za ndani zilizovuja, hakuna zilizoripotiwa kuwa na unyeti wa hali ya juu. Zinajumuisha maombi ya kazi, taarifa za vyama, na orodha ya wanachama. Baadhi ya taraifa hizo zilikuwa na zaidi ya mwaka mmoja. Waziri wa sheria wa Ujerumani Katarina Barley amelaani uvujaji wa taarifa binafsi za wanasiasa mtandaoni na kusema kitendo hicho ni kuishambulia demokrasia ya nchi.

"Mhusika wa shambulio anataka kuharibu imani katika demokrasia na taasisi zetu", alisema waziri huyo, akiongeza kwamba wahusika ni lazima watafutwe na kuchukuliwa hatua za kisheria. "Wahalifu na wale wanaowaunga mkono wasiruhusiwe kulazimisha mjadala wowote katika nchi yetu", alimalizia waziri huyo.Hapajawa na uthibitisho ikiwa data hizo zote ni halisi, na nani hasa alihusika na kwa lengo gani. 

Mwandishi: Sylvia Mwehozi/dw/dpa/reuters

Mhariri: Mohammed Khelef