Mamia waachiwa huru na IS Syria | Matukio ya Kisiasa | DW | 14.08.2016
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Mamia waachiwa huru na IS Syria

Wanamgambo wa kundi la Dola la Kiislamu wamewaachia mamia ya raia waliowatumia kama ngao ya binadamu wakati wakiikimbia ngome yao kaskazini mwa Syria,lakini hatima ya wengine haijulikani tangu jana Jumamosi(13.08.2016).

Syrien Manbij Zivilisten

Mwanamke akimkumbatia mpiganaji wa Kikurdi baada ya mji wa Manbij kukombolewa

Katika eneo jingine, raia kadhaa waliuwawa jana Jumamosi katika shambulio la ndege za kijeshi za jeshi la serikali ya Syria pamoja na washirika wao wa Urusi, na katika mashambulizi ya makombora yaliyofanywa na waasi katika eneo la mapigano katika jimbo la Aleppo, limesema kundi linaloangalia hali nchini humo.

Syrien Zivilisten in Manbij

Watoto wakifurahi baada ya mji wa Manbij kukombolewa

Kiasi ya raia 51 ikiwa ni pamoja na watoto waliuwawa mjini Aleppo na linalozunguka mji huo, wakati raia wengine 22 waliuwawa katika jimbo jirani la Idlib, shirika linaloangalia haki za binadamu nchini Syria limesema.

Wapiganaji wa mwisho wa kundi la IS walikimbia kutoka mji wa Manbij karibu na mpaka na Uturuki siku ya Ijumaa baada ya kushambuliwa na wizara ya ulinzi ya Marekani Pentagon kusema inaonekana kuwa wapiganaji hao wenye itikadi kali wamekabwa.

Kukimbia kutoka mji huo ambao ulikamatwa na wapiganaji wa IS mwaka 2014 ilikuwa pigo kubwa kabisa kwa wapiganaji hao wa jihadi kuwahi kutokea dhidi ya vikosi vya Syrian Democratic Forces SDF, muungano wa Wakurdi na Waarabu unaoungwa mkono na mashambulizi ya anga ya Marekani.

Syrien Zivilisten in Manbij

Watu wakishangiria baada ya mji wa Manbij kukombolewa

Ngao ya binadamu

Wapiganaji wanaokimbia waliondoka pamoja na kiasi ya raia 2,000, ikiwa ni pamoja na wanawake na watoto, siku ya Ijumaa kuzuwia mashambulizi ya anga wakati wakielekea katika mji wa mpakani unaoshikiliwa bado na kundi hilo wa Jarabulus, kwa mujibu wa wapiganaji hao wa SDF.

Kiasi ya baadhi ya watu waliochukuliwa na wanamgambo hao baadaye waliachiliwa ama walitoroka, vikosi hivyo vya muungano vilisema jana Jumamosi, lakini haijulikani watu wengine wako wapi.

Syrien Manbij Zivilisten

Akina mama wakitoka nje kufurahia kukombolewa kwa mji wa Manbij kutoka kwa kundi la IS

"Hakuna wapiganaji tena wa IS" waliobakia mjini Manbij, mpiganaji mmoja wa SDF alisema.

Televisheni ya Wakurdi ilionesha picha za raia wakifurahia mjini Manbij, ikiwa ni pamoja na akina mama waliokuwa wakitabasamu, ambao waliondoa hijabu zao na wanawake waliwakumbatia wapiganaji wa Kikurdi.

Mwanamke mmoja alichoma nguo nyeusi ambayo wapiganaji hao wa jihadi waliwalazimisha wakaazi kuvaa, wakati wanaume ambao waliishi kwa wiki kadhaa wakilazimishwa kuacha ndevu zao bila kuzinyoa , walizinyoa.

Mabomu kila nyumba

"Mapambano yalikuwa makali," duru kutoka kwa wakurdi zimezungumza na shirika la habari la afp, na kuongeza wapiganaji wa jihadi waliweka mabomu katika mji huo.

Syrien Manbij Zivilisten

Akina mama katika mji wa Manbij

"Mmoja kati ya wapiganaji wa SDF aliingia katika nyumba siku ya Ijumaa na kuona kiatu kimewekwa juu ya kitabu cha Koran. Alipokiondoa kulikuwa na mripuko na aliuwawa," duru hiyo ilisema.

Mkaazi mmoja aliliambia shirika la habari la afp hakukuwa na hata nyumba moja katika eneo anakoishi ambalo halikutegwa mabomu.

Syrien Manbij Zivilisten

Mpiganaji wa Syria Democratic Forces mjini Manbij akimfariji mkaazi wa mji huo

"Tunawaomba watu wanaohusika kuchukua hatua" ya kuyaondoa mabomu hayo, Jamal Abul Ababiyya alisema, na kuongeza kwamba mabomu yanawajeruhi watu kila siku.

Picha za shirika la habari la afp zinaonesha mitaa ya mji huo ikiwa imetapakaa taka na ukuta bado ukiwa umechorwa bendera ya wapiganaji hao wa jihadi yenye rangi nyeusi na nyeupe.

Mwandishi: Sekione Kitojo/afp

Mhariri: Josephat Charo

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com