1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

David cameron aadhirika

Admin.WagnerD11 Mei 2016

Waziri Mkuu David Cameron amerikodiwa akisema huenda Afghanistan na Nigeria zikawa nchi zilizokithiri katika ufisadi duniani,bila ya yeye mwenyewe kujua kwamba alikuwa anarekodiwa. Malkia pia aliteleza ulimi.

https://p.dw.com/p/1IlYQ
Malkia wa Uingereza Elizabeth II
Malkia wa Uingereza Elizabeth IIPicha: Reuters/S. Wermuth

Waziri Mkuu Cameron alirekodiwa akiyasema hayo wakati alipokuwa anaongea na Askofu Mkuu wa Canterburry Justin Welby na Malkia Elizabeth wa pili, kwenye halfa iliyofanyika kwenye kasri ya Buckingham mjini London.

Bwana Cameron alisema viongozi fulani kutoka nchi zenye ufisadi mkubwa sana wanakuja Uingereza. Waziri Mkuu Cameron atakuwa mwenyeji wa mkutano wa kilele juu ya kupambana na ufisadi utakaofanyika kesho mjini London.

Bila ya kujua kwamba alikuwa anarekodiwa Bwana Cameron alisema huenda Nigeria na Afghanistan zikawa nchi zenye ufisadi mkubwa kabisa duniani.

Rais huyu si fisadi

Hata hivyo Askofu Mkuu wa Canterburry Welby ambae hapo awali alifanya kazi kama Meneja wa kampuni ya mafuta katika Afrika magharibi kabla ya kuwa Askofu, alimwambia Waziri Mkuu Cameron katika maongezi yao "Rais huyu si fisadi".

Mhashamu Welby pia alifanya kazi ya kusuluhisha migogoro nchini Nigeria.Welby alisema kwamba Rais huyo anajitahidi sana. Lakini haikujulikana walikuwa wanazungumzia Rais yupi. Hata hivyo kwa mujibu wa taarifa marais wa Nigeria Muhammadu Buhari na wa Afghanistan Ashraf Ghani pia watahudhuria mkutano wa kesho mjini London.

Askofu Mkuu wa Canterburry Justin Welby
Askofu Mkuu wa Canterburry Justin WelbyPicha: Reuters

Wakati huo huo kwenye hafla nyingine katika kasri ya Buckingham Malkia Elizabeth wa pili nae aliteleza ulimi alipokuwa anaongea na kamanda wa polisi. Alisema maafisa wa China walikuwa wajeuri sana kwa Balozi wa Uingereza:

Malkia Elizabeth wa 2 aliyasema hayo bila ya kujua kwamba alikuwa anarekodiwa. Alikuwa anaongea na kamanda wa polisi Lucy D' orsi baada ya kamanda huyo kutambulishwa kwake.

Kamanda huyo ndiye aliyesimamia usalama wakati wa ziara ya Rais wa China Xi Jinping nchini Uingereza mwezi Oktoba mwaka uliopita.

Mpaka sasa serikali ya China haijasema kitu juu ya mkasa huo na wala vyombo vya habari vya nchi hiyo havijaripoti juu ya mkasa huo. Lakini gazeti la kila siku nchini Uingereza Daily Mail limeikariri kasri ya Buckingham ikisema kuwa haitasema chochote juu ya maongezi ya faragha. Hata hivyo msemaji wa Rais wa Nigeria amesema kauli ya Waziri Mkuu wa Uingereza inafedhehesha.

Msemaji huyo Garba Shehu ameeleza kuwa Waziri Mkuu Cameron bado anaziangalia picha za zamani juu ya Nigeria. Amesema mambo yanabadilika kuhusu ufisadi na kuhusu kila kitu.

Mwandishi:Mtullya Abdu.ape,rtre,

Mhariri: Gakuba Daniel