1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Malkia Elizabeth II ashushwa eneo maalum tayari kwa mazishi

19 Septemba 2022

Uingereza na ulimwengu kwa jumla umemuaga Malkia Elizabeth II wa Uingereza amezikwa Jumatatu mjini London.

https://p.dw.com/p/4H4IB
Queen Eilzabeth II, Staatsbegräbnis
Picha: Hannah McKay/REUTERS

Ibada ya mwisho kabla ya kuzikwa kwa Malkia Elizabeth II ilifanyika katika kanisa la St George kwenye kasri la Winsor. Shughuli hiyo iliongozwa na mkuu wa kanisa hilo David Conner aliyepokea pia ala za kifalme za utawala ikiwemo taji ambazo Malkia Elizabeth alipewa mwanzoni mwa utawala wake. Hadi jeneza lake lilipowasili katika kanisa hilo, ala hizo zilikuwa zimewekwa juu ya jeneza lake.

Taratibu nyingine za mazishi ya kifalme pia zilifuata mfano Mfalme Charles III kupokea kijibendera alichokiweka juu ya jeneza la marehemu.

Nyuso za waliohudhuria mazishi hayo ya kitaifa zilidhihirisha huzuni na majonzi.

Baadaye jeneza la Malkia liliteremshwa taratibu kwenye chumba cha kifalme kabla ya mazishi rasmi yatakayofanywa faraghani na yatahudhuriwa na watu wa familia pekee baadaye.

Mazishi ya aina yake

Jeneza lililoubeba mwili wa Malkia Elizabeth II lilipitishwa katika mitaa kadhaa na misafara kuongozwa na wanajeshi.
Jeneza lililoubeba mwili wa Malkia Elizabeth II lilipitishwa katika mitaa kadhaa na misafara kuongozwa na wanajeshi.Picha: Emilio Morenatti/AP Photo/picture alliance

Ilikuwa mazishi ya kipekee na ya aina yake tangu yale ya kitaifa ya Winston Churchil. Kabla ya misa ya kumuaga, kengele ilipigwa mara 96. Moja kwa kila dakika kuashiria miaka 96 ambayo Malkia Elizabeth II aliishi duniani.

Awali ibada ya kumuaga Elizabeth pia iliandaliwa mapema Jumatatu katika kanisa la Westminster Abbey mjini London ambayo ilihudhuriwa na watu 2,000 wakiwemo takriban wakuu wa nchi 500.

Marais, mawaziri wakuu, wafalme kutoka mataifa mbalimbali ulimwenguni walihudhuria hafla ya kumuaga Malkia Elizabeth II huku mamia kwa maelfu ya watu wakikusanyika mitaani kufuatilia na kushuhudia msafara wa jeneza la Malkia huyo aliyeaga dunia akiwa na miaka 96 na ambaye utawala wake ulidumu kwa miaka 70. 

Mamilioni ya watu walifuatilia mazishi hayo kwenye runinga zao huku maelfu wakikusanyika kwenye bustani na maeneo ya wazi kote Uingereza kutizama hafla hiyo ya kumpa buriani malkia wa uingereza aliyetawala kwa miongo mingi zaidi, ikitangazwa moja kwa moja kwenye televisheni.

Malkia Elizabeth II aliaga akiwa na umri wa miaka 96 na utawala wake ulidumu kwa miaka 70.
Malkia Elizabeth II aliaga akiwa na umri wa miaka 96 na utawala wake ulidumu kwa miaka 70.Picha: Chris Radburn/dpa/picture alliance

Kwenye mahubiri yake katika ibada ya kumuaga malkia, askofu mkuu wa kanisa la Canterbury Justin Welby alisema ni viongozi wachache ambao hupokea mapenzi makubwa kama ambavyo wameshuhudia Malkia Elizabeth II akipata.

"Marehemu Malkia Elizabeth II alitangaza katika sherehe yake ya miaka 21 ya kuzaliwa kwake kwamba alijitolea maisha yake yote kuihudumia nchi na jumuiya ya madola. Ni nadra sana ahadi kama hiyo hutimizwa. Viongozi wachachendio humiminiwa upendo kama ambavyo tumeshuhudia," alisema askofu Justin Welby.

Msafara wa mwili wa Malkia Elizabeth II wapitishwa mitaa ya London

Jeneza lililoubeba mwili wa Malkia lilipitishwa katika mitaa ya London huku baadhi ya waombolezaji wakitupa maua kwenye msafara huo. Hatimaye mwili ulifikishwa katika kasri la Windsor, ambako Malkia Elizabeth II aliishi kwa miaka mingi.

Mamia kwa maelfu ya waombolezaji walijitokeza mitaani na katika maeneo ya wazi kutizama jeneza la Malkia Elizabeth II likipelekwa kwenye kasri la Winsor kwa mazishi.
Mamia kwa maelfu ya waombolezaji walijitokeza mitaani na katika maeneo ya wazi kutizama jeneza la Malkia Elizabeth II likipelekwa kwenye kasri la Winsor kwa mazishi.Picha: Paul Childs/EUTERS

Mwili wa Malkia Elizabeth utazikwa kando ya kaburi la mume wake Mwanamfalme Philip katika hafla ya faragha ambayo inahudhuriwa na familia ya kifalme pamoja na jamaa wa karibu pekee.

Mfalme mpya wa Uingereza Charles III aliwapongeza raia wa Uingereza na ulimwengu mzima akisema yeye pamoja na mke wake Camilla wameguswa kupita kifani na idadi kubwa ya watu waliojitokeza kutoa heshima zao za mwisho kwa malkia.

Mnamo Jumapili saa mbili usiku, watu nchini Uingereza walitulia kwa dakika moja kutoa heshima za mwisho kwa malkia Elizabeth.

Katika mataifa mengine mfano kisiwa cha Hong Kong, waombolezaji walimiminika nje ya ubalozi wa Uingereza kutoa heshima zao  mwisho.

(Ape, Fpe, Rtre)