Mali yaondowa hali ya hatari | Matukio ya Afrika | DW | 06.07.2013
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Afrika

Mali yaondowa hali ya hatari

Mali imeondowa hali ya hatari Jumamosi(06.07.2013) iliokuwa imedumishwa kwa miezi sita nchini humo ili kuruhusu kuanza kwa kampeni ya uchaguzi wa rais uliopangwa kufanyika tarehe 28 mwezi wa Julai.

Wanajeshi wa Mali.

Wanajeshi wa Mali.

Agizo la kuweka muda maalum kwa watu kutoka nje na kupiga marufuku mikusanyiko ya watu lilianza kutumika tarehe 12 Januari siku moja baada ya Ufaransa kufanya shambulio la ghafla la kijeshi kulisaidia jeshi dhaifu la Mali kuwatimuwa wapiganaji wa itikadi kali za Kiislamu waliokuwa wamelidhibiti eneo la kaskazini mwa nchi hiyo kwa miezi tisa.

Hatua hiyo ya mkoloni wa zamani wa Mali ilikuja wakati wanamgambo wa itikadi kali za Kiislamu wenye mafungamano na kundi la Al Qaeda wenye kushikilia miji muhimu ya kaskazani walipokuwa wanasonga mbele kuelekea katika mji mkuu wa Bamako.

Mali ilikuja kutumbukia kwenye mzozo wa kisiasa baada ya mapinduzi ya mwezi wa Machi 2012 yaliofanywa na wanajeshi waliokuwa wamekasirishwa kutokana na kutimuliwa kwao kutoka maeneo ya kaskazini na makundi ya waasi ambapo walimlaumu Rais Amadou Toumani waliyempinduwa kwa kushindwa kwao.

Kuondolewa kwa hali hiyo ya hatari kunakuja baada ya jeshi la Mali hapo Ijumaa kuingia kwa amani katika mji wa mwisho uliokuwa ukishikiliwa na waasi.

Wakiandamana na wanajeshi wa Ufaransa na maafisa wa Umoja wa Mataifa, wanajeshi na wanamgambo 200 wa Mali waliingia katika mji wa Kidal ulioko mbali kaskazini mashariki mwa nchi hiyo.

Waasi wa Tuareg warudi kambini

Waasi wa Tuareg wanaopigania kujitenga kwa jimbo la kaskazini mwa Mali.

Waasi wa Tuareg wanaopigania kujitenga kwa jimbo la kaskazini mwa Mali.

Makundi mawili ya waasi wa kabila la Tuareg waliokuwa wakiudhibiti mji huo tayari wamekubali kubakia kambini na kuweka chini silaha zao wakati wa kipindi cha kampeni za uchaguzi.

Kidal kama vile miji mengine ya kaskazini uliangukia kwenye mikono ya makundi mbali mbali ya waasi hapo mwezi Machi mwaka 2012 na umeendelea kubakia chini ya mikono ya waasi hata baada ya Ufaransa kufanya mashambulizi ya kijeshi kulikomboa eneo la kaskazini kutoka kwa wanamgambo wa itikadi kali za Kiislamu na kufanikiwa kuikomboa miji mengine yote mikubwa.

Waasi wa Tuareg waliingia upya katika mji wa Kidal hapo mwezi wa Februari na Machi mwaka huu na kuweka vizuizi vya barabarani,kutoza kodi wananchi na kuanzisha mamlaka sawa na serikali.

Watu wa kabila la wachache la Tuareg wa kaskazini mwa Mali wamekuwa wakilalamika kwa muda mrefu kwa kupuuzwa na serikali ya Mali na walifanya uasi mara kadhaa katika kipindi cha miongo iliopita wakidai mamlaka ya kujitawala kwa kile wanachokiona kuwa taifa lao.

Hapo Jumamosi watu kadhaa waliandamana mbele ya kambi ya jeshi la Mali kupinga kuingia kwa jeshi hilo katika mji wa Kidal.

Wasi wasi wa uchaguzi

Watu wakiwa katika misururu ya kuchukuwa vitambulisho vya uchaguzi nchini Mali.

Watu wakiwa katika misururu ya kuchukuwa vitambulisho vya uchaguzi nchini Mali.

Watu wengi walikuwa wakijiuliza vipi nchi hiyo inaweza kufanya uchaguzi wake mkuu wakati mji muhimu wa jimbo ukiwa chini ya udhibiti wa waasi na waangalizi wengi wameelezea wasi wasi wao juu ya ugumu wa kufanyika kwa uchaguzi huo mapema.

Usambazaji wa kadi za kupigia kura milioni 7.6 umeanza katika kumbi za miji na shule nchini kote.

Kwa mujibu wa Tume Huru ya Uchaguzi ya Taifa nchini Mali (CENI) takriban wapiga kura watarajiwa milioni 1.1 majina yao yanakosekana katika orodha ya kupiga kura wakiwemo vijana 300,000 wenye umri kati ya miaka 18 na 19.

CENI pia imesema kwamba kwa sababu ya kuhamishwa au kupotezewa makaazi kutokana na vita,takriban watu 800,000 watashindwa kupata kadi zao kutokana na kadi hizo kupelekwa kwenye maeneo ambapo watu walijiandikisha tokea mwaka 2009.

Chama kimoja cha kisiasa kimesema kitafunguwa kesi katika Mahakama ya Katiba hapo Jumatatu kutaka kuahirishwa kwa uchaguzi huo.

Uchaguzi kuhitimisha serikali ya mpito

Rais wa serikali ya mpito nchini Mali Dioncounda Traoré.

Rais wa serikali ya mpito nchini Mali Dioncounda Traoré.

Uchaguzi huo utahitimisha serikali ya mpito iliokuwa madarakani tokea mwezi wa Aprili mwaka 2012 baada ya mapinduzi ya nchi hiyo.

Mahakama ya Katiba nchini Mali hapo Ijumaa ilitoa orodha ya wagombea urais 26 wakiwemo mawaziri wakuu wanne wa zamani na vigogo kadhaa wa kisiasa akiwemo msuluhishi mkuu wa makubaliano ya kusitisha mapigano na waasi wa Tuareg na mwanamke mmoja.

Umoja wa Ulaya tayari umeanza kuweka waangalizi wa uchaguzi nchini Mali kabla ya kuanza kwa uchaguzi huo.

Takriban wanajeshi 3,200 wa Ufaransa bado wako Mali lakini taratibu wamekuwa wakipinguzwa idadi yao ili kuweza kuwabakisha 1,000 kusaidia shughuli za kulinda amani za Umoja wa Mataifa zilizoanza Julai Mosi ambazo hivi sasa zinajumuisha wanajeshi 6,300 wa Afrika.

Mwandishi : Mohamed Dahman/AFP/AP/dpa

Mhariri : Caro Robi