Malawi yapata bendera mpya. | Matukio ya Kisiasa | DW | 18.08.2010
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Malawi yapata bendera mpya.

Bendera mpya ya taifa ya Malawi yenye kuonesha ishara ya kile kilichoelezwa kwamba Wamalawi ''wamezindukana'' tangu nchi hiyo kupata uhuru kutoka kwa Mwingireza miaka 46 iliyopita, imezinduliwa rasmi.

Rais wa malawi Bingu wa Mutharika.

Rais wa malawi Bingu wa Mutharika.

Uzinduzi huo umefanywa na Rais wa nchi hiyo Bingu wa Mutharika wakati wa mkutano wa viongozi wa Jumuia ya Maendeleo ya nchi za kusini mwa Afrika SADC, uliomalizika jana nchini Namibia.

Akizungumza wakati wa mkutano wa kilele wa Jumuia ya Maendeleo ya nchi za kusini mwa Afrika mjini Windhoek, kuhusiana na bendera hiyo mpya ya taifa lake, Rais Bingu wa Mutharika huku akionesha bendera mpya ya Malawi, aliwaambia wajumbe wa mkutano huo kwa sasa, karibu nusu karne ya uhuru wa nchi hiyo, ni muda sasa wa kuionesha dunia kwamba Wamalawi wapatao milioni 14, sasa wamezindukana kikamilifu

Akizungmza kwa mzaha kuhusiana na sura ya bendera ya zamani, Rais Mutharika alisema, ilikuwa ni kama Wamalawi walikuwa wakiishi gizani na kwamba Waingereza wakawaletea mwanga.

Amefafanua kwa kusema kuwa wakati nchi hiyo, ambayo zamani ilikuwa ikifahamika kama Nyasaland ilipopata uhuru wake mwaka 1964, ilikuwa iko nusu gizani, hivyo alama iliyokuwa katika bendera ya taifa ikionesha mapambazuko ya jua , inaashiria kwamba bado wako nusu usingizini.

Kama ilivyo katika bendera ya zamani, bendera mpya ya Malawi ina miraba iliyolala ya rangi, nyekundu, nyeusi na kijani., huku tofauti ikiwa ni alama ya nusu jua lililokuwa katikati katika bendera ya zamani, ikibadilishwa na jua kamili na kwamba alama ya rangi ya nusu jua ambayo ilikuwa nyekundu kwa sasa imebadilishwa na kuwa alama nyeupe ya jua kamili.

Wakati Rais Mutharika akielezea furaha yake kwa mabadiliko hayo ya bendera ya nchi yake kwa viongozi wenziye wa Afrika, serikali yake imekuwa ikibanwa na upinzani na makanisa nchini Malawi, ambao wamekuwa wakilalamika kuwa mabadiliko hayo yamepitishwa bila ya mashauriano ya kutosha.

Aidha Katibu mkuu wa jumuia ya Kiislamu nchini Malawi Imran Sharif Mohammed amesema pia jumuia yao haikushirikishwa kutoa ushairi juu ya mabadiliko hayo.

Wabunge wa upinzani nchini Malawi walitoka nje ya bunge mjini lilongwe siku ya Ijumaa, wakati wabunge ambao wengi ni kutoka chama tawala kinachoongozwa na Rais Mutharika cha Democratic Progressive Party, walipoupigia kura muswada unaounga mkono mabadiliko ya bendera hiyo.

Muswada huo ulipitishwa kwa kura 117 dhidi ya 27 za walioukataa huku kura mbili zikiharibika na kwamba wabunge wengine 42 waliorodheshwa hawakuweko katika kikao hicho.

Wapinzani na wananchi wa kawaida wa malawi wameyapinga mabadiliko hayo kwa kusema kuwa hawaoni uhalali wowote wa kufanya hivyo.

Mwandishi: Halima Nyanza

Mhariri: Abdul-Rahman.

 • Tarehe 18.08.2010
 • Mwandishi Halima Nyanza
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/Oq2W
 • Tarehe 18.08.2010
 • Mwandishi Halima Nyanza
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/Oq2W
Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com